1 Samweli 22
22
Daudi akiwa Adulamu na Mispa
1Daudi akaondoka Gathi na kukimbilia kwenye pango la Adulamu. Ndugu zake na watu wa nyumba ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko. 2Wale wote waliokuwa katika dhiki au waliokuwa na madeni au wale ambao hawakuridhika wakamkusanyikia Daudi, naye akawa kiongozi wao. Watu wapatao mia nne walikuwa naye.
3Kutoka huko Daudi akaenda Mispa iliyoko Moabu na kumwambia mfalme wa Moabu, “Naomba uwaruhusu baba yangu na mama yangu waje kukaa nawe hadi nijue nini Mungu atakachonifanyia.” 4Hivyo akawaacha wazazi wake wakae na mfalme wa Moabu, nao wakakaa naye muda wote ambao Daudi alikuwa ngomeni.
5Ndipo nabii Gadi akamwambia Daudi, “Usikae ngomeni. Nenda katika nchi ya Yuda.” Hivyo Daudi akaondoka na kwenda katika msitu wa Herethi.
Sauli awaua makuhani wa Nobu
6Basi Sauli akasikia kwamba Daudi na watu wake wameonekana. Sauli akiwa na mkuki mkononi, alikuwa ameketi chini ya mti wa mkwaju kwenye kilima huko Gibea, maafisa wake wote wakiwa wamesimama kumzunguka. 7Sauli akawaambia, “Sikilizeni enyi Wabenyamini! Je, mwana wa Yese atawapa ninyi nyote mashamba na mashamba ya mizabibu? Je, atawafanya ninyi nyote majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia? 8Je, ndiyo sababu ninyi mkapanga hila mbaya dhidi yangu? Hakuna hata mmoja wenu ambaye ameniambia ni lini mwanangu alifanya agano na mwana wa Yese. Hapana hata mmoja wenu anayejishughulisha nami wala anayeniambia kwamba mwanangu amechochea mtumishi wangu kunivizia, kama afanyavyo leo.”
9Lakini Doegi Mwedomu, aliyekuwa akisimama na maafisa wa Sauli, akasema, “Nilimwona mwana wa Yese akija kwa Ahimeleki mwana wa Ahitubu huko Nobu. 10Ahimeleki akamuuliza Mwenyezi Mungu kwa ajili yake; pia akampa vyakula na ule upanga wa Goliathi Mfilisti.”
11Kisha mfalme akatuma watu wamwite kuhani Ahimeleki mwana wa Ahitubu, na jamaa yote ya baba yake, waliokuwa makuhani huko Nobu, nao wote wakaja kwa mfalme. 12Sauli akasema, “Sikiliza sasa, mwana wa Ahitubu.”
Akajibu, “Naam, bwana wangu.”
13Sauli akamwambia, “Kwa nini umepanga njama dhidi yangu, wewe na mwana wa Yese, ukampa vyakula na upanga, tena, ulimuuliza Mungu kwa ajili yake na kwa sababu hiyo ameasi dhidi yangu na kunivizia, kama afanyavyo leo?”
14Ahimeleki akamjibu mfalme, “Ni nani miongoni mwa watumishi wako wote aliye mwaminifu kama Daudi, mkwewe mfalme, kiongozi wa walinzi wako na anayeheshimika sana katika watu wa nyumbani mwako? 15Je, siku hiyo ilikuwa ndiyo ya kwanza kumwomba Mungu kwa ajili yake? La hasha! Mfalme na usiwashutumu watumishi wako wala yeyote wa jamaa ya baba yake, kwa kuwa mtumishi wako hafahamu lolote kabisa kuhusu jambo hili lote.”
16Lakini mfalme akasema, “Ahimeleki, hakika utakufa, wewe na jamaa yote ya baba yako.”
17Ndipo mfalme akawaamuru walinzi wake waliokuwa kando yake: “Geukeni na kuwaua makuhani wa Mwenyezi Mungu, kwa sababu nao pia wamejiunga na Daudi. Walijua kuwa alikuwa anakimbia, wala hawakuniambia.”
Lakini maafisa wa mfalme hawakuwa radhi kuinua mkono kuwaua makuhani wa Mwenyezi Mungu.
18Kisha mfalme akamwagiza Doegi, “Wewe geuka ukawaue makuhani.” Hivyo basi Doegi Mwedomu, akageuka na kuwaua. Siku ile aliwaua watu themanini na watano waliovaa vizibau vya kitani. 19Pia akaupiga Nobu, mji wa makuhani kwa upanga, wakiwemo wanaume na wanawake, watoto na wale watoto wanaonyonya, ng’ombe, punda na kondoo wake.
20Lakini Abiathari, mwana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, akatoroka, akakimbia na kujiunga na Daudi. 21Abiathari akamwambia Daudi kuwa Sauli amewaua makuhani wa Mwenyezi Mungu. 22Kisha Daudi akamwambia Abiathari: “Siku ile Doegi Mwedomu alipokuwa pale, nilijua atahakikisha amemwambia Sauli kuwa mimi ninawajibika kwa vifo vya jamaa yote ya baba yako. 23Kaa pamoja nami; usiogope. Mtu anayeutafuta uhai wako anautafuta uhai wangu pia. Ukiwa pamoja nami utakuwa salama.”
Iliyochaguliwa sasa
1 Samweli 22: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.