2 Wakorintho 10:12-18
2 Wakorintho 10:12-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa vyovyote hatungethubutu kujiweka au kujilinganisha na wale watu wanaojisifia wenyewe. Watu wenye kujifanya wao kuwa kipimo cha kujipimia, na watu wanaojilinganisha wenyewe kwa wenyewe, ni wapumbavu. Lakini sisi hatutajivuna kupita kiasi; kujivuna huko kutabaki katika kile kipimo cha kazi aliyotukabidhi Mungu, kazi ambayo tunaifanya pia kwenu. Hatukuruka mipaka tuliyowekewa wakati tulipokuja kwenu. Sisi tulikuwa wa kwanza kuja kwenu tukiwaleteeni Habari Njema juu ya Kristo. Basi, hatujivunii kazi waliyofanya wengine zaidi ya kipimo tulichopewa; ila tunatumaini kwamba imani yenu itazidi miongoni mwenu kufuatana na kipimo alichotuwekea Mungu. Hapo tutaweza kuihubiri Habari Njema katika nchi nyingine, mbali nanyi; na haitakuwa shauri la kujivunia kazi waliyofanya watu wengine mahali pengine. Lakini kama yasemavyo Maandiko: “Mwenye kujivuna na ajivunie kazi ya Bwana.” Anayekubaliwa si yule anayejisifu mwenyewe, bali yule anayesifiwa na Bwana.
2 Wakorintho 10:12-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa kuwa hatuthubutu kujihesabu pamoja na baadhi yao wanaojisifu wenyewe, wala kujilinganisha nao; lakini wanapojipima wenyewe kwa wenyewe na kujilinganisha wenyewe kwa wenyewe, hawaonekani kuwa na ufahamu mwema. Lakini sisi hatutajisifu zaidi ya kadiri yetu; bali kwa kadiri ya kipimo tulichopimiwa na Mungu, yaani, kadiri ya kufika hata kwenu. Maana hatujitanui nafsi zetu kupita kadiri yetu, kana kwamba hatuwafikii ninyi; kwa sababu tulitangulia kufika mpaka kwenu katika Injili ya Kristo; wala hatujisifu zaidi ya kadiri yetu, yaani, katika taabu za watu wengine; bali tukiwa na tumaini ya kwamba, imani yenu ikuapo, tutakuzwa kwenu kwa kadiri ya kipimo chetu, na kupata ziada; hata kuihubiri Injili katika nchi zilizo mbele kupita nchi zenu; tusijisifu katika kipimo cha mtu mwingine kwa mambo yaliyokwisha kutengenezwa. Lakini, Yeye ajisifuye, na ajisifu katika Bwana. Maana mtu mwenye kukubaliwa si yeye ajisifuye, bali yeye asifiwaye na Bwana.
2 Wakorintho 10:12-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa kuwa hatuthubutu kujihesabu pamoja na baadhi yao wanaojisifu wenyewe, wala kujilinganisha nao; bali wao wenyewe wakijipima nafsi zao na nafsi zao, na wakijilinganisha nafsi zao na nafsi zao, hawana akili. Lakini sisi hatutajisifu zaidi ya kadiri yetu; bali kwa kadiri ya kipimo tulichopimiwa na Mungu, yaani, kadiri ya kufika hata kwenu. Maana hatujitanui nafsi zetu kupita kadiri yetu, kana kwamba hatuwafikii ninyi; kwa sababu tulitangulia kufika mpaka kwenu katika injili ya Kristo; wala hatujisifu zaidi ya kadiri yetu, yaani, katika taabu za watu wengine; bali tukiwa na tumaini ya kwamba, imani yenu ikuapo, tutakuzwa kwenu kwa kadiri ya kipimo chetu, na kupata ziada; hata kuihubiri Injili katika nchi zilizo mbele kupita nchi zenu; tusijisifu katika kipimo cha mtu mwingine kwa mambo yaliyokwisha kutengenezwa. Lakini, Yeye ajisifuye, na ajisifu katika Bwana. Maana mtu mwenye kukubaliwa si yeye ajisifuye, bali yeye asifiwaye na Bwana.
2 Wakorintho 10:12-18 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Hatuthubutu kujiweka kwenye kundi moja au kujilinganisha na hao wanaojitukuza wenyewe kuwa wao ni wa maana sana. Wanapojipima na kujilinganisha wenyewe kwa wenyewe, wanaonesha ya kuwa hawana busara. Lakini sisi hatujajivuna kupita kiasi, bali majivuno yetu yatakuwa katika mipaka ya huduma ile Mungu aliyotuwekea, mipaka ambayo inawafikia hata ninyi. Kwa maana hatukuwa tunavuka mipaka katika kujisifu kwetu, kama ambavyo ingekuwa tusingekuja kwenu. Kwa maana sisi ndio tuliokuwa wa kwanza kuja kwenu na Injili ya Al-Masihi. Wala hatuvuki mipaka kwa kujisifu kwetu kwa ajili ya kazi iliyofanywa na watu wengine. Tumaini letu ni kwamba imani yenu inavyozidi kukua, ndivyo eneo letu la utendaji miongoni mwenu litapanuka zaidi, ili tuweze kuhubiri Injili sehemu zilizo mbali na maeneo yenu. Kwa maana hatutaki kujisifu kwa ajili ya kazi ambayo imekwisha kufanyika tayari katika eneo la mtu mwingine. Lakini, “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Mwenyezi Mungu.” Kwa maana si yeye ajisifuye mwenyewe akubaliwaye, bali yeye ambaye Mwenyezi Mungu humsifu.