Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 15

15
Azaria mfalme wa Yuda
(2 Nyakati 26)
1Katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Yeroboamu mfalme wa Israeli, Azaria mwana wa Amazia mfalme wa Yuda alianza kutawala. 2Alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka hamsini na mbili. Mama yake aliitwa Yekolia, kutoka Yerusalemu. 3Akatenda yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, kama Amazia baba yake alivyofanya. 4Hata hivyo, mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.
5Mwenyezi Mungu akampiga mfalme kwa ukoma hadi siku aliyokufa, naye aliishi katika nyumba iliyotengwa peke yake. Yothamu mwana wa mfalme akawa msimamizi wa jumba la mfalme, na akawatawala watu wa nchi.
6Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Azaria na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 7Azaria akalala na baba zake, naye akazikwa karibu nao katika Mji wa Daudi. Naye Yothamu mwanawe akawa mfalme baada yake.
Zekaria mfalme wa Israeli
8Katika mwaka wa thelathini na nane wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Zekaria mwana wa Yeroboamu akawa mfalme wa Israeli katika Samaria, naye akatawala miezi sita. 9Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, kama baba zake walivyofanya. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati ambazo alisababisha Israeli kuzitenda.
10Shalumu mwana wa Yabeshi akapanga njama dhidi ya Zekaria. Akamshambulia mbele ya watu, akamuua, na akawa mfalme baada yake. 11Matukio mengine ya utawala wa Zekaria yameandikwa kwenye kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli. 12Kwa hiyo neno la Mwenyezi Mungu lililonenwa kwa Yehu likatimia, kwamba, “Wazao wako wataketi kwenye kiti cha utawala cha Israeli hadi kizazi cha nne.”#15:12 2 Wafalme 10:30
Shalumu mfalme wa Israeli
13Shalumu mwana wa Yabeshi akawa mfalme katika mwaka wa thelathini na tisa wa Uzia mfalme wa Yuda, naye akatawala katika Samaria kwa mwezi mmoja. 14Kisha Menahemu mwana wa Gadi akaenda kutoka Tirsa hadi Samaria. Akamshambulia Shalumu mwana wa Yabeshi huko Samaria, akamuua, na akawa mfalme baada yake.
15Matukio mengine ya utawala wa Shalumu, na njama alizozipanga, yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli.
16Wakati ule, akianzia Tirsa, Menahemu alishambulia Tifsa na kila mtu ndani yake, na wale waliokuwa maeneo jirani, kwa sababu walikataa kufungua malango yao. Akaiangamiza Tifsa yote, na kuwapasua tumbo wanawake wote wenye mimba.
Menahemu mfalme wa Israeli
17Katika mwaka wa thelathini na tisa wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Menahemu mwana wa Gadi akawa mfalme wa Israeli, akatawala huko Samaria kwa miaka kumi. 18Akatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu. Katika wakati wa utawala wake wote, hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati ambazo alisababisha Israeli kuzitenda.
19Kisha Pulu mfalme wa Ashuru akaishambulia Israeli. Menahemu mfalme wa Israeli akampa talanta elfu moja#15:19 Talanta 1,000 ni sawa na tani 34. za fedha ili amsaidie na kumwezesha katika utawala wake. 20Menahemu akatoza fedha hizi kwa nguvu kutoka kwa Israeli. Kila mtu tajiri alilazimika kuchanga shekeli hamsini#15:20 Shekeli 50 ni sawa na gramu 600. za fedha ambazo alipewa mfalme wa Ashuru. Basi mfalme wa Ashuru akajiondoa na hakuendelea kuikalia nchi.
21Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Menahemu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 22Menahemu akalala na baba zake. Naye Pekahia mwanawe akawa mfalme baada yake.
Pekahia mfalme wa Israeli
23Katika mwaka wa hamsini wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Pekahia mwana wa Menahemu akawa mfalme wa Israeli huko Samaria, akatawala miaka miwili. 24Pekahia akafanya uovu machoni pa Mwenyezi Mungu. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda. 25Mmoja wa maafisa wake wakuu, Peka mwana wa Remalia, akapanga njama dhidi yake. Akachukua watu hamsini wa Gileadi pamoja naye, akamuua Pekahia, pamoja na Argobu na Aria, katika ngome ya jumba la kifalme huko Samaria. Kwa hiyo Peka akamuua Pekahia, naye akawa mfalme baada yake.
26Matukio mengine ya utawala wa Pekahia na yote aliyoyafanya yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli.
Peka mfalme wa Israeli
27Katika mwaka wa hamsini na mbili wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Peka mwana wa Remalia akawa mfalme wa Israeli huko Samaria, naye alitawala miaka ishirini. 28Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda.
29Wakati wa utawala wa Peka mfalme wa Israeli, Tiglath-Pileseri mfalme wa Ashuru alikuja na kuteka Iyoni, Abel-Beth-Maaka, Yanoa, Kedeshi na Hazori. Akateka miji ya Gileadi na Galilaya, pamoja na nchi yote ya Naftali, na kuwahamishia watu wote Ashuru. 30Kisha Hoshea mwana wa Ela akapanga njama dhidi ya Peka mwana wa Remalia. Hoshea akamshambulia Peka na kumuua, kisha akawa mfalme baada yake katika mwaka wa ishirini wa Yothamu mwana wa Uzia.
31Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Peka na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
Yothamu mfalme wa Yuda
(2 Nyakati 27)
32Katika mwaka wa pili wa utawala wa Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli, Yothamu mwana wa Uzia mfalme wa Yuda alianza kutawala. 33Alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita. Mama yake aliitwa Yerusha binti Sadoki. 34Akafanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, kama Uzia baba yake alivyokuwa amefanya. 35Hata hivyo, mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko. Yothamu akajenga upya Lango la Juu la Hekalu la Mwenyezi Mungu.
36Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yothamu na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 37(Katika siku hizo, Mwenyezi Mungu akaanza kuwatuma Resini mfalme wa Aramu na Peka mwana wa Remalia dhidi ya Yuda.) 38Yothamu akalala na baba zake, akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi, mji wa baba zake. Naye Ahazi mwanawe akawa mfalme baada yake.

Iliyochaguliwa sasa

2 Wafalme 15: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia