Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 12:1-11

1 Wafalme 12:1-11 NENO

Rehoboamu akaenda Shekemu, kwa kuwa Waisraeli wote walikuwa wameenda huko kumfanya mfalme. Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia hili (alikuwa bado yuko Misri alikokuwa amekimbilia awe mbali na Mfalme Sulemani), akarudi kutoka Misri. Kwa hiyo wakatuma watu kumwita Yeroboamu; yeye na kusanyiko lote la Israeli wakamwendea Rehoboamu na kumwambia, “Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini sasa tupunguzie kazi za kikatili na nira nzito aliyoweka juu yetu, nasi tutakutumikia.” Rehoboamu akajibu, “Nendeni kwa muda wa siku tatu na kisha mnirudie.” Basi watu wakaenda zao. Kisha Mfalme Rehoboamu akataka ushauri kwa wazee ambao walimtumikia Sulemani baba yake wakati wa uhai wake akawauliza, “Mnanishauri niwajibu nini watu hawa?” Wakajibu, “Kama leo utakuwa mtumishi wa watu hawa na kuwahudumia na kuwapa jibu linaloridhisha, watakuwa watumishi wako daima.” Lakini Rehoboamu akakataa ushauri aliopewa na wazee, na akataka ushauri kwa vijana wa rika lake waliokuwa wakimtumikia. Akawauliza, “Ninyi ushauri wenu ni nini? Tutawajibuje watu hawa wanaoniambia, ‘Ifanye nyepesi nira baba yako aliyoweka juu yetu’?” Wale vijana wa rika lake wakamjibu, “Watu hawa walikuambia, ‘Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini ifanye nira yetu nyepesi.’ Wewe waambie, ‘Kidole changu kidogo ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu. Baba yangu aliweka nira nzito juu yenu, mimi nitaifanya hata iwe nzito zaidi. Baba yangu aliwapiga mijeledi; mimi nitawapiga kwa nge.’ ”