Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 21

21
Shamba la mizabibu la Nabothi
1Baada ya hayo, pakawa na tukio lililohusisha shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli. Shamba hilo lilikuwa Yezreeli, karibu na jumba la kifalme la Ahabu, mfalme wa Samaria. 2Ahabu akamwambia Nabothi, “Nipe shamba lako la mizabibu liwe langu, nilime bustani ya mboga kwa kuwa liko karibu na jumba langu. Nitakupa shamba jingine la mizabibu lililo zuri zaidi, au kama utapenda, nitakulipa kulingana na thamani ya shamba lako.”
3Lakini Nabothi akamjibu, “Mwenyezi Mungu na apishe mbali kukupa wewe urithi wa baba zangu.”
4Basi Ahabu akaenda nyumbani kwa uchungu na hasira kwa sababu Nabothi Myezreeli alikuwa amemwambia, “Sitakupa urithi wa baba zangu.” Akajinyoosha juu ya kitanda akisononeka, na akakataa kula.
5Yezebeli mke wake akaingia na akamuuliza, “Kwa nini unahuzunika hivi? Kwa nini huli chakula?”
6Akamjibu, “Kwa sababu nilimwambia Nabothi Myezreeli, ‘Niuzie shamba lako la mizabibu, au ukipenda, nitakupa shamba jingine la mizabibu badala yake.’ Lakini akasema, ‘Sitakupa shamba langu la mizabibu.’ ”
7Yezebeli mke wake akamuuliza, “Hivi ndivyo unavyofanya, nawe ni mfalme wa Israeli yote? Inuka na ule! Changamka. Nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli.”
8Kwa hiyo akaandika barua kwa jina la Ahabu, akaweka muhuri wa Ahabu juu ya hizo barua; kisha akazituma kwa wazee na kwa watu wenye vyeo walioishi na Nabothi katika mji wake. 9Katika barua hizo aliandika:
“Tangazeni siku ya watu kufunga, na mkamketishe Nabothi mbele ya watu. 10Waketisheni walaghai wawili mkabala naye, nao washuhudie dhidi yake kuwa amemlaani Mungu na mfalme pia. Kisha mtoeni nje na kumpiga kwa mawe hadi afe.”
11Hivyo wazee na watu wenye vyeo walioishi katika mji wa Nabothi wakafanya kama Yezebeli alivyoelekeza katika barua alizowaandikia. 12Wakatangaza mfungo na kumketisha Nabothi mbele ya watu. 13Kisha walaghai wawili wakaja wakaketi mkabala naye; nao wakaleta mashtaka dhidi ya Nabothi mbele ya watu, wakisema, “Nabothi amemlaani Mungu na mfalme pia.” Kwa hiyo wakamtoa nje na kumpiga kwa mawe hadi akafa. 14Kisha wakatuma ujumbe kwa Yezebeli, kusema, “Nabothi amepigwa mawe na amekufa.”
15Mara tu Yezebeli aliposikia kwamba Nabothi amepigwa mawe na amekufa, akamwambia Ahabu, “Amka na umiliki lile shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ambalo alikataa kukuuzia. Hayuko hai tena, bali amekufa.” 16Ahabu aliposikia Nabothi amekufa, akainuka, kisha akashuka kwenda kulimiliki shamba la mizabibu la Nabothi.
17Kisha neno la Mwenyezi Mungu likamjia Ilya Mtishbi, kusema: 18“Shuka ukakutane na Ahabu mfalme wa Israeli, anayetawala Samaria. Sasa yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ambalo ameenda kulimiliki. 19Umwambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Je, hujamuua mtu na kuitwaa mali yake?’ Kisha umwambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Mahali mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba damu yako pia; naam, yako wewe!’ ”
20Ahabu akamwambia Ilya, “Kwa hiyo umenipata, wewe adui yangu!”
Akajibu, “Ndiyo, nimekupata. Kwa sababu umejiuza mwenyewe kwa kufanya uovu mbele za macho ya Mwenyezi Mungu. 21‘Nitaleta maafa juu yako. Nitaangamiza uzao wako na kukatilia mbali kila mwanaume wa jamaa ya Ahabu katika Israeli, awe mtumwa au mtu huru. 22Nitaifanya nyumba yako kuwa kama ile ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa sababu umenighadhibisha kwa kusababisha Israeli kutenda dhambi.’
23“Pia Mwenyezi Mungu anasema kumhusu Yezebeli: ‘Mbwa watamla Yezebeli karibu na ukuta wa Yezreeli.’
24“Mbwa watawala wale wa nyumba ya Ahabu watakaofia mjini, nao wale watakaofia mashambani wataliwa na ndege wa angani.”
25(Hapajapata kamwe kuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza mwenyewe kutenda uovu machoni pa Mwenyezi Mungu, akiwa anachochewa na Yezebeli mkewe. 26Alitenda uovu sana kwa kuzifuata sanamu, kama Waamori ambao Mwenyezi Mungu aliowafukuza mbele ya Israeli.)
27Ahabu aliposikia maneno haya, akararua nguo zake, akavaa gunia na kufunga. Akalala na kujifunika gunia na kwenda kwa unyenyekevu.
28Ndipo neno la Mwenyezi Mungu lilipomjia Ilya Mtishbi kusema, 29“Umeona jinsi Ahabu alivyojinyenyekeza mbele zangu? Kwa kuwa amejishusha mwenyewe, sitaleta maafa haya wakati akiwa hai, lakini nitayaleta juu ya nyumba yake katika siku za mwanawe.”

Iliyochaguliwa sasa

1 Wafalme 21: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia