2 Samweli 16
16
Daudi na Siba
1Daudi alipokuwa ameenda umbali mfupi kupita kilele cha mlima, akamkuta huko Siba, msimamizi wa shughuli za Mefiboshethi, akingojea kumlaki Daudi. Alikuwa na punda wawili wakiwa wametandikwa na kupakiwa mikate mia mbili, maandazi mia ya zabibu kavu, maandazi mia ya tini, na kiriba cha divai.
2Mfalme Daudi akamuuliza Siba, “Kwa nini umeleta vitu hivi?”
Siba akamjibu, “Punda ni kwa ajili ya watu wa nyumba ya mfalme kupanda, mikate na matunda ni kwa ajili ya watu kula, nayo divai ni kwa kuwaburudisha watakaochoka jangwani.”
3Kisha mfalme akauliza, “Yuko wapi mwana wa bwana wako?”
Siba akamwambia, “Anakawia Yerusalemu, kwa sababu anafikiri, ‘Leo nyumba ya Israeli itanirudishia utawala wa baba yangu.’ ”
4Ndipo mfalme akamwambia Siba, “Yote yaliyokuwa mali ya Mefiboshethi sasa ni mali yako.”
Siba akasema, “Nasujudu kwa unyenyekevu. Naomba nipate kibali mbele yako, bwana wangu mfalme.”
Shimei amlaani Daudi
5Mfalme Daudi alipokuwa anakaribia Bahurimu, mtu mmoja wa ukoo wa jamaa ya Sauli, akatoka humo. Jina lake ni Shimei mwana wa Gera; akawa analaani alipokuwa akitoka. 6Akamtupia Daudi na maafisa wote wa mfalme mawe, ingawa vikosi vyote na walinzi maalum walikuwa kulia na kushoto mwa Daudi. 7Shimei alivyokuwa akilaani, akasema, “Toka hapa, toka hapa, wewe mtu wa damu, wewe mtu mbaya kabisa! 8Mwenyezi Mungu amekulipiza kwa ajili ya damu yote uliyomwaga ya watu wa nyumba ya Sauli, ambaye nafasi yake umeimiliki wewe. Mwenyezi Mungu amekabidhi ufalme mkononi mwa mwanao Absalomu. Maangamizi yamekupata kwa sababu wewe ni mtu wa damu!”
9Ndipo Abishai mwana wa Seruya akamwambia mfalme, “Kwa nini huyu mbwa mfu amlaani bwana wangu mfalme? Niruhusu nivuke nikatilie mbali kichwa chake.”
10Lakini mfalme akamwambia, “Mna nini nami, enyi wana wa Seruya? Ikiwa analaani kwa sababu Mwenyezi Mungu amemwambia, ‘Mlaani Daudi,’ nani awezaye kuuliza, ‘Kwa nini unafanya hivi?’ ”
11Ndipo Daudi akamwambia Abishai na maafisa wake wote, “Mwanangu, ambaye ametoka viunoni mwangu mwenyewe, anajaribu kuniua. Je, si zaidi sana huyu Mbenyamini! Mwacheni; acha alaani, kwa maana Mwenyezi Mungu amemwambia afanye hivyo. 12Inawezekana kwamba Mwenyezi Mungu ataona dhiki yangu na kunilipa mema kwa ajili ya laana ninayopokea leo.”
13Kwa hiyo Daudi na watu wake wakaendelea na safari yao barabarani, huku Shimei akiwa anatembea pembezoni mwa kilima sambamba na Daudi, huku akimlaani na kumtupia Daudi mawe na kumrushia mavumbi. 14Mfalme na watu wote aliokuwa pamoja nao wakafika kwenye kituo chao wakiwa wamechoka. Mfalme akajiburudisha hapo.
Ushauri wa Hushai na Ahithofeli
15Wakati huo, Absalomu pamoja na wanaume wote wa Israeli wakafika Yerusalemu, naye Ahithofeli alikuwa pamoja naye. 16Ndipo Hushai Mwarki, rafiki wa Daudi, akamwendea Absalomu na kumwambia, “Mfalme aishi maisha marefu! Mfalme aishi maisha marefu!”
17Absalomu akamuuliza Hushai, “Je, huu ndio upendo unaomwonesha rafiki yako? Kwa nini hukufuatana na rafiki yako?”
18Hushai akamwambia Absalomu, “La hasha! Yeye aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu, aliyechaguliwa na watu hawa, atakayechaguliwa tena na wanaume wote wa Israeli, huyu ndiye nitakayekuwa wake, nami nitabakia pamoja naye. 19Zaidi ya hayo, nimtumikie nani? Je, nisimtumikie mwana? Kama vile nilivyomtumikia baba yako, ndivyo nitakavyokutumikia wewe.”
20Absalomu akamwambia Ahithofeli, “Tupe ushauri wako. Tufanye nini?”
21Ahithofeli akamjibu Absalomu, “Kutana kimwili na masuria wa baba yako aliowaacha kutunza jumba la kifalme. Ndipo Israeli yote itakaposikia kwamba umejifanya chukizo kwa baba yako, nayo mikono ya kila mmoja aliye pamoja nawe itatiwa nguvu.” 22Kwa hiyo wakamtengenezea Absalomu hema juu ya dari, naye akakutana kimwili na masuria wa baba yake machoni pa Israeli wote.
23Ilikuwa katika siku hizo shauri lililotolewa na Ahithofeli lilikuwa kama lile ambalo limeulizwa kwa Mungu. Ndivyo Daudi na Absalomu walivyoyaheshimu mashauri yote ya Ahithofeli.
Iliyochaguliwa sasa
2 Samweli 16: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.