Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 3:1-15

1 Wafalme 3:1-15 NENO

Sulemani akafanya mapatano na Mfalme Farao wa Misri na akamwoa binti yake. Akamleta huyo binti Farao katika Mji wa Daudi hadi alipomaliza kujenga jumba lake la kifalme na Hekalu la Mwenyezi Mungu, pamoja na ukuta kuzunguka Yerusalemu. Hata hivyo, watu bado walikuwa wakitoa dhabihu huko kwenye mahali pa juu pa kuabudia, kwa sababu Hekalu lilikuwa bado halijajengwa kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu. Sulemani akaonesha upendo wake kwa Mwenyezi Mungu kwa kuenenda sawasawa na amri za Daudi baba yake, ila yeye alitoa dhabihu na kufukiza uvumba huko mahali pa juu pa kuabudia. Mfalme akaenda Gibeoni kutoa dhabihu, kwa maana ndipo palipokuwa mahali pa juu pa kuabudia pakuu, naye Sulemani akatoa sadaka elfu moja za kuteketezwa juu ya hayo madhabahu. Mwenyezi Mungu akamtokea Sulemani huko Gibeoni wakati wa usiku katika ndoto, naye Mungu akasema, “Omba lolote utakalo nikupe.” Sulemani akajibu, “Umemfanyia mtumishi wako, baba yangu Daudi, fadhili nyingi, kwa kuwa alikuwa mwaminifu kwako na mwenye haki, tena mnyofu wa moyo. Nawe umemzidishia fadhili hii kuu kwani umempa mwana wa kuketi kwenye kiti chake cha ufalme, kama ilivyo leo. “Sasa, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, umemfanya mtumishi wako mfalme mahali pa baba yangu Daudi. Lakini mimi ni mtoto mdogo tu, wala sijui jinsi ya kutekeleza wajibu wangu. Mtumishi wako yuko hapa miongoni mwa watu uliowachagua: taifa kubwa, watu wengi wasioweza kuhesabika wala kutoa idadi yao. Hivyo mpe mtumishi wako moyo wa ufahamu ili kutawala watu wako na kupambanua kati ya mema na mabaya. Kwa maana, ni nani awezaye kutawala watu wako hawa walio wengi hivi?” Bwana akapendezwa kwamba Sulemani ameliomba jambo hili. Basi Mungu akamwambia, “Kwa kuwa umeomba neno hili na hukuomba maisha marefu au upate utajiri kwa nafsi yako, wala adui zako wafe, bali umeomba busara katika kutoa haki, nitafanya uliloomba. Nitakupa moyo wa hekima na wa ufahamu, kiasi kwamba hajakuwa mtu mwingine kama wewe, wala kamwe hatakuwa baada yako. Zaidi ya hayo, nitakupa yale ambayo hukuomba: utajiri na heshima; siku za maisha yako yote hapatakuwa na mtu kama wewe miongoni mwa wafalme. Nawe ukienenda katika njia zangu na kutii sheria na amri zangu vile baba yako Daudi alivyofanya, nitakupa maisha marefu.” Ndipo Sulemani akaamka, akatambua kuwa ilikuwa ndoto. Akarudi Yerusalemu, akasimama mbele ya Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, naye akatoa dhabihu za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha akawafanyia watumishi wake wote karamu.