2 Wakorintho 7
7
1Wapendwa, kwa kuwa tunazo ahadi hizi, basi na tujitakase nafsi zetu kutokana na kila kitu kitiacho mwili na roho unajisi, tukitimiza utakatifu kwa kumcha Mungu.
Furaha ya Paulo
2Tupatieni nafasi mioyoni mwenu. Hatujamkosea mtu yeyote, wala hatujampotosha mtu yeyote, wala hatujamdhulumu mtu yeyote. 3Sisemi haya ili kuwahukumu, kwa kuwa nilisema mwanzo kwamba ninyi mko mioyoni mwetu hata kwa kufa pamoja au kuishi pamoja. 4Nina ujasiri mwingi kwa ajili yenu; naona fahari juu yenu. Nimejawa na faraja. Nina furaha kupita kiasi katika mateso yetu yote.
5Kwa maana hata tulipoingia Makedonia, miili yetu haikuwa na amani. Tulisumbuliwa kila upande; kwa nje kulikuwa na mapigano, na mioyoni mwetu tulikuwa na hofu. 6Bali Mungu, yeye awafarijie wenye huzuni, alitufariji kwa Tito kufika kwetu. 7Lakini si kule kuja kwa Tito tu, bali pia kwa faraja mliyompa. Alitueleza jinsi mlivyonionea shauku, huzuni yenu kubwa na juhudi yenu kwa ajili yangu, ili furaha yangu ipate kuwa kubwa kuliko wakati wowote.
8Hata kama niliwahuzunisha kwa barua yangu, sijutii. Ingawa nilijuta kwa muda mfupi, kwa kuwa najua kwamba barua yangu iliwaumiza, lakini ni kwa kitambo tu. 9Lakini sasa nina furaha, si kwa sababu mlihuzunika, bali kwa kuwa huzuni hiyo iliwafanya mtubu. Kwa maana mlihuzunishwa kama Mungu alivyokusudia watu wahuzunike, na hivyo sisi hatukuwadhuru kwa njia yoyote.
10Kwa maana huzuni ya kiungu huleta toba iletayo wokovu, wala haina majuto. Lakini huzuni ya kidunia husababisha mauti. 11Tazameni jinsi huzuni hii ya kiungu ilivyoleta faida ndani yenu: bidii mliyo nayo, juhudi mliyofanya kujitetea, uchungu wenu, hofu yenu, upendo wenu, shauku yenu na jinsi mlivyokuwa tayari kutoa adhabu inayostahili. Kwa kila njia mmejithibitisha kuwa safi katika jambo hilo. 12Hivyo, ingawa niliwaandikia, haikuwa kwa sababu ya huyo aliyekosa au huyo aliyekosewa. Lakini nilitaka ninyi wenyewe mwone mbele za Mungu jinsi mlivyojitoa kwa ajili yetu. 13Kwa ajili ya haya yote tumefarijika.
Zaidi ya kule sisi kutiwa moyo, tulifurahi sana kumwona Tito alivyo na furaha, kwa sababu roho yake imeburudishwa na ninyi nyote. 14Nilikuwa nimewasifu ninyi kwake, nanyi hamkuniaibisha. Lakini kama vile yale yote tuliyowaambia yalikuwa kweli, hivyo kule kujisifu kwetu kwa Tito kuwahusu ninyi kumethibitishwa kuwa kweli pia. 15Upendo wake kwenu unaongezeka sana anapokumbuka jinsi mlivyokuwa watiifu, mkampokea kwa hofu na kutetemeka. 16Nafurahi kwamba ninaweza kuwatumaini ninyi kabisa.
Iliyochaguliwa sasa
2 Wakorintho 7: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.