2 Wafalme 14
14
Amazia mfalme wa Yuda
(2 Nyakati 25)
1Katika mwaka wa pili wa utawala wa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli, Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala. 2Alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani, kutoka Yerusalemu. 3Akatenda yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, lakini sio kama Daudi baba yake alivyokuwa amefanya. Katika kila kitu alifuata mfano wa Yoashi baba yake.
4Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.
5Baada ya ufalme kuimarika mkononi mwake, aliwaua maafisa waliomuua mfalme baba yake. 6Hata hivyo, hakuwaua wana wa wale wauaji, sawasawa na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Torati ya Musa, ambako Mwenyezi Mungu aliamuru, “Baba hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto kwa ajili ya baba zao. Kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.”#14:6 Kumbukumbu 24:16
7Ndiye aliwashinda Waedomu elfu kumi katika Bonde la Chumvi, na akauteka Sela katika vita, naye akauita Yoktheeli, jina ambalo mji huo unalo hadi leo.
8Kisha Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, “Njoo, tukabiliane uso kwa uso.”
9Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli akamjibu Amazia mfalme wa Yuda: “Mbaruti uliokuwa Lebanoni ulituma ujumbe kwa mwerezi uliokuwa Lebanoni, ‘Mtoe binti yako aolewe na mwanangu.’ Kisha mnyama wa mwituni aliyekuwa Lebanoni akaja na kuukanyaga ule mbaruti. 10Hakika umeishinda Edomu, na sasa unajivuna. Jisifu katika ushindi wako, lakini kaa nyumbani mwako! Kwa nini unachokoza na kujiletea anguko lako mwenyewe na la Yuda pia?”
11Hata hivyo, Amazia hakusikia, hivyo Yehoashi mfalme wa Israeli akashambulia. Yeye na Amazia mfalme wa Yuda wakakutana uso kwa uso huko Beth-Shemeshi katika Yuda. 12Yuda ikashindwa na Israeli, na kila mtu akakimbilia nyumbani mwake. 13Yehoashi mfalme wa Israeli akamteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-Shemeshi. Kisha Yehoashi akaenda Yerusalemu na kuubomoa ukuta wa Yerusalemu kuanzia Lango la Efraimu hadi Lango la Pembeni, sehemu yenye urefu wa kama dhiraa mia nne#14:13 Dhiraa 400 ni sawa na mita 180.. 14Akachukua dhahabu yote na fedha na vyombo vyote vilivyopatikana ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu na katika hazina zote za jumba la mfalme. Akachukua pia mateka na akarudi Samaria.
15Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehoashi, aliyoyafanya na mafanikio yake, pamoja na vita vyake dhidi ya Amazia mfalme wa Yuda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 16Yehoashi akalala na baba zake, akazikwa Samaria na wafalme wa Israeli. Naye Yeroboamu mwanawe akawa mfalme baada yake.
17Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na tano baada ya kifo cha Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli. 18Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Amazia, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
19Wakapanga njama dhidi ya Amazia huko Yerusalemu, naye akakimbilia Lakishi, lakini wakawatuma watu wamfuatilie huko Lakishi, nao wakamuua huko. 20Akarudishwa kwa farasi, akazikwa huko Yerusalemu pamoja na baba zake katika Mji wa Daudi.
21Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Azaria#14:21 au Uzia aliyekuwa na umri wa miaka kumi na sita, na kumfanya mfalme mahali pa Amazia baba yake. 22Ndiye aliijenga upya Elathi na kuirudisha kwa Yuda baada ya Amazia kulala na baba zake.
Yeroboamu wa pili mfalme wa Israeli
23Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yeroboamu mwana wa Yehoashi mfalme wa Israeli alianza kutawala huko Samaria, naye akatawala kwa miaka arobaini na moja. 24Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, na hakuacha dhambi hata moja ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda. 25Ndiye alirudishia mipaka ya Israeli kuanzia Lebo-Hamathi hadi Bahari ya Araba, sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, lililosemwa kupitia mtumishi wake Yona mwana wa Amitai, nabii kutoka Gath-Heferi.
26Mwenyezi Mungu alikuwa ameona jinsi kila mmoja katika Israeli, awe mtumwa au aliye huru, alivyoteseka kwa uchungu; hapakuwa na yeyote wa kuwasaidia. 27Kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa hajasema kuwa atafuta jina la Israeli chini ya mbingu, akawaokoa kwa mkono wa Yeroboamu mwana wa Yehoashi.
28Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yeroboamu, yote aliyoyafanya na mafanikio yake ya kijeshi, ikiwa ni pamoja na jinsi alivyorudisha Dameski na Hamathi kwa Israeli, ambayo ilikuwa mali ya Yuda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 29Yeroboamu akalala na baba zake, wafalme wa Israeli. Naye Zekaria mwanawe akawa mfalme baada yake.
Iliyochaguliwa sasa
2 Wafalme 14: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.