Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Petro 3

3
Siku ya Mwenyezi Mungu
1Wapendwa, huu ndio waraka wangu wa pili ninaowaandikia. Katika nyaraka hizi mbili ninajaribu kuziamsha nia zenu safi kwa mawazo makamilifu. 2Nataka ninyi mkumbuke maneno yaliyosemwa zamani na manabii watakatifu na ile amri ya Bwana na Mwokozi wetu mliyopewa kupitia kwa mitume wenu.
3Kwanza kabisa, ni lazima mfahamu kwamba siku za mwisho watakuja watu wenye dhihaka, wakidhihaki na kuzifuata tamaa zao mbovu. 4Watasema, “Iko wapi ile ahadi ya kuja kwake? Tangu baba zetu walipofariki, kila kitu kinaendelea kama kilivyokuwa tangu mwanzo wa kuumbwa.” 5Lakini wao kwa makusudi hupuuza ukweli huu, kwamba kwa neno la Mungu mbingu zilikuwa tangu zamani, nayo dunia ilifanyizwa kutoka ndani ya maji na kwa maji. 6Ulimwengu wa wakati ule uligharikishwa kwa hayo maji na kuangamizwa. 7Kwa neno lilo hilo, mbingu za sasa na dunia zimewekwa akiba kwa ajili ya moto, zikihifadhiwa hadi siku ile ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu.
8Lakini wapendwa, msisahau neno hili: kwamba kwa Mwenyezi Mungu, siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. 9Mwenyezi Mungu hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba.
10Lakini siku ya Mwenyezi Mungu itakuja kama mwizi. Ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; navyo vitu vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia na kila kitu kilicho ndani yake kitaunguzwa.
11Kwa kuwa vitu vyote vitaharibiwa namna hii, je, ninyi imewapasa kuwa watu wa namna gani? Inawapasa kuishi maisha matakatifu na ya kumcha Mungu, 12mkingojea na kuhimiza kuja kwa hiyo siku ya Mungu. Siku hiyo italeta mbingu kuchomwa moto na kutoweka, na vitu vya asili vitayeyuka kwa moto. 13Lakini kufuatana na ahadi yake, sisi tunatazamia mbingu mpya na dunia mpya, ambayo haki hukaa ndani yake.
14Kwa sababu hii, wapendwa, kwa kuwa mnatazamia mambo haya, fanyeni bidii ili awakute bila mawaa wala dosari, na mkiwa na amani kwake. 15Hesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile ndugu yetu mpendwa Paulo alivyowaandikia kwa hekima ile aliyopewa na Mungu. 16Huandika vivyo hivyo katika nyaraka zake zote, akizungumzia ndani yake mambo haya. Katika nyaraka zake kuna mambo mengine ambayo ni vigumu kuyaelewa, ambayo watu wajinga na wasio thabiti huyapotosha, kama wanavyopotosha Maandiko mengine na kujiletea maangamizi yao wenyewe.
17Basi, ninyi wapendwa, kwa kuwa mmekwisha kujua mambo haya, jilindeni msije mkachukuliwa na kosa la watu hao waasi na kuanguka kutoka kwa uthabiti wenu. 18Bali kueni katika neema na katika kumjua Bwana na Mwokozi wetu Isa Al-Masihi.
Utukufu una yeye sasa na milele! Amen.

Iliyochaguliwa sasa

2 Petro 3: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia