2 Samweli 17
17
1Ahithofeli akamwambia Absalomu, “Nipe ruhusa niwachague watu elfu kumi na mbili, nao waanze safari usiku huu huu kumfuatia Daudi. 2Nitamshambulia wakati akiwa amechoka na ni dhaifu. Nitampiga na hofu, na kisha watu wote walio pamoja naye watakimbia. Nitampiga mfalme peke yake 3na kuwarudisha watu wote kwako. Kifo cha mtu yule unayemtafuta kitamaanisha kurudi kwa wote, hakuna hata mtu mmoja atakayeumizwa.” 4Mpango huu ulionekana mzuri kwa Absalomu na kwa wazee wote wa Israeli.
5Lakini Absalomu akasema, “Pia mwiteni Hushai, Mwarki, ili tuweze kusikia anachokisema.” 6Hushai alipokuja, Absalomu akasema, “Ahithofeli ametoa ushauri huu. Je, tufanye anavyosema? Kama sivyo, tupe maoni yako.”
7Hushai akamjibu Absalomu, “Ushauri alioutoa Ahithofeli haufai kwa wakati huu. 8Unamfahamu baba yako na watu wake, ni wapiganaji hodari, nao ni wakali kama dubu aliyepokonywa watoto wake. Zaidi ya hayo, baba yako ni mpiganaji jasiri, usiku hatalala pamoja na vikosi. 9Hata sasa, amefichwa ndani ya pango au mahali pengine. Kama atatangulia kushambulia vikosi vyako, yeyote asikiaye habari hii atasema, ‘Kuna machinjo makubwa miongoni mwa vikosi vinavyomfuata Absalomu.’ 10Basi hata yule askari hodari kuliko wengine wote, ambaye moyo wake ni kama wa simba, atayeyuka kwa hofu, kwa maana Israeli yote wanajua kwamba baba yako ni mpiganaji na kwamba wale walio pamoja naye ni watu hodari.
11“Kwa hiyo nakushauri: Israeli wote na wakusanyike kwako, kuanzia Dani hadi Beer-Sheba, wakiwa wengi kama mchanga wa ufuo wa bahari; wakusanyike kwako, nawe ukiwaongoza vitani. 12Ndipo tutakapomshambulia popote atakapoonekana, nasi tutamwangukia kama umande unavyoshuka juu ya ardhi. Yeye mwenyewe na watu wake hakuna atakayeachwa hai. 13Kama atakimbilia katika mji wowote, basi Israeli wote watazungushia mji ule kamba, nasi tutauburuta mji huo hadi bondeni, wala isionekane hata changarawe ya huo mji.”
14Absalomu na wanaume wote wa Israeli wakasema, “Ushauri wa Hushai, Mwarki, ni mwema kuliko ule wa Ahithofeli.” Kwa maana Mwenyezi Mungu alikuwa amekusudia kupinga ushauri mwema wa Ahithofeli, ili kuleta maafa kwa Absalomu.
15Hushai akawaambia makuhani Sadoki na Abiathari, “Ahithofeli amemshauri Absalomu na wazee wa Israeli kufanya hivi na hivi, lakini mimi nimewashauri wao kufanya lile na lile. 16Sasa tumeni ujumbe haraka na kumwambia Daudi, ‘Usiku huu usilale kwenye vivuko katika jangwa; vuka bila kukosa, la sivyo, mfalme pamoja na watu wote waliofuatana naye watamezwa.’ ”
17Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakingoja huko En-Rogeli. Naye mjakazi mmoja alipaswa kuwapasha habari nao wakawa waende kumwambia Mfalme Daudi, kwa maana wasingetaka kujihatarisha kuonekana wakiingia mjini. 18Lakini kijana mmoja mwanaume akawaona, naye akamwambia Absalomu. Basi wote wawili wakaondoka haraka, wakaenda hadi kwenye nyumba ya mtu mmoja huko Bahurimu. Mtu huyo alikuwa na kisima uani mwake, nao Yonathani na Ahimaasi wakateremka ndani ya kisima hicho. 19Mkewe akachukua kifuniko, akakiweka juu ya mdomo wa kile kisima na kuanika nafaka juu yake. Hakuna mtu yeyote aliyefahamu chochote kuhusu jambo hilo.
20Watu wa Absalomu walipofika kwa huyo mwanamke, wakamuuliza, “Wako wapi Ahimaasi na Yonathani?”
Huyo mwanamke akawajibu, “Walivuka kijito.” Watu wa Absalomu wakapekua lakini hawakuwaona hata mmoja, hivyo wakarudi Yerusalemu.
21Baada ya watu hao kuondoka, wale watu wawili yaani Yonathani na Ahimaasi wakapanda kutoka mle kisimani na kwenda kumpasha Mfalme Daudi habari. Wakamwambia, “Ondoka, uvuke mto haraka. Ahithofeli ameshauri hivi na hivi dhidi yako.” 22Kwa hiyo Daudi na watu wote aliokuwa nao waliondoka na kuvuka Yordani. Kufika wakati wa mapambazuko, hapakuwa na mtu hata mmoja aliyekuwa hajavuka Mto Yordani.
23Ahithofeli alipoona kwamba ushauri wake haukufuatwa, akatandika punda wake, akaondoka kwenda nyumbani mwake kwenye mji wake. Akaiweka nyumba yake katika utaratibu, kisha akajinyonga mwenyewe. Hivyo akafa na akazikwa katika kaburi la baba yake.
Kifo cha Absalomu
24Daudi akaenda Mahanaimu, naye Absalomu akavuka Yordani pamoja na wanaume wote wa Israeli. 25Absalomu alikuwa amemweka Amasa awe mkuu wa jeshi badala ya Yoabu. Amasa alikuwa mwana wa mtu mmoja aliyeitwa Yetheri, Mwishmaeli aliyekuwa amemwoa Abigaili binti Nahashi, dada yake Seruya mamaye Yoabu. 26Waisraeli na Absalomu wakapiga kambi huko nchi ya Gileadi.
27Daudi alipofika Mahanaimu, Shobi mwana wa Nahashi kutoka Raba ya Waamoni, Makiri mwana wa Amieli kutoka Lo-Debari, na Barzilai Mgileadi kutoka Rogelimu 28wakaleta matandiko ya kitanda, mabakuli na vyombo vya mfinyanzi. Walileta pia ngano na shayiri, unga na bisi, maharagwe na kunde, 29asali na maziwa yaliyoganda, kondoo na jibini kutoka maziwa ya ng’ombe kwa ajili ya Daudi na watu wake ili wale. Kwa maana walisema, “Watu wameona njaa, tena wamechoka na wamepata kiu huko jangwani.”
Iliyochaguliwa sasa
2 Samweli 17: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.