Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 22:13-28

1 Wafalme 22:13-28 NENO

Mjumbe aliyekuwa ameenda kumwita Mikaya akamwambia, “Tazama, manabii wote kama mtu mmoja wanatabiri ushindi kwa mfalme. Neno lako na likubaliane na lao, nawe unene mema kuhusu mfalme.” Lakini Mikaya akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, nitamwambia kile tu Mwenyezi Mungu atakachoniambia.” Alipofika, mfalme akamuuliza, “Mikaya, je, twende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi au niache?” Akamjibu, “Shambulia na ushinde, kwa kuwa Mwenyezi Mungu atawatia mkononi mwa mfalme.” Mfalme akamwambia, “Je, ni mara ngapi nitakuapisha ili usiniambie kitu chochote ila kweli tu kwa jina la Mwenyezi Mungu?” Ndipo Mikaya akajibu, “Niliona Israeli wote wametawanyika vilimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye Mwenyezi Mungu akasema, ‘Watu hawa hawana kiongozi. Mwache kila mmoja aende nyumbani kwa amani.’ ” Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kwamba huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu, ila mabaya tu?” Mikaya akaendelea, “Kwa hiyo lisikie neno la Mwenyezi Mungu: Nilimwona Mwenyezi Mungu ameketi kwenye kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni likiwa limesimama kumzunguka upande wa kulia na wa kushoto. Naye Mwenyezi Mungu akasema, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu ili aishambulie Ramoth-Gileadi na kukiendea kifo chake huko?’ “Mmoja akapendekeza hili na mwingine lile. Hatimaye, pepo mchafu akajitokeza, akasimama mbele za Mwenyezi Mungu na kusema, ‘Nitamshawishi.’ “Mwenyezi Mungu akauliza, ‘Kwa njia gani?’ “Akasema, ‘Nitaenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote.’ “Mwenyezi Mungu akasema, ‘Utafanikiwa katika kumshawishi. Nenda ukafanye hivyo.’ “Kwa hiyo sasa Mwenyezi Mungu ameweka roho ya kudanganya ndani ya vinywa vya hawa manabii wako wote. Mwenyezi Mungu ameamuru maafa kwa ajili yako.” Kisha Sedekia mwana wa Kenaana akatoka na kumpiga Mikaya kofi usoni. Akauliza, “Huyo Roho kutoka kwa Mwenyezi Mungu alipita njia gani alipotoka kwangu ili kusema nawe?” Mikaya akajibu, “Utagundua siku hiyo utakapoenda kujificha kwenye chumba cha ndani.” Kisha mfalme wa Israeli akaagiza, “Mchukueni Mikaya, mkamrudishe kwa Amoni mtawala wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme. Mkaseme, ‘Hivi ndivyo asemavyo mfalme: Mwekeni mtu huyu gerezani na asipewe chochote ila mkate na maji hadi nitakaporudi salama.’ ” Mikaya akasema, “Kama utarudi salama, basi Mwenyezi Mungu hajanena kupitia kwangu.” Kisha akaongeza kusema, “Zingatieni maneno yangu, enyi watu wote!”