1 Wafalme 13:23-34
1 Wafalme 13:23-34 NENO
Huyo mtu wa Mungu alipomaliza kula na kunywa, nabii aliyekuwa amemrudisha akamtandikia punda wake. Alipokuwa akienda akakutana na simba njiani, akamuua na maiti yake ikabwagwa barabarani, huku punda wake na simba wakiwa wamesimama kando yake. Watu waliopita pale, waliona maiti iliyokuwa imebwagwa, simba akiwa amesimama kando yake. Nao wakaenda kutoa habari katika mji ambao nabii mzee alikuwa anaishi. Yule nabii aliyekuwa amemrudisha kutoka safari yake aliposikia habari hii akasema, “Ni yule mtu wa Mungu aliyeliasi neno la Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu amemtoa kwa simba, ambaye amemrarua na kumuua, sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu lilivyokuwa limemwonya.” Nabii akawaambia wanawe, “Nitandikieni punda,” nao wakafanya hivyo. Akaondoka na akakuta maiti imetupwa barabarani, punda na simba wakiwa wamesimama kando yake. Simba hakuwa amekula ile maiti wala kumrarua punda. Basi yule nabii mzee akachukua maiti ya mtu wa Mungu, akailaza juu ya punda na akairudisha katika mji wake, ili amwombolezee na kumzika. Kisha akailaza ile maiti katika kaburi lake huyo nabii mzee, nao wakaomboleza juu yake na kusema, “Ee ndugu yangu!” Baada ya kumzika, akawaambia wanawe, “Nitakapokufa, mnizike kwenye kaburi alimozikwa huyu mtu wa Mungu; lazeni mifupa yangu kando ya mifupa yake. Kwa maana ujumbe alioutangaza kwa neno la Mwenyezi Mungu dhidi ya madhabahu huko Betheli, na dhidi ya nyumba zote za ibada katika mahali pa juu pa kuabudia ndani ya miji ya Samaria, hakika utatimia.” Hata baada ya haya, Yeroboamu hakubadili njia zake mbaya, lakini mara nyingine tena akaweka makuhani kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia kutoka watu wa aina zote. Yeyote aliyetaka kuwa kuhani alimweka wakfu kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia. Hii ilikuwa ndiyo dhambi ya nyumba ya Yeroboamu ambayo iliisababishia kuanguka na kuangamia kwake hadi kutoweka kwenye uso wa dunia.