1 Nyakati 15
15
Sanduku la Mungu laletwa Yerusalemu
(2 Samweli 6:12-22)
1Baada ya Daudi kujijengea nyumba zake katika Mji wa Daudi, akatengeneza sehemu kwa ajili ya Sanduku la Mungu, na akasimamisha hema kwa ajili yake. 2Kisha Daudi akasema, “Hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kulibeba Sanduku la Mungu isipokuwa Walawi peke yao, kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwachagua kulibeba Sanduku la Mwenyezi Mungu na kuhudumu mbele zake milele.”
3Daudi akawakusanya Israeli wote huko Yerusalemu ili kulipandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu na kulileta hadi kwenye sehemu aliyokuwa ametengeneza kwa ajili yake.
4Kisha Daudi akawakusanya wazao wa Haruni na Walawi:
5Kutoka wazao wa Kohathi,
Urieli kiongozi na ndugu zake mia moja na ishirini.
6Kutoka wazao wa Merari,
Asaya kiongozi na ndugu zake mia mbili na ishirini.
7Kutoka wazao wa Gershoni#15:7 au Gershomu,
Yoeli kiongozi na ndugu zake mia moja na thelathini.
8Kutoka wazao wa Elisafani,
Shemaya kiongozi na ndugu zake mia mbili.
9Kutoka wazao wa Hebroni,
Elieli kiongozi na ndugu zake themanini.
10Kutoka wazao wa Uzieli,
Aminadabu kiongozi na ndugu zake mia moja na kumi na wawili (112).
11Kisha Daudi akawaita makuhani Sadoki na Abiathari, pamoja na Walawi Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli na Aminadabu. 12Akawaambia, “Ninyi ndio viongozi wa jamaa za Walawi. Ninyi pamoja na Walawi wenzenu inawapasa mjitakase na kulipandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, hadi mahali pale nimetengeneza kwa ajili yake. 13Ilikuwa ni kwa sababu hii, ninyi Walawi, hamkulipandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu mara ya kwanza, hata ikasababisha Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kuwaka hasira dhidi yetu. Hatukumuuliza jinsi ya kufanya ili tupate kulileta jinsi alivyoagiza.” 14Kwa hiyo makuhani pamoja na Walawi wakajitakasa ili kulipandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. 15Nao Walawi wakalichukua Sanduku la Mungu mabegani mwao wakitumia mipiko, kama vile Musa alivyoamuru sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu.
16Daudi akawaambia viongozi wa Walawi wawateue ndugu zao waimbaji ili waimbe nyimbo za shangwe, wakiwa na vyombo vya uimbaji: zeze, vinubi na matoazi.
17Basi Walawi wakawateua Hemani mwana wa Yoeli; kutoka miongoni mwa ndugu zake, Asafu mwana wa Berekia; kutoka miongoni mwa ndugu zao Wamerari, Ethani mwana wa Kushaiya; 18hawa ndio waliochaguliwa kuwa wasaidizi wao: Zekaria, Yaazieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Benaya, Maaseya, Matithia, Elifelehu, Mikneya, pamoja na mabawabu Obed-Edomu na Yehieli.
19Waimbaji Hemani, Asafu na Ethani walichaguliwa kupiga matoazi ya shaba; 20Zekaria, Azieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Maaseya na Benaya walikuwa wapiga zeze kufuatana na sauti ya alamothi#15:20 Huenda ni aina ya uimbaji., 21na Matithia, Elifelehu, Mikneya, Obed-Edomu, Yehieli na Azazia walikuwa wapiga vinubi, wakiongozwa kwa kufuata sauti ya sheminithi#15:21 Huenda ni aina ya uimbaji.. 22Kenania kiongozi wa Walawi alikuwa msimamizi wa uimbaji; huu ndio uliokuwa wajibu wake kwa sababu alikuwa stadi katika hilo.
23Berekia na Elkana walikuwa mabawabu kwa ajili ya Sanduku. 24Shebania, Yoshafati, Nethaneli, Amasai, Zekaria, Benaya na Eliezeri, makuhani, walikuwa wapiga tarumbeta mbele ya Sanduku la Mungu. Obed-Edomu na Yehiya waliwekwa pia kuwa mabawabu wa Sanduku.
25Basi Daudi pamoja na wazee wa Israeli na majemadari wa vikosi vya elfu wakaenda ili kulipandisha Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu kutoka nyumba ya Obed-Edomu kwa shangwe. 26Kwa sababu Mungu alikuwa amewasaidia Walawi waliokuwa wanalichukua Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, mafahali saba na kondoo dume saba walitolewa dhabihu. 27Basi Daudi alikuwa amevaa joho la kitani safi, kama walivyokuwa wamevaa Walawi wote waliokuwa wanalichukua lile Sanduku, waimbaji nao walivaa vivyo hivyo, pamoja na Kenania aliyekuwa anaongoza nyimbo za waimbaji. Daudi alivaa pia kizibau cha kitani safi. 28Hivyo Israeli wote wakalipandisha Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu kwa shangwe, wakipiga pembe za kondoo dume, tarumbeta, na kucheza matoazi, zeze na vinubi.
29Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu lilipokuwa linaingia Mji wa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia dirishani. Naye alipomwona Mfalme Daudi akicheza na kusherehekea, akamdharau moyoni mwake.
Iliyochaguliwa sasa
1 Nyakati 15: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.