1 Wafalme 22
22
Mikaya atabiri dhidi ya Ahabu
(2 Nyakati 18:2-27)
1Kwa miaka mitatu hapakuwa na vita kati ya Aramu na Israeli. 2Lakini katika mwaka wa tatu, Yehoshafati mfalme wa Yuda akateremka kwenda kumwona mfalme wa Israeli. 3Mfalme wa Israeli alikuwa amewaambia maafisa wake, “Je, hamjui Ramoth-Gileadi ni mali yetu, na bado hatufanyi chochote kuirudisha kwetu kutoka kwa mfalme wa Aramu?”
4Kwa hiyo akamuuliza Yehoshafati, “Je, utaenda pamoja nami kupigana dhidi ya Ramoth-Gileadi?”
Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako.” 5Lakini Yehoshafati pia akamwambia mfalme wa Israeli, “Kwanza tafuta ushauri wa Mwenyezi Mungu.”
6Kwa hiyo mfalme wa Israeli akawaleta pamoja manabii, wanaume wapatao mia nne, akawauliza, “Je, niende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi, au niache?”
Wakajibu, “Naam, nenda, kwa kuwa Bwana ataiweka Ramoth-Gileadi mkononi mwa mfalme.”
7Lakini Yehoshafati akauliza, “Je, hayuko nabii wa Mwenyezi Mungu hapa ambaye tunaweza kumuuliza?”
8Mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Bado yupo mtu mmoja ambaye kupitia kwake twaweza kuuliza ushauri wa Mwenyezi Mungu, lakini namchukia kwa sababu hatabiri jambo lolote jema kunihusu, ila hunitabiria mabaya kila mara. Yeye ni Mikaya mwana wa Imla.”
Yehoshafati akajibu, “Mfalme hapaswi kusema hivyo.”
9Kwa hiyo mfalme wa Israeli akamwita mmoja wa maafisa wake na kusema, “Mlete Mikaya mwana wa Imla mara moja.”
10Wakiwa wamevalia majoho yao ya kifalme, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wameketi juu ya viti vyao vya kifalme katika sakafu ya kupuria, kwenye ingilio la lango la Samaria, huku manabii wote wakitabiri mbele yao. 11Wakati huu Sedekia mwana wa Kenaana alikuwa ametengeneza pembe za chuma. Naye akatangaza, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, ‘Kwa hizi pembe utawapiga Waaramu hadi waangamizwe.’ ”
12Manabii wengine wote walikuwa wanatabiri kitu hicho hicho wakisema, “Ishambulie Ramoth-Gileadi na uwe mshindi. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ataitia mkononi mwa mfalme.”
13Mjumbe aliyekuwa ameenda kumwita Mikaya akamwambia, “Tazama, manabii wote kama mtu mmoja wanatabiri ushindi kwa mfalme. Neno lako na likubaliane na lao, nawe unene mema kuhusu mfalme.”
14Lakini Mikaya akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, nitamwambia kile tu Mwenyezi Mungu atakachoniambia.”
15Alipofika, mfalme akamuuliza, “Mikaya, je, twende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi au niache?”
Akamjibu, “Shambulia na ushinde, kwa kuwa Mwenyezi Mungu atawatia mkononi mwa mfalme.”
16Mfalme akamwambia, “Je, ni mara ngapi nitakuapisha ili usiniambie kitu chochote ila kweli tu kwa jina la Mwenyezi Mungu?”
17Ndipo Mikaya akajibu, “Niliona Israeli wote wametawanyika vilimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye Mwenyezi Mungu akasema, ‘Watu hawa hawana kiongozi. Mwache kila mmoja aende nyumbani kwa amani.’ ”
18Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kwamba huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu, ila mabaya tu?”
19Mikaya akaendelea, “Kwa hiyo lisikie neno la Mwenyezi Mungu: Nilimwona Mwenyezi Mungu ameketi kwenye kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni likiwa limesimama kumzunguka upande wa kulia na wa kushoto. 20Naye Mwenyezi Mungu akasema, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu ili aishambulie Ramoth-Gileadi na kukiendea kifo chake huko?’
“Mmoja akapendekeza hili na mwingine lile. 21Hatimaye, pepo mchafu akajitokeza, akasimama mbele za Mwenyezi Mungu na kusema, ‘Nitamshawishi.’
22“Mwenyezi Mungu akauliza, ‘Kwa njia gani?’
“Akasema, ‘Nitaenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote.’
“Mwenyezi Mungu akasema, ‘Utafanikiwa katika kumshawishi. Nenda ukafanye hivyo.’
23“Kwa hiyo sasa Mwenyezi Mungu ameweka roho ya kudanganya ndani ya vinywa vya hawa manabii wako wote. Mwenyezi Mungu ameamuru maafa kwa ajili yako.”
24Kisha Sedekia mwana wa Kenaana akatoka na kumpiga Mikaya kofi usoni. Akauliza, “Huyo Roho kutoka kwa Mwenyezi Mungu alipita njia gani alipotoka kwangu ili kusema nawe?”
25Mikaya akajibu, “Utagundua siku hiyo utakapoenda kujificha kwenye chumba cha ndani.”
26Kisha mfalme wa Israeli akaagiza, “Mchukueni Mikaya, mkamrudishe kwa Amoni mtawala wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme. 27Mkaseme, ‘Hivi ndivyo asemavyo mfalme: Mwekeni mtu huyu gerezani na asipewe chochote ila mkate na maji hadi nitakaporudi salama.’ ”
28Mikaya akasema, “Kama utarudi salama, basi Mwenyezi Mungu hajanena kupitia kwangu.” Kisha akaongeza kusema, “Zingatieni maneno yangu, enyi watu wote!”
Ahabu auawa huko Ramoth-Gileadi
(2 Nyakati 18:28-34)
29Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakaenda Ramoth-Gileadi. 30Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Nitaingia vitani nikiwa nimejibadilisha, lakini wewe uvae majoho yako ya kifalme.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akajibadilisha na kwenda vitani.
31Wakati huu, mfalme wa Aramu alikuwa amewaagiza majemadari thelathini na wawili wa magari ya vita, “Msipigane na yeyote, mdogo au mkubwa, isipokuwa mfalme wa Israeli.” 32Wale majemadari wa magari ya vita walipomwona Yehoshafati wakafikiri, “Hakika huyu ndiye mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo wakageuka ili wamshambulie, lakini Yehoshafati alipopiga kelele, 33wale majemadari wakaona kwamba hakuwa mfalme wa Israeli, wakaacha kumfuatilia.
34Lakini mtu mmoja akavuta upinde pasipo lengo na kumpiga mfalme wa Israeli katikati ya kiungio cha mavazi yake ya chuma. Mfalme akamwambia mwendesha gari lake la vita, “Geuza gari na uniondoe katika mapigano, nimejeruhiwa.” 35Vita vikaendelea mchana kutwa, naye Mfalme Ahabu akategemezwa ndani ya gari lake la vita kuelekea Waaramu. Damu kutoka jeraha lake ikatiririka ndani ya gari lake, na jioni yake akafa. 36Jua lilipokuwa linazama, mbiu ikaenea katika jeshi lote: “Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake!”
37Basi mfalme akafa na akaletwa Samaria, nao wakamzika huko. 38Wakasafisha lile gari la vita katika bwawa la Samaria (mahali makahaba walipooga), na mbwa wakaramba damu yake, sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu lilivyokuwa limesema.
39Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Ahabu, pamoja na yote aliyoyafanya, jumba la kifalme alilojenga na kupambwa kwa pembe za ndovu, nayo miji aliyoijengea ngome, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 40Ahabu akalala na baba zake. Naye Ahazia mwanawe akawa mfalme baada yake.
Yehoshafati mfalme wa Yuda
(2 Nyakati 20:31–21:1)
41Yehoshafati mwana wa Asa akawa mfalme wa Yuda katika mwaka wa nne wa Ahabu mfalme wa Israeli. 42Yehoshafati alikuwa na umri wa miaka thelathini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka ishirini na tano. Mama yake aliitwa Azuba binti Shilhi. 43Katika kila jambo alitembea katika njia za Asa baba yake wala hakuenda kinyume chake. Alifanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu. Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko. 44Yehoshafati pia alikuwa na amani na mfalme wa Israeli.
45Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehoshafati, mafanikio aliyokuwa nayo na uhodari wake katika vita, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 46Aliondolea mbali katika nchi mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu waliobaki huko hata baada ya utawala wa baba yake Asa. 47Wakati ule, hakukuwa na mfalme katika Edomu; naibu ndiye alitawala.
48Wakati huu Yehoshafati akaunda merikebu nyingi za biashara#22:48 au za Tarshishi (taz. 1 Wafalme 10:22; 2 Nyakati 9:21; 20:36; Isaya 2:16; 60:9). ili kwenda Ofiri kuchukua dhahabu; lakini kamwe hazikusafiri, kwa maana zilivunjikia huko Esion-Geberi. 49Wakati ule, Ahazia mwana wa Ahabu akamwambia Yehoshafati, “Waache watu wangu wasafiri baharini pamoja na watu wako,” lakini Yehoshafati akakataa.
50Kisha Yehoshafati akalala na baba zake, akazikwa pamoja nao katika mji wa Daudi baba yake. Yehoramu mwanawe akawa mfalme baada yake.
Ahazia mfalme wa Israeli
51Ahazia mwana wa Ahabu akawa mfalme wa Israeli huko Samaria katika mwaka wa kumi na saba wa Yehoshafati mfalme wa Yuda. Naye akatawala katika Israeli kwa miaka miwili. 52Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu kwa sababu alienenda katika njia za baba yake na mama yake na katika njia za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye alisababisha Israeli itende dhambi. 53Alimtumikia na kumwabudu Baali na kumghadhibisha Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kama vile baba yake alivyokuwa amefanya.
Iliyochaguliwa sasa
1 Wafalme 22: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.