1 Wafalme 22:29-40
1 Wafalme 22:29-40 NEN
Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakaenda Ramoth-Gileadi. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Nitaingia vitani nikiwa nimejibadilisha, lakini wewe uvae majoho yako ya kifalme.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akajibadilisha na kwenda vitani. Wakati huu, mfalme wa Aramu alikuwa amewaagiza majemadari thelathini na wawili wa magari ya vita, “Msipigane na yeyote, mdogo au mkubwa, isipokuwa mfalme wa Israeli.” Wakati wale majemadari wa magari ya vita walipomwona Yehoshafati wakafikiri, “Hakika huyu ndiye mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo wakageuka ili wamshambulie, lakini Yehoshafati akapiga kelele, wale majemadari wakaona kwamba hakuwa mfalme wa Israeli, nao wakaacha kumfuatilia. Lakini mtu fulani akavuta upinde pasipo lengo na kumpiga mfalme wa Israeli katikati ya kiungio cha mavazi yake ya chuma. Mfalme akamwambia mwendesha gari lake, “Geuza gari na uniondoe mimi katika mapigano, nimejeruhiwa.” Vita vikaendelea mchana kutwa, naye Mfalme Ahabu akategemezwa ndani ya gari kuelekea Waaramu. Damu kutoka kwenye jeraha lake ikachuruzika ndani ya gari na jioni yake akafa. Jua lilipokuwa linazama, mbiu ikaenea katika jeshi lote: “Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake!” Basi mfalme akafa na akaletwa Samaria, nao wakamzika huko. Wakasafisha lile gari la vita katika bwawa la Samaria (mahali makahaba walipooga), na mbwa wakaramba damu yake, sawasawa na neno la BWANA lilivyokuwa limesema. Kwa matukio mengine ya utawala wa Ahabu, pamoja na yote aliyoyafanya, jumba la kifalme alilojenga na kupambwa kwa pembe za ndovu, nayo miji aliyoijengea maboma, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? Ahabu akalala pamoja na baba zake. Naye Ahazia mwanawe akawa mfalme baada yake.