Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 6:19-38

1 Wafalme 6:19-38 NENO

Ndani ya Hekalu akatengeneza mahali patakatifu pa kuliweka Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu. Mahali patakatifu palikuwa na urefu wa dhiraa ishirini, upana wa dhiraa ishirini, na kimo cha dhiraa ishirini. Akapafunika upande wa ndani, na madhabahu ya mwerezi pia, kwa dhahabu safi. Sulemani akalifunika Hekalu upande wa ndani kwa dhahabu safi, na akaitandaza mikufu ya dhahabu kutoka upande mmoja hadi ule mwingine mbele ya mahali patakatifu, palipofunikwa kwa dhahabu. Basi akafunika upande wote wa ndani kwa dhahabu. Pia akafunika kwa dhahabu yale madhabahu yaliyokuwa ndani ya mahali patakatifu. Katika mahali patakatifu, akatengeneza makerubi wawili kwa mzeituni, kila moja likiwa na dhiraa kumi kwenda juu. Bawa moja la kerubi wa kwanza lilikuwa na urefu wa dhiraa tano na bawa jingine dhiraa tano, hivyo urefu kutoka ncha ya bawa moja hadi ncha ya bawa jingine ulikuwa dhiraa kumi. Kerubi wa pili alikuwa na urefu wa dhiraa kumi pia, kwa kuwa makerubi hao wawili walifanana kwa vipimo na kwa umbo. Kimo cha kila kerubi kilikuwa dhiraa kumi. Aliwaweka makerubi hao katika chumba cha ndani kabisa cha Hekalu, mabawa yao yakiwa yamekunjuliwa. Bawa la kerubi mmoja liligusa ukuta mmoja, wakati bawa la yule mwingine liligusa ukuta wa upande mwingine, nayo mabawa yao mengine yaligusana katikati ya chumba. Akafunika wale makerubi kwa dhahabu. Kuta zote za Hekalu, za vyumba vya ndani na vya nje, zilipambwa kwa nakshi za makerubi, mitende na maua yaliyochanua. Pia alifunika sakafu zote za vyumba vya ndani na vya nje vya Hekalu kwa dhahabu. Katika ingilio la mahali patakatifu sana, alitengeneza milango ya mbao za mzeituni, yenye miimo ya sehemu moja ya tano ya upana wa madhabahu. Kwenye milango hiyo miwili ya mbao za mzeituni, alinakshi makerubi, mitende, pamoja na maua yaliyochanua, na kufunika makerubi na mitende kwa dhahabu iliyofuliwa. Kwa namna hiyo hiyo, alitengeneza miimo kwa mbao za mzeituni yenye upana wa robo ya upana wa ukumbi mkuu kwa ajili ya ingilio la ukumbi huo. Pia akatengeneza milango miwili kwa mbao za msunobari, kila mmoja ukiwa na vipande viwili ambavyo vilikunjwa kwa bawaba. Akanakshi makerubi, mitende na maua yaliyochanua juu yake, na kufunika kwa dhahabu iliyonyoshwa vizuri juu ya michoro. Tena akajenga ua wa ndani safu tatu za mawe yaliyochongwa, na safu moja ya boriti za mwerezi zilizosawazishwa. Msingi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu uliwekwa katika mwaka wa nne, katika mwezi wa Zivu. Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, Hekalu lilikamilika katika hatua zake zote kwa kufuatana na maelekezo yake Sulemani. Alilijenga kwa miaka saba.