1 Wafalme 16
16
121 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yehu mwana wa Hanani dhidi ya Baasha, kusema: 2“Nilikuinua kutoka mavumbini na kukufanya mtawala wa watu wangu Israeli, lakini ukaenenda katika njia za Yeroboamu na kusababisha watu wangu Israeli kutenda dhambi na kunikasirisha kwa dhambi zao. 3Basi nitamwangamiza Baasha pamoja na nyumba yake, nami nitaifanya nyumba yako kama ile ya Yeroboamu mwanawe Nebati. 4Mbwa watawala walio wa nyumba ya Baasha watakaofia ndani ya mji, na ndege wa angani watawala wale watakaofia mashambani.”
5Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Baasha, aliyoyafanya na mafanikio yake, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 6Baasha akalala na baba zake naye akazikwa huko Tirsa. Naye Ela mwanawe akawa mfalme baada yake.
7Zaidi ya hayo, neno la Mwenyezi Mungu likamjia Baasha pamoja na nyumba yake kupitia kwa nabii Yehu mwana wa Hanani, kwa sababu ya maovu yote aliyokuwa ametenda machoni pa Mwenyezi Mungu, akimkasirisha kwa mambo aliyotenda, na kuwa kama nyumba ya Yeroboamu aliyoiangamiza.
Ela mfalme wa Israeli
8Katika mwaka wa ishirini na sita wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ela mwana wa Baasha akawa mfalme wa Israeli, naye akatawala huko Tirsa kwa miaka miwili.
9Zimri, mmoja wa maafisa wake, aliyekuwa na amri juu ya nusu ya magari yake ya vita, akapanga njama dhidi ya Ela. Wakati huo Ela alikuwa Tirsa, akilewa katika nyumba ya Arsa, aliyekuwa msimamizi wa jumba la kifalme huko Tirsa. 10Zimri akaingia, akampiga na kumuua katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda. Kisha Zimri akawa mfalme baada yake.
11Mara tu alipoanza kutawala na kukalia kiti chake cha kifalme, aliua jamaa yote ya Baasha. Hakumwacha mwanaume hata mmoja, akiwa ni ndugu au rafiki. 12Hivyo, Zimri akawaangamiza jamaa yote ya Baasha, kama Mwenyezi Mungu alivyonena dhidi ya Baasha kupitia kwa nabii Yehu: 13kwa sababu ya dhambi zote Baasha na mwanawe Ela walizokuwa wametenda na wakasababisha Israeli kuzitenda, basi wakamkasirisha Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kwa sanamu zao batili.
14Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Ela, na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
Zimri mfalme wa Israeli
15Katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Zimri akatawala huko Tirsa siku saba. Jeshi lilikuwa limepiga kambi karibu na Gibethoni, mji wa Wafilisti. 16Waisraeli waliokuwa kambini waliposikia kuwa Zimri amepanga njama ya kumuua mfalme, wakamtangaza Omri, jemadari wa jeshi, kuwa mfalme wa Israeli yote siku hiyo hiyo huko kambini. 17Ndipo Omri na Waisraeli wote pamoja naye wakaondoka Gibethoni na kuizingira Tirsa. 18Zimri alipoona kuwa mji umechukuliwa, alienda ndani ya ngome ya jumba la kifalme na kulichoma moto hilo jumba na kujiteketeza ndani yake. Kwa hiyo akafa, 19kwa sababu ya dhambi alizotenda, akifanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu na kuenenda katika njia za Yeroboamu na katika dhambi alizotenda na kusababisha Israeli kuzifanya.
20Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Zimri, na uasi alioutenda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
Omri mfalme wa Israeli
21Kisha, watu wa Israeli wakagawanyika katika makundi mawili, nusu wakamuunga mkono Tibni mwana wa Ginathi ili awe mfalme, na nusu nyingine wakamuunga mkono Omri. 22Lakini wafuasi wa Omri wakajionesha kuwa wenye nguvu kuliko wale wa Tibni, mwana wa Ginathi. Hivyo Tibni akafa, na Omri akawa mfalme.
23Katika mwaka wa thelathini na moja wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Omri akawa mfalme wa Israeli, naye akatawala kwa miaka kumi na mbili, sita kati ya hiyo katika Tirsa. 24Alinunua kilima cha Samaria kutoka kwa Shemeri kwa talanta mbili#16:24 Talanta 2 za fedha ni sawa na kilo 70. za fedha na akajenga mji juu ya hicho kilima, akiuita Samaria, kutokana na Shemeri, jina la mmiliki wa kwanza wa kilima hicho.
25Lakini Omri akatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu na kutenda dhambi kuliko wote waliomtangulia. 26Akaenenda katika njia zote za Yeroboamu mwana wa Nebati na katika dhambi zake, ambazo alisababisha Israeli kutenda, hivyo basi wakamkasirisha Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kwa sanamu zao batili.
27Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Omri, yale aliyofanya na mafanikio aliyokuwa nayo, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 28Omri akalala na baba zake, akazikwa huko Samaria. Naye Ahabu mwanawe akawa mfalme baada yake.
Ahabu afanywa mfalme wa Israeli
29Katika mwaka wa thelathini na nane wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ahabu mwana wa Omri akawa mfalme wa Israeli, naye akatawala Israeli akiwa Samaria kwa miaka ishirini na mbili. 30Ahabu mwana wa Omri akafanya maovu zaidi machoni pa Mwenyezi Mungu kuliko yeyote aliyemtangulia. 31Kama vile haikutosha kuishi kama Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, naye akaanza kumtumikia Baali na kumwabudu. 32Akatengeneza madhabahu kwa ajili ya Baali katika hekalu la Baali alilolijenga huko Samaria. 33Pia Ahabu alitengeneza nguzo ya Ashera na kufanya mengi ili kumkasirisha Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kuliko walivyofanya wafalme wote wa Israeli waliomtangulia.
34Wakati wa Ahabu, Hieli ule Mbetheli, akaijenga Yeriko upya. Aliweka misingi yake kwa gharama ya mzaliwa wake wa kwanza Abiramu, na kuweka malango yake kwa gharama ya mwanawe mdogo Segubu, kama Mwenyezi Mungu alivyonena kupitia kwa Yoshua, mwana wa Nuni.
Iliyochaguliwa sasa
1 Wafalme 16: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.