2 Wakorintho 8
8
Kutoa kwa ukarimu
1Basi sasa ndugu, nataka ninyi mjue kuhusu ile neema ambayo Mungu amewapa waumini wa Makedonia. 2Ingawa walikuwa na majaribu makali, furaha yao kubwa na umaskini wao mkuu zilifurika kwa ukarimu mwingi. 3Kwa maana nashuhudia kwamba wao walitoa kwa kadiri walivyoweza, hata na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao, 4wakitusihi kwa bidii wapewe fursa ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watakatifu. 5Wala hawakufanya tulivyotazamia, bali walijitoa wao wenyewe kwa Bwana Isa kwanza, na ndipo wakajitoa kwa ajili yetu kufuatana na mapenzi ya Mungu. 6Kwa hiyo tulimsihi Tito, kwa kuwa ndiye alianzisha jambo hili, akamilishe tendo hili la neema kwa upande wenu. 7Lakini kama vile mlivyo mbele sana katika yote, iwe ni katika imani, katika usemi, katika maarifa, katika uaminifu wote na katika upendo wenu kwetu sisi, vivyo hivyo tunataka pia mzidi katika neema hii ya kutoa.
8Siwaamrishi, lakini nataka kujaribu unyofu wa upendo wenu kwa kuulinganisha na bidii ya wengine. 9Kwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi, kwamba ingawa alikuwa tajiri, kwa ajili yenu alikubali kuwa maskini, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri.
10Ushauri wangu kuhusu lile lililo bora kwenu katika jambo hili ni huu: Mwaka uliopita ninyi mlikuwa wa kwanza si tu kutoa lakini pia mlikuwa na shauku ya kufanya hivyo. 11Sasa ikamilisheni kazi hii, ili shauku yenu ya kuitenda iandamane na kuimaliza, mkijitolea kulingana na uwezo wenu. 12Kwa kuwa kama nia ya kutoa ipo, kitolewacho kinakubalika kulingana na kile mtu alicho nacho, wala si kwa kile ambacho hana.
13Nia yetu si kwamba wengine wasaidike wakati ninyi mnateseka, bali pawe na uwiano. 14Kwa wakati huu, wingi wa vitu mlivyo navyo utasaidia kutosheleza mahitaji yao, ili wakati wao watakapokuwa na wingi wa vitu, nao wapate kutosheleza mahitaji yenu. 15Ndipo patakuwa na usawa, kama ilivyoandikwa: “Aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa.”#8:15 Kutoka 16:18
Tito atumwa Korintho
16Ninamshukuru Mungu ambaye amemtia Tito moyo wa kuwajali ninyi kama mimi ninavyowajali. 17Si kwamba Tito amekubali tu ombi letu, bali anakuja kwenu akiwa na shauku kuliko wakati mwingine, tena kwa hiari yake mwenyewe. 18Nasi tunamtuma pamoja naye ndugu ambaye anasifiwa na makundi yote ya waumini kwa huduma yake ya kuhubiri Injili. 19Zaidi ya hayo, alichaguliwa na makundi ya waumini ili asafiri pamoja nasi tulipokuwa tunapeleka matoleo ya ukarimu, kwa ajili ya utukufu wa Bwana Isa mwenyewe, na ili kuonesha hisani yetu kuwasaidia. 20Tunataka kuepuka lawama yoyote kuhusu jinsi tunavyosimamia matoleo haya ya ukarimu. 21Kwa kuwa tunakusudia kufanya kile kilicho haki, si machoni mwa Bwana Isa peke yake, bali pia machoni mwa wanadamu.
22Pamoja nao, tunamtuma ndugu yetu ambaye mara kwa mara ametuthibitishia kwa njia nyingi kwamba ana shauku, naam, zaidi sana sasa kwa sababu analo tumaini kuu kwenu. 23Kwa habari ya Tito, yeye ni mwenzangu na mtendakazi pamoja nami miongoni mwenu. Kwa habari za ndugu zetu, wao ni wawakilishi wa makundi ya waumini, na utukufu kwa Al-Masihi. 24Kwa hiyo waonesheni wazi hawa ndugu uthibitisho wa upendo wenu, na sababu inayotufanya tujivune kwa ajili yenu, ili makundi ya waumini yapate kuuona upendo wenu.
Iliyochaguliwa sasa
2 Wakorintho 8: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.