2 Wakorintho 6
6
1Kama watendakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msipokee neema ya Mungu bure. 2Kwa maana asema:
“Wakati wangu uliokubalika nilikusikia,
siku ya wokovu nilikusaidia.”#6:2 Isaya 49:8
Tazama, wakati uliokubalika ndio huu, siku ya wokovu ndiyo hii.
Taabu za Paulo
3Hatuweki kikwazo katika njia ya mtu yeyote, ili huduma yetu isionekane kuwa na lawama. 4Bali tunajidhihirisha kuwa watumishi wa Mungu kwa kila njia: katika saburi nyingi; katika dhiki, katika misiba, na katika shida; 5katika kupigwa, katika kufungwa gerezani na katika ghasia; katika kazi ngumu, katika kukesha na katika kufunga; 6katika utakatifu, katika ufahamu, katika uvumilivu, na katika utu wema; katika Roho wa Mungu na upendo wa kweli; 7katika maneno ya kweli na katika nguvu za Mungu; kwa silaha za haki mkononi wa kuume na mkononi wa kushoto; 8katika utukufu na katika kudharauliwa, katika sifa mbaya na katika sifa nzuri; tukionekana kama wadanganyaji, lakini tukiwa wakweli; 9tukiwa maarufu, lakini tukihesabiwa kama tusiojulikana; tukiwa kama wanaokufa, lakini tunaishi; tukipigwa, lakini hatuuawi; 10tukiwa kama wenye huzuni, lakini siku zote tukifurahi; tukionekana maskini, lakini tukitajirisha wengi; tukiwa kama wasio na kitu, lakini tuna vitu vyote.
11Tumesema nanyi wazi, enyi Wakorintho na kuwafungulieni mioyo yetu wazi kabisa. 12Sisi hatujizuii kuwapenda, bali ninyi mmeuzuia upendo wenu kwetu. 13Sasa nasema kama na watoto wangu: Ninyi pia ifungueni mioyo yenu kabisa.
Msifungiwe nira pamoja na wasioamini
14Msifungiwe nira pamoja na watu wasioamini. Kwa maana pana uhusiano gani kati ya haki na uovu? Au kuna ushirika gani kati ya nuru na giza? 15Kuna mapatano gani kati ya Al-Masihi na Beliari#6:15 maana yake Uovu, yaani Shetani? Yeye aaminiye ana sehemu gani na yeye asiyeamini? 16Kuna mapatano gani kati ya Hekalu la Mungu na sanamu? Kwa kuwa sisi tu Hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu alivyosema:
“Nitakaa pamoja nao
na kutembea katikati yao,
nami nitakuwa Mungu wao,
nao watakuwa watu wangu.”#6:16 Walawi 26:12; Yeremia 32:38; Ezekieli 37:27
17Kwa hiyo,
“Tokeni miongoni mwao,
mkatengwe nao,
asema Mwenyezi Mungu.
Msiguse kitu chochote kilicho najisi,
nami nitawakaribisha.”#6:17 Isaya 52:11; Ezekieli 20:34, 41
18Na,
“Mimi nitakuwa Baba kwenu,
nanyi mtakuwa wanangu wa kiume na wa kike,
asema Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni.”#6:18 2 Samweli 7:14; 7:8
Iliyochaguliwa sasa
2 Wakorintho 6: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.