1 Wakorintho 7
7
Kuhusu ndoa
1Basi kuhusu mambo yale mliyoyaandika: “Ni vyema mwanaume asimguse mwanamke.” 2Lakini ili kuepuka zinaa, kila mwanaume na awe na mke wake mwenyewe na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe. 3Mume atimize wajibu wake wa ndoa kwa mkewe, naye vivyo hivyo mke kwa mumewe. 4Mwanamke hana mamlaka juu ya mwili wake bali mumewe, wala mume hana mamlaka juu ya mwili wake bali mkewe. 5Msinyimane, isipokuwa mmekubaliana kufanya hivyo kwa muda, ili mweze kujitoa kwa maombi. Kisha mrudiane tena, ili Shetani asije akapata nafasi ya kuwajaribu kwa sababu ya kutokuwa na kiasi. 6Nasema haya kama ushauri na si amri. 7Laiti watu wangekuwa kama mimi nilivyo. Lakini kila mtu amepewa kipawa chake kutoka kwa Mungu, mmoja ana kipawa cha namna hii na mwingine ana cha namna ile.
8Kwa wale wasiooa na kwa wajane, nasema hivi, ingekuwa vizuri wasioe. 9Lakini kama hawawezi kujizuia, basi waoe na kuolewa, kwa maana ni afadhali kuoa au kuolewa kuliko kuwaka tamaa.
10Kwa wale waliooana nawapa amri (si mimi, ila ni Bwana Isa): Mke asitengane na mumewe. 11Lakini akitengana, ni lazima akae bila kuolewa, ama sivyo apatane tena na mumewe. Wala mume asimpe mkewe talaka.
12Lakini kwa wengine nasema (si Bwana Isa, ila ni mimi): Kama ndugu ana mke asiyeamini, naye huyo mke anakubali kuishi pamoja naye, basi asimwache. 13Naye mwanamke aaminiye kama ameolewa na mwanaume asiyeamini na huyo mume anakubali kuishi naye, basi huyo mwanamke asimwache. 14Kwa maana huyo mume asiyeamini anatakaswa kupitia mkewe, naye mke asiyeamini anatakaswa kupitia mumewe anayeamini. Kama haingekuwa hivyo watoto wenu wangakuwa si safi; lakini ilivyo sasa, wao ni watakatifu.
15Lakini kama yule asiyeamini akijitenga, basi afanye hivyo. Katika hali kama hiyo mwanamke au mwanaume aaminiye hafungwi, kwa sababu Mungu ametuita tuishi kwa amani. 16Wewe mke, unajuaje kama utamwokoa mumeo? Au wewe mume, unajuaje kama utamwokoa mkeo?
Kuishi kama alivyoagiza Bwana Isa
17Lakini kila mtu na aishi maisha aliyopangiwa na Bwana Isa, yale Mungu aliyomwitia. Hii ni sheria ninayoiweka kwa makundi yote ya waumini. 18Je, mtu alikuwa tayari ametahiriwa alipoitwa? Asijifanye asiyetahiriwa. Je, mtu alikuwa hajatahiriwa alipoitwa? Asitahiriwe. 19Kutahiriwa si kitu, na kutokutahiriwa si kitu. Lakini kuzitii amri za Mungu ndilo jambo muhimu. 20Basi kila mtu na abaki katika hali aliyoitwa nayo.
21Je, wewe ulipoitwa ulikuwa mtumwa? Jambo hilo lisikusumbue. Ingawaje unaweza kupata uhuru, tumia nafasi uliyo nayo sasa kuliko wakati mwingine wowote. 22Kwa maana yeyote aliyeitwa katika Bwana Isa akiwa mtumwa yeye ni mtu huru kwa Bwana Isa, kama vile yeyote aliyekuwa huru alipoitwa yeye ni mtumwa wa Al-Masihi. 23Mlinunuliwa kwa gharama; msiwe watumwa wa wanadamu. 24Ndugu zangu, kama kila mtu alivyoitwa, akae katika wito wake alioitiwa na Mungu.
Wajane na wasioolewa
25Basi, kuhusu wale walio bikira, mimi sina amri kutoka kwa Bwana Isa, lakini mimi natoa shauri kama mtu ambaye ni mwaminifu kwa rehema za Bwana Isa. 26Kwa sababu ya shida iliyopo sasa, naona ni vyema mkibaki kama mlivyo. 27Je, umeolewa? Basi usitake talaka. Je, hujaoa? Usitafute mke. 28Lakini kama ukioa, hujatenda dhambi; na kama bikira akiolewa, hajatenda dhambi. Lakini wale wanaooa watakabiliana na matatizo mengi katika maisha haya, nami nataka kuwazuilia hayo.
29Lakini ndugu zangu, nina maana kwamba muda uliobaki ni mfupi. Tangu sasa wale waliooa waishi kama wasio na wake; 30nao wanaoomboleza, kama ambao hawaombolezi; wenye furaha kama wasiokuwa nayo; wale wanaonunua, kama vile vitu walivyonunua si mali yao; 31nao wale wanaoshughulika na vitu vya dunia hii, kama ambao hawahusiki navyo. Kwa maana dunia hii kama tunavyoiona sasa inapita.
32Ningetaka msiwe na masumbufu. Mwanaume ambaye hajaoa anajishughulisha na mambo ya Bwana Isa, jinsi ya kumpendeza Bwana Isa. 33Lakini mwanaume aliyeoa anajishughulisha na mambo ya dunia, jinsi ya kumfurahisha mkewe, 34na mawazo yake yamegawanyika. Mwanamke asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana: lengo lake ni awe mtakatifu kimwili na kiroho. Lakini yule aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia, jinsi atakavyoweza kumfurahisha mumewe. 35Ninasema haya kwa faida yenu wenyewe, sio ili kuwawekea vizuizi bali mpate kuishi kwa jinsi ilivyo vyema bila kuvutwa pengine katika kujitoa kwenu kwa Bwana Isa.
36Kama mtu yeyote anadhani kwamba hamtendei ilivyo sawa mwanamwali ambaye amemposa, naye akiwa umri wake unazidi kuendelea na mtu huyo anajisikia kwamba inampasa kuoa, afanye kama atakavyo. Yeye hatendi dhambi. Yawapasa waoane. 37Lakini mwanaume ambaye ameamua moyoni mwake kutooa bila kulazimishwa na mtu yeyote, bali anaweza kuzitawala tamaa zake kutomwoa huyo mwanamwali, basi anafanya ipasavyo. 38Hivyo basi, mwanaume amwoaye mwanamwali afanya vyema, lakini yeye asiyemwoa afanya vyema zaidi.
39Mwanamke aliyeolewa amefungwa na sheria maadamu mumewe yu hai. Lakini mumewe akifa, basi mwanamke huyo yuko huru kuolewa na mume mwingine ampendaye, lakini lazima awe katika Bwana Isa. 40Lakini kwa maoni yangu, angekuwa na furaha zaidi akibaki alivyo. Nami nadhani pia nina Roho wa Mungu.
Iliyochaguliwa sasa
1 Wakorintho 7: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.