2 Wakorintho 10:12-18
2 Wakorintho 10:12-18 NENO
Hatuthubutu kujiweka kwenye kundi moja au kujilinganisha na hao wanaojitukuza wenyewe kuwa wao ni wa maana sana. Wanapojipima na kujilinganisha wenyewe kwa wenyewe, wanaonesha ya kuwa hawana busara. Lakini sisi hatujajivuna kupita kiasi, bali majivuno yetu yatakuwa katika mipaka ya huduma ile Mungu aliyotuwekea, mipaka ambayo inawafikia hata ninyi. Kwa maana hatukuwa tunavuka mipaka katika kujisifu kwetu, kama ambavyo ingekuwa tusingekuja kwenu. Kwa maana sisi ndio tuliokuwa wa kwanza kuja kwenu na Injili ya Al-Masihi. Wala hatuvuki mipaka kwa kujisifu kwetu kwa ajili ya kazi iliyofanywa na watu wengine. Tumaini letu ni kwamba imani yenu inavyozidi kukua, ndivyo eneo letu la utendaji miongoni mwenu litapanuka zaidi, ili tuweze kuhubiri Injili sehemu zilizo mbali na maeneo yenu. Kwa maana hatutaki kujisifu kwa ajili ya kazi ambayo imekwisha kufanyika tayari katika eneo la mtu mwingine. Lakini, “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Mwenyezi Mungu.” Kwa maana si yeye ajisifuye mwenyewe akubaliwaye, bali yeye ambaye Mwenyezi Mungu humsifu.