Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 15:17-26

2 Wafalme 15:17-26 NENO

Katika mwaka wa thelathini na tisa wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Menahemu mwana wa Gadi akawa mfalme wa Israeli, akatawala huko Samaria kwa miaka kumi. Akatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu. Katika wakati wa utawala wake wote, hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati ambazo alisababisha Israeli kuzitenda. Kisha Pulu mfalme wa Ashuru akaishambulia Israeli. Menahemu mfalme wa Israeli akampa talanta elfu moja za fedha ili amsaidie na kumwezesha katika utawala wake. Menahemu akatoza fedha hizi kwa nguvu kutoka kwa Israeli. Kila mtu tajiri alilazimika kuchanga shekeli hamsini za fedha ambazo alipewa mfalme wa Ashuru. Basi mfalme wa Ashuru akajiondoa na hakuendelea kuikalia nchi. Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Menahemu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? Menahemu akalala na baba zake. Naye Pekahia mwanawe akawa mfalme baada yake. Katika mwaka wa hamsini wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Pekahia mwana wa Menahemu akawa mfalme wa Israeli huko Samaria, akatawala miaka miwili. Pekahia akafanya uovu machoni pa Mwenyezi Mungu. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda. Mmoja wa maafisa wake wakuu, Peka mwana wa Remalia, akapanga njama dhidi yake. Akachukua watu hamsini wa Gileadi pamoja naye, akamuua Pekahia, pamoja na Argobu na Aria, katika ngome ya jumba la kifalme huko Samaria. Kwa hiyo Peka akamuua Pekahia, naye akawa mfalme baada yake. Matukio mengine ya utawala wa Pekahia na yote aliyoyafanya yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli.