Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 21

21
Daudi huko Nobu
1Daudi akaenda Nobu, kwa Ahimeleki kuhani. Ahimeleki akatetemeka alipokutana naye, akamuuliza, “Kwa nini uko peke yako? Kwa nini hukufuatana na mtu yeyote?”
2Daudi akamjibu Ahimeleki kuhani, akisema, “Mfalme ameniagiza shughuli fulani na kuniambia, ‘Mtu yeyote asijue chochote kuhusu kazi niliyokutuma kuifanya, wala maagizo niliyokupa!’ Kuhusu watu wangu, nimewaambia mahali pa kukutana. 3Sasa basi, una nini mkononi? Nipatie mikate mitano au chochote unachoweza kupata.”
4Lakini kuhani akamjibu Daudi, “Sina mkate wowote wa kawaida kwa sasa. Hata hivyo, ipo hapa mikate iliyowekwa wakfu, iwapo watu wamejitenga na wanawake.”
5Daudi akajibu, “Hakika tumejitenga na wanawake kwa siku hizi chache kama kawaida ya ninapotoka kwenda kwenye shughuli. Navyo vyombo vya wale vijana huwa ni vitakatifu hata kwenye safari ya kawaida, si zaidi sana leo vyombo vyao vitakuwa ni vitakatifu?” 6Hivyo kuhani akampa ile mikate iliyowekwa wakfu, kwa kuwa hapakuwa na mikate mingine isipokuwa hiyo ya Wonesho, iliyokuwa imeondolewa hapo mbele za Mwenyezi Mungu na kubadilishwa na mingine yenye moto siku ile ilipoondolewa.
7Basi siku hiyo palikuwepo mmoja wa watumishi wa Sauli, aliyezuiliwa mbele za Mwenyezi Mungu; alikuwa Doegi Mwedomu, kiongozi wa wachungaji wa Sauli.
8Daudi akamuuliza Ahimeleki, “Je, unao mkuki au upanga hapa? Sikuleta upanga wala silaha nyingine yoyote, kwa sababu shughuli ya mfalme ilikuwa ya haraka.”
9Kuhani akajibu, “Upanga wa Goliathi Mfilisti, ambaye ulimuua katika Bonde la Ela, upo hapa, umefungwa katika kitambaa nyuma ya kizibau. Kama unauhitaji, uchukue, hakuna upanga mwingine hapa ila huo tu.”
Daudi akasema, “Hakuna upanga mwingine kama huo. Nipatie huo.”
Daudi huko Gathi
10Siku ile Daudi akamkimbia Sauli na kwenda kwa Akishi mfalme wa Gathi. 11Nao watumishi wa Akishi wakamwambia, “Je, huyu si ndiye Daudi mfalme wa nchi? Je, huyu si ndiye yule ambaye wanaimba katika ngoma zao wakisema:
“ ‘Sauli amewaua elfu zake,
naye Daudi makumi elfu yake’?”
12Daudi akayaweka maneno haya moyoni naye akamwogopa sana Akishi mfalme wa Gathi. 13Basi akajifanya mwendawazimu mbele yao; naye alipokuwa mikononi mwao, alitenda kama kichaa, akikwaruza kwa kutia alama juu ya milango ya lango, na kuachia mate kutiririka kwenye ndevu zake.
14Akishi akawaambia watumishi wake, “Tazameni mtu huyu! Ana wazimu! Kwa nini mnamleta kwangu? 15Je, mimi nimepungukiwa na wenda wazimu kiasi kwamba mmeniletea mtu huyo hapa aendelee kufanya hivi mbele yangu? Je, ilikuwa ni lazima mtu huyo aje nyumbani mwangu?”

Iliyochaguliwa sasa

1 Samweli 21: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia