Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wakorintho 6

6
Kushtakiana miongoni mwa waumini
1Kama mtu yeyote wa kwenu ana ugomvi na mwenzake, anathubutuje kuupeleka kwa wasiomcha Mungu ili kuamuliwa badala ya kuupeleka kwa watakatifu? 2Je, hamjui kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Nanyi kama mtauhukumu ulimwengu, je, hamwezi kuamua mambo madogo madogo? 3Hamjui kwamba tutawahukumu malaika? Je, si zaidi mambo ya maisha haya? 4Kwa hiyo kama kuna ugomvi miongoni mwenu kuhusu mambo kama haya, je, mnachagua watu ambao wanaonekana hata sio wa heshima katika kundi la waumini kuwa waamuzi kati yenu? 5Nasema hivi ili mwone aibu. Je, inawezekana kuwa miongoni mwenu hakuna mtu mwenye hekima ya kutosha kuamua ugomvi kati ya waumini? 6Badala yake ndugu mmoja anampeleka mwenzake mahakamani, tena mbele ya watu wasioamini!
7Huko kuwa na mashtaka miongoni mwenu ina maana kwamba tayari ni kushindwa kabisa. Kwa nini msikubali kutendewa mabaya? Kwa nini msikubali kunyang’anywa? 8Badala yake, ninyi wenyewe mwadanganya na kutenda mabaya, tena mwawatendea ndugu zenu.
9Je, hamjui kwamba wasio haki hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike: Waasherati, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wahanithi, wala walawiti, 10wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyang’anyi hawataurithi ufalme wa Mungu. 11Baadhi yenu mlikuwa kama hao. Lakini mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki kwa jina la Bwana Isa Al-Masihi na katika Roho wa Mungu wetu.
Dhambi za zinaa
12“Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini si vitu vyote vyenye faida. “Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini sitatawaliwa na kitu chochote. 13“Chakula ni cha tumbo, na tumbo ni la chakula”: lakini Mungu ataviangamiza vyote viwili. Mwili sio kwa ajili ya zinaa, bali kwa ajili ya Bwana Isa, na Bwana Isa kwa ajili ya mwili. 14Naye Mungu aliyemfufua Bwana Isa kutoka kwa wafu atatufufua sisi pia kwa uweza wake. 15Je, hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya Al-Masihi mwenyewe? Je, nichukue viungo vya mwili wa Al-Masihi na kuviunganisha na mwili wa kahaba? La hasha! 16Hamjui kwamba aliyeungwa na kahaba anakuwa mwili mmoja naye? Kwa kuwa imenenwa, “Hao wawili watakuwa mwili mmoja.”#6:16 Mwanzo 2:24 17Lakini mtu aliyeungwa na Bwana Isa anakuwa roho moja naye.
18Ikimbieni zinaa. Dhambi zingine zote atendazo mtu ziko nje ya mwili wake, lakini yeye aziniye hutenda dhambi ndani ya mwili wake mwenyewe. 19Je, hamjui kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu wa Mungu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe, 20kwa maana mmenunuliwa kwa gharama. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu.

Iliyochaguliwa sasa

1 Wakorintho 6: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia