1 Wafalme 21:1-16
1 Wafalme 21:1-16 NENO
Baada ya hayo, pakawa na tukio lililohusisha shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli. Shamba hilo lilikuwa Yezreeli, karibu na jumba la kifalme la Ahabu, mfalme wa Samaria. Ahabu akamwambia Nabothi, “Nipe shamba lako la mizabibu liwe langu, nilime bustani ya mboga kwa kuwa liko karibu na jumba langu. Nitakupa shamba jingine la mizabibu lililo zuri zaidi, au kama utapenda, nitakulipa kulingana na thamani ya shamba lako.” Lakini Nabothi akamjibu, “Mwenyezi Mungu na apishe mbali kukupa wewe urithi wa baba zangu.” Basi Ahabu akaenda nyumbani kwa uchungu na hasira kwa sababu Nabothi Myezreeli alikuwa amemwambia, “Sitakupa urithi wa baba zangu.” Akajinyoosha juu ya kitanda akisononeka, na akakataa kula. Yezebeli mke wake akaingia na akamuuliza, “Kwa nini unahuzunika hivi? Kwa nini huli chakula?” Akamjibu, “Kwa sababu nilimwambia Nabothi Myezreeli, ‘Niuzie shamba lako la mizabibu, au ukipenda, nitakupa shamba jingine la mizabibu badala yake.’ Lakini akasema, ‘Sitakupa shamba langu la mizabibu.’ ” Yezebeli mke wake akamuuliza, “Hivi ndivyo unavyofanya, nawe ni mfalme wa Israeli yote? Inuka na ule! Changamka. Nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli.” Kwa hiyo akaandika barua kwa jina la Ahabu, akaweka muhuri wa Ahabu juu ya hizo barua; kisha akazituma kwa wazee na kwa watu wenye vyeo walioishi na Nabothi katika mji wake. Katika barua hizo aliandika: “Tangazeni siku ya watu kufunga, na mkamketishe Nabothi mbele ya watu. Waketisheni walaghai wawili mkabala naye, nao washuhudie dhidi yake kuwa amemlaani Mungu na mfalme pia. Kisha mtoeni nje na kumpiga kwa mawe hadi afe.” Hivyo wazee na watu wenye vyeo walioishi katika mji wa Nabothi wakafanya kama Yezebeli alivyoelekeza katika barua alizowaandikia. Wakatangaza mfungo na kumketisha Nabothi mbele ya watu. Kisha walaghai wawili wakaja wakaketi mkabala naye; nao wakaleta mashtaka dhidi ya Nabothi mbele ya watu, wakisema, “Nabothi amemlaani Mungu na mfalme pia.” Kwa hiyo wakamtoa nje na kumpiga kwa mawe hadi akafa. Kisha wakatuma ujumbe kwa Yezebeli, kusema, “Nabothi amepigwa mawe na amekufa.” Mara tu Yezebeli aliposikia kwamba Nabothi amepigwa mawe na amekufa, akamwambia Ahabu, “Amka na umiliki lile shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ambalo alikataa kukuuzia. Hayuko hai tena, bali amekufa.” Ahabu aliposikia Nabothi amekufa, akainuka, kisha akashuka kwenda kulimiliki shamba la mizabibu la Nabothi.