Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 6:19-38

1 Wafalme 6:19-38 Biblia Habari Njema (BHN)

Katika sehemu ya ndani kabisa ya jengo hilo, Solomoni alitayarisha chumba cha pekee ambamo sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu liliwekwa. Chumba hicho kilikuwa na urefu wa mita 9, upana wa mita 9, na kimo cha mita 9; nacho kilipambwa kwa dhahabu safi. Pia, alitengeneza madhabahu kwa mbao za mierezi. Solomoni aliipamba kwa dhahabu safi sehemu ya ndani ya nyumba, na mbele ya hicho chumba cha ndani akaweka minyororo ya dhahabu kutoka upande mmoja mpaka upande wa pili, aliipamba kwa dhahabu. Nyumba yote aliipamba kwa dhahabu, na madhabahu iliyokuwa katika chumba cha ndani kabisa. Alitengeneza kwa mbao za mizeituni sanamu za viumbe wawili wenye mabawa, kila sanamu ikiwa na kimo cha mita 4.5, akaziweka katika chumba cha ndani kabisa. Kila bawa lilikuwa na urefu wa mita 2.5; kwa hiyo urefu kutoka ncha ya bawa moja mpaka ncha ya bawa lingine ulikuwa mita 4.5. Kiumbe mwingine alikuwa na urefu wa mita 4.5; viumbe wote wawili walikuwa na vipimo vilevile na umbo lilelile. Urefu wa kiumbe mmoja ulikuwa mita 4.5; pia urefu wa kiumbe mwingine ulikuwa uleule. Sanamu hizo zilikuwa sambamba, zikiwa na mabawa yaliyokunjuliwa: Bawa la mmoja likigusa ukuta mmoja, na bawa la mwingine likigusa ukuta wa pili, huku yale mengine yaligusana katikati ya chumba. Nazo sanamu hizo alizipamba kwa dhahabu. Kuta za kila chumba alizipamba kwa kuchongwa michoro ya viumbe wenye mabawa, mitende na michoro ya maua yaliyochanua. Aliipaka dhahabu sakafu ya vyumba vya ndani na vya nje. Kwa kuingia chumba cha ndani kabisa alitengeneza milango kwa mbao za mizeituni. Vizingiti na miimo ya milango vilifanya umbo la pembe tano. Katika milango hiyo miwili ya mizeituni, alichora viumbe wenye mabawa, mitende na maua yaliyochanua; akaipamba michoro hiyo kwa dhahabu. Hali kadhalika, alitengeneza mlango wa mraba wa kuingia sebuleni. Miimo ya mlango huo ilikuwa ya mizeituni, na mabamba yake mawili yalikuwa ya miberoshi; kila bamba liliweza kukunjwa mara moja. Juu ya mabamba hayo ya mlango, kulichorwa viumbe wenye mabawa, mitende na maua yaliyochanua; akaipamba vizuri michoro hiyo kwa dhahabu. Alijenga ukumbi wa ndani ambao kuta zake zilikuwa za tabaka tatu za mawe yaliyochongwa, na tabaka moja la boriti za mwerezi. Msingi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu ulijengwa mnamo mwezi wa Zifu katika mwaka wa nne. Na katika mwezi wa Buli, yaani mwezi wa nane, katika mwaka wa kumi na mmoja, ujenzi wa nyumba ulimalizika, na kazi ilikuwa imekamilika kama ilivyopangwa. Ujenzi huo ulimchukua Solomoni miaka saba.

1 Wafalme 6:19-38 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Akaweka tayari chumba cha ndani katikati ya nyumba ndani, ili atie humo sanduku la Agano la BWANA. Na ndani yake chumba hicho cha ndani mlikuwa na nafasi, mikono ishirini urefu, na mikono ishirini upana, na mikono ishirini kwenda juu kwake; akaifunika na dhahabu safi. Akaifunika madhabahu nayo kwa mwerezi. Hivyo Sulemani akaifunika nyumba ndani kwa dhahabu safi. Akaitenga kwa mikufu ya dhahabu mbele ya chumba cha ndani; akapafunika na dhahabu. Akaifunika nyumba yote kwa dhahabu, hata ilipokwisha nyumba yote; tena madhabahu yote iliyokuwa ya chumba cha ndani akaifunika kwa dhahabu. Akafanya ndani ya chumba cha ndani makerubi mawili ya mzeituni, kwenda juu mikono kumi. Na bawa moja la kerubi lilikuwa mikono mitano urefu wake, na bawa la pili la kerubi mikono mitano; mikono kumi toka mwisho wa bawa moja hata mwisho wa bawa la pili. Na kerubi la pili lilikuwa mikono kumi; makerubi yote mawili walikuwa ya cheo kimoja na namna moja. Kwenda juu kwake kerubi moja kulikuwa mikono kumi, na kerubi la pili vivyo hivyo. Akayaweka hayo makerubi katika nyumba ya ndani; na mabawa ya makerubi yakanyoshwa, bawa la moja likafika ukutani huko, na bawa la kerubi la pili likafika ukutani huko; mabawa yao yakagusana katikati ya nyumba. Akayafunika makerubi kwa dhahabu. Akazinakshi kuta zote za nyumba kwa nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, pande za ndani na nje. Na sakafu ya nyumba akaifunika na dhahabu ndani na nje. Akayafanyia maingilio ya chumba cha ndani milango ya mzeituni; kizingiti na miimo ilikuwa ya pande tano. Hivyo akafanya milango miwili ya mzeituni; akanakshi juu yake nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, akaifunika kwa dhahabu; akatia dhahabu juu ya makerubi, na juu ya mitende. Ndivyo alivyoyafanyia maingilio ya hekalu miimo ya mzeituni, yenye pande nne; na milango miwili ya mberoshi; mbao mbili za mlango mmoja zilikuwa za kukunjana, na mbao mbili za mlango wa pili za kukunjana. Akanakshi juu yake makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi; akazifunika kwa dhahabu iliyonyoshwa juu ya machoro. Akaijengea behewa ya ndani safu tatu za mawe ya kuchongwa, na safu moja ya mihimili ya mierezi. Katika mwaka wa nne nyumba ya BWANA ilitiwa msingi, katika mwezi wa Zivu. Na katika mwaka wa kumi na mmoja, katika mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, nyumba ikaisha, mambo yake yote, kulingana na kanuni zote. Basi muda wa miaka saba alikuwa katika kuijenga.

1 Wafalme 6:19-38 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Akaweka tayari chumba cha ndani katikati ya nyumba ndani, ili atie humo sanduku la agano la BWANA. Na ndani yake chumba hicho cha ndani mlikuwa na nafasi, mikono ishirini urefu, na mikono ishirini upana, na mikono ishirini kwenda juu kwake; akaifunika na dhahabu safi. Akaifunika madhabahu nayo kwa mwerezi. Hivyo Sulemani akaifunika nyumba ndani kwa dhahabu safi. Akaitenga kwa mikufu ya dhahabu mbele ya chumba cha ndani; akapafunika na dhahabu. Akaifunika nyumba yote kwa dhahabu, hata ilipokwisha nyumba yote; tena madhabahu yote iliyokuwa ya chumba cha ndani akaifunika kwa dhahabu. Akafanya ndani ya chumba cha ndani makerubi mawili ya mzeituni, kwenda juu mikono kumi. Na bawa moja la kerubi lilikuwa mikono mitano urefu wake, na bawa la pili la kerubi mikono mitano; mikono kumi toka mwisho wa bawa moja hata mwisho wa bawa la pili. Na kerubi la pili lilikuwa mikono kumi; makerubi yote mawili walikuwa ya cheo kimoja na namna moja. Kwenda juu kwake kerubi moja kulikuwa mikono kumi, na kerubi la pili vivyo. Akayaweka hayo makerubi katika nyumba ya ndani; na mabawa ya makerubi yakanyoshwa, bawa la moja likafika ukutani huko, na bawa la kerubi la pili likafika ukutani huko; mabawa yao yakagusana katikati ya nyumba. Akayafunika makerubi kwa dhahabu. Akazinakshi kuta zote za nyumba kwa nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, pande za ndani na nje. Na sakafu ya nyumba akaifunika na dhahabu ndani na nje. Akayafanyia maingilio ya chumba cha ndani milango ya mzeituni; kizingiti na miimo ilikuwa ya pande tano. Hivyo akafanya milango miwili ya mzeituni; akanakshi juu yake nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, akaifunika kwa dhahabu; akatia dhahabu juu ya makerubi, na juu ya mitende. Ndivyo alivyoyafanyia maingilio ya hekalu miimo ya mzeituni, yenye pande nne; na milango miwili ya mberoshi; mbao mbili za mlango mmoja zilikuwa za kukunjana, na mbao mbili za mlango wa pili za kukunjana. Akanakshi juu yake makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi; akazifunika kwa dhahabu iliyonyoshwa juu ya machoro. Akaijengea behewa ya ndani safu tatu za mawe ya kuchongwa, na safu moja ya mihimili ya mierezi. Katika mwaka wa nne nyumba ya BWANA ilitiwa msingi, katika mwezi wa Zivu. Hata katika mwaka wa kumi na mmoja, katika mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, nyumba ikaisha, mambo yake yote, na sharti zake zote. Basi muda wa miaka saba alikuwa katika kuijenga.

1 Wafalme 6:19-38 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Ndani ya Hekalu akatengeneza mahali patakatifu pa kuliweka Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu. Mahali patakatifu palikuwa na urefu wa dhiraa ishirini, upana wa dhiraa ishirini, na kimo cha dhiraa ishirini. Akapafunika upande wa ndani, na madhabahu ya mwerezi pia, kwa dhahabu safi. Sulemani akalifunika Hekalu upande wa ndani kwa dhahabu safi, na akaitandaza mikufu ya dhahabu kutoka upande mmoja hadi ule mwingine mbele ya mahali patakatifu, palipofunikwa kwa dhahabu. Basi akafunika upande wote wa ndani kwa dhahabu. Pia akafunika kwa dhahabu yale madhabahu yaliyokuwa ndani ya mahali patakatifu. Katika mahali patakatifu, akatengeneza makerubi wawili kwa mzeituni, kila moja likiwa na dhiraa kumi kwenda juu. Bawa moja la kerubi wa kwanza lilikuwa na urefu wa dhiraa tano na bawa jingine dhiraa tano, hivyo urefu kutoka ncha ya bawa moja hadi ncha ya bawa jingine ulikuwa dhiraa kumi. Kerubi wa pili alikuwa na urefu wa dhiraa kumi pia, kwa kuwa makerubi hao wawili walifanana kwa vipimo na kwa umbo. Kimo cha kila kerubi kilikuwa dhiraa kumi. Aliwaweka makerubi hao katika chumba cha ndani kabisa cha Hekalu, mabawa yao yakiwa yamekunjuliwa. Bawa la kerubi mmoja liligusa ukuta mmoja, wakati bawa la yule mwingine liligusa ukuta wa upande mwingine, nayo mabawa yao mengine yaligusana katikati ya chumba. Akafunika wale makerubi kwa dhahabu. Kuta zote za Hekalu, za vyumba vya ndani na vya nje, zilipambwa kwa nakshi za makerubi, mitende na maua yaliyochanua. Pia alifunika sakafu zote za vyumba vya ndani na vya nje vya Hekalu kwa dhahabu. Katika ingilio la mahali patakatifu sana, alitengeneza milango ya mbao za mzeituni, yenye miimo ya sehemu moja ya tano ya upana wa madhabahu. Kwenye milango hiyo miwili ya mbao za mzeituni, alinakshi makerubi, mitende, pamoja na maua yaliyochanua, na kufunika makerubi na mitende kwa dhahabu iliyofuliwa. Kwa namna hiyo hiyo, alitengeneza miimo kwa mbao za mzeituni yenye upana wa robo ya upana wa ukumbi mkuu kwa ajili ya ingilio la ukumbi huo. Pia akatengeneza milango miwili kwa mbao za msunobari, kila mmoja ukiwa na vipande viwili ambavyo vilikunjwa kwa bawaba. Akanakshi makerubi, mitende na maua yaliyochanua juu yake, na kufunika kwa dhahabu iliyonyoshwa vizuri juu ya michoro. Tena akajenga ua wa ndani safu tatu za mawe yaliyochongwa, na safu moja ya boriti za mwerezi zilizosawazishwa. Msingi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu uliwekwa katika mwaka wa nne, katika mwezi wa Zivu. Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, Hekalu lilikamilika katika hatua zake zote kwa kufuatana na maelekezo yake Sulemani. Alilijenga kwa miaka saba.