Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 15:17-26

2 Wafalme 15:17-26 Biblia Habari Njema (BHN)

Katika mwaka wa thelathini na tisa wa enzi ya mfalme Azaria wa Yuda, Menahemu mwana wa Gadi alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa muda wa miaka kumi. Alimwasi Mwenyezi-Mungu siku zote za utawala wala hakuacha maovu ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye aliwapotosha watu wa Israeli wakatenda dhambi. Basi, Pulu mfalme wa Ashuru, aliivamia Israeli, naye Menahemu akampa kilo thelathini na nne za fedha ili amsaidie kuimarisha mamlaka yake juu ya nchi ya Israeli. Menahemu alipata fedha hiyo kwa kuwalazimisha matajiri wa Israeli kutoa mchango wa shekeli hamsini za fedha kila mmoja. Halafu Pulu hakukaa Israeli bali alirudi katika nchi yake. Matendo mengine yote ya Menahemu yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. Menahemu alifariki, naye mwanawe Pekahia alitawala mahali pake. Katika mwaka wa hamsini wa enzi ya mfalme Azaria wa Yuda, Pekahia mwana wa Menahemu alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa muda wa miaka miwili. Alimwasi Mwenyezi-Mungu na kufuata mfano mbaya wa mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye aliwafanya watu wa Israeli watende dhambi. Peka mwana wa Remalia, ambaye alikuwa ofisa wa jeshi la Pekahia, alishirikiana na watu wengine hamsini kutoka Gileadi, akamuua Pekahia katika ngome ya ndani ya nyumba ya mfalme huko Samaria, na kuwa mfalme mahali pake. Matendo mengine ya Pekahia na yote aliyofanya yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.

2 Wafalme 15:17-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Katika mwaka wa thelathini na tisa wa Uzia mfalme wa Yuda Menahemu mwana wa Gadi alianza kutawala juu ya Israeli, akatawala miaka kumi katika Samaria. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA; hakuyaacha siku zake zote makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli. Akaja Pulu mfalme wa Ashuru juu ya nchi; naye Menahemu akampa Pulu talanta elfu moja za fedha, ili kwamba mkono wake uwe pamoja naye, na ufalme uwe imara mkononi mwake. Na Menahemu akawatoza Israeli fedha hiyo, yaani, matajiri wote wenye mali, kila mtu shekeli hamsini za fedha, ili ampe huyo mfalme wa Ashuru. Basi mfalme wa Ashuru akarejea, wala hakukaa huko katika nchi. Basi mambo yote ya Menahemu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli? Menahemu akalala na babaze; na Pekahia mwanawe akatawala mahali pake. Katika mwaka wa hamsini wa Uzia mfalme wa Yuda Pekahia mwana wa Menahemu alianza kutawala juu ya Israeli hatika Samaria; akatawala miaka miwili. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli. Na Peka mwana wa Remalia, jemadari wake, akamfanyia uhaini, akampiga huko Samaria, katika ngome ya nyumba ya mfalme, pamoja na Argobu na Arie; na pamoja naye walikuwako watu hamsini wa Wagileadi. Akamwua, akatawala mahali pake. Basi mambo yote ya Pekahia yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, tazama, yameandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli.

2 Wafalme 15:17-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Katika mwaka wa thelathini na kenda wa Uzia mfalme wa Yuda Menahemu mwana wa Gadi alianza kutawala juu ya Israeli, akatawala miaka kumi katika Samaria. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA; hakuyaacha siku zake zote makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli. Akaja Pulu mfalme wa Ashuru juu ya nchi; naye Menahemu akampa Pulu talanta elfu za fedha, ili kwamba mkono wake uwe pamoja naye, na ufalme uwe imara mkononi mwake. Na Menahemu akawatoza Israeli fedha hiyo, yaani, wakuu wote wenye mali, kila mtu shekeli hamsini za fedha, ili ampe huyo mfalme wa Ashuru. Basi mfalme wa Ashuru akarejea, wala hakukaa huko katika nchi. Basi mambo yote ya Menahemu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli? Menahemu akalala na babaze; na Pekahia mwanawe akatawala mahali pake. Katika mwaka wa hamsini wa Uzia mfalme wa Yuda Pekahia mwana wa Menahemu alianza kutawala juu ya Israeli hatika Samaria; akatawala miaka miwili. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli. Na Peka mwana wa Remalia, jemadari wake, akamfanyia fitina, akampiga huko Samaria, katika ngome ya nyumba ya mfalme, pamoja na Argobu na Arie; na pamoja naye walikuwako watu hamsini wa Wagileadi. Akamwua, akatawala mahali pake. Basi mambo yote ya Pekahia yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, tazama, yameandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli.

2 Wafalme 15:17-26 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Katika mwaka wa thelathini na tisa wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Menahemu mwana wa Gadi akawa mfalme wa Israeli, akatawala huko Samaria kwa miaka kumi. Akatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu. Katika wakati wa utawala wake wote, hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati ambazo alisababisha Israeli kuzitenda. Kisha Pulu mfalme wa Ashuru akaishambulia Israeli. Menahemu mfalme wa Israeli akampa talanta elfu moja za fedha ili amsaidie na kumwezesha katika utawala wake. Menahemu akatoza fedha hizi kwa nguvu kutoka kwa Israeli. Kila mtu tajiri alilazimika kuchanga shekeli hamsini za fedha ambazo alipewa mfalme wa Ashuru. Basi mfalme wa Ashuru akajiondoa na hakuendelea kuikalia nchi. Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Menahemu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? Menahemu akalala na baba zake. Naye Pekahia mwanawe akawa mfalme baada yake. Katika mwaka wa hamsini wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Pekahia mwana wa Menahemu akawa mfalme wa Israeli huko Samaria, akatawala miaka miwili. Pekahia akafanya uovu machoni pa Mwenyezi Mungu. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda. Mmoja wa maafisa wake wakuu, Peka mwana wa Remalia, akapanga njama dhidi yake. Akachukua watu hamsini wa Gileadi pamoja naye, akamuua Pekahia, pamoja na Argobu na Aria, katika ngome ya jumba la kifalme huko Samaria. Kwa hiyo Peka akamuua Pekahia, naye akawa mfalme baada yake. Matukio mengine ya utawala wa Pekahia na yote aliyoyafanya yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli.