1 Wafalme 19:15-21
1 Wafalme 19:15-21 NENO
Mwenyezi Mungu akamwambia, “Rudi kwa njia uliyoijia, uende kwenye Jangwa la Dameski. Utakapofika huko, mpake Hazaeli mafuta awe mfalme wa Aramu. Pia mpake mafuta Yehu, mwana wa Nimshi awe mfalme wa Israeli, na umpake mafuta Al-Yasa mwana wa Shafati kutoka Abel-Mehola awe nabii baada yako. Yehu atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Hazaeli, naye Al-Yasa atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Yehu. Hata sasa nimeweka akiba ya watu elfu saba katika Israeli, wote ambao hawajampigia Baali magoti, na wote ambao midomo yao haijambusu.” Hivyo Ilya akaondoka huko na kumkuta Al-Yasa mwana wa Shafati. Alikuwa akilima kwa jozi kumi na mbili za maksai, na yeye mwenyewe aliiongoza ile jozi ya kumi na mbili. Ilya akamwendea, na kumvisha vazi lake. Kisha Al-Yasa akawaacha maksai wake, akamkimbilia Ilya, akamwambia, “Niruhusu nikawabusu baba yangu na mama yangu, halafu nitafuatana nawe.” Ilya akajibu, “Rudi zako, kwani nimekufanya nini?” Basi Al-Yasa akamwacha Ilya, naye akarudi. Akachukua ile jozi yake ya maksai na kuwachinja. Akaipika ile nyama kwa kutumia miti ya nira kama kuni na kuwapa watu, nao wakala. Kisha akaondoka, akamfuata Ilya, akamtumikia.