2 Samweli 6
6
Sanduku la Mungu laletwa Yerusalemu
(1 Nyakati 13:1-14; 15:25–16:6, 43)
1Tena Daudi akakusanya vijana wenye uwezo wote wa Israeli: watu elfu thelathini. 2Yeye na watu wake wote wakatoka Baala ya Yuda#6:2 yaani Kiriath-Yearimu kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka huko, linaloitwa kwa Jina, naam, jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, anayeketi kwenye kiti cha enzi kati ya makerubi walio juu ya hilo Sanduku. 3Wakaweka hilo Sanduku la Mungu juu ya gari jipya la kukokotwa na kulileta kutoka nyumba ya Abinadabu, iliyokuwa juu ya kilima. Uza na Ahio, wana wa Abinadabu, walikuwa wakiongoza hilo gari jipya la kukokotwa 4likiwa na Sanduku la Mungu juu yake, naye Ahio alikuwa anatembea akiwa mbele yake. 5Daudi na nyumba yote ya Israeli walikuwa wanacheza mbele za Mwenyezi Mungu kwa nguvu zao zote, kwa nyimbo, vinubi, zeze, matari, kayamba na matoazi.
6Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Nakoni, Uza akanyoosha mkono na kulishika Sanduku la Mungu kwa sababu maksai walijikwaa. 7Hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya Uza kwa sababu ya kitendo chake cha kukosa heshima, kwa hiyo Mungu akampiga akafia papo hapo kando ya Sanduku la Mungu.
8Ndipo Daudi akakasirika kwa sababu ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ilifurika dhidi ya Uza, hivyo hadi leo mahali hapo panaitwa Peres-Uza.
9Daudi akamwogopa Mwenyezi Mungu siku ile, akasema, “Ni jinsi gani Sanduku la Mwenyezi Mungu litakavyoweza kunijia?” 10Hakuwa radhi kulichukua Sanduku la Mwenyezi Mungu kwake katika Mji wa Daudi. Badala yake akalipeleka kwenye nyumba ya Obed-Edomu, Mgiti. 11Sanduku la Mwenyezi Mungu likakaa katika nyumba ya Obed-Edomu, Mgiti, kwa miezi mitatu, naye Mwenyezi Mungu akambariki pamoja na nyumba yake yote.
12Kisha Mfalme Daudi akaambiwa, “Mwenyezi Mungu ameibariki nyumba ya Obed-Edomu pamoja na kila alicho nacho, kwa sababu ya Sanduku la Mungu.” Basi Daudi akateremka na kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka nyumba ya Obed-Edomu hadi Mji wa Daudi kwa shangwe. 13Wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Mwenyezi Mungu walipotembea hatua sita, Daudi alitoa dhabihu fahali na ndama aliyenoneshwa. 14Daudi, akiwa amevaa kizibau cha kitani, alicheza mbele za Mwenyezi Mungu kwa nguvu zake zote, 15wakati yeye na nyumba yote ya Israeli walipopandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu kwa shangwe na sauti za tarumbeta.
16Sanduku la Mwenyezi Mungu lilipokuwa linaingia Mji wa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia dirishani. Naye alipomwona Mfalme Daudi akirukaruka na kucheza mbele za Mwenyezi Mungu, akamdharau moyoni mwake.
17Wakaleta Sanduku la Mwenyezi Mungu na kuliweka mahali pake ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelisimamisha kwa ajili yake, naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Mwenyezi Mungu. 18Baada ya kumaliza kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, Daudi akawabariki watu katika jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. 19Kisha akatoa mkate, andazi la tende na andazi la zabibu kavu kwa kila mtu katika mkutano wote wa Waisraeli, wanaume kwa wanawake. Nao watu wote wakaenda nyumbani.
20Daudi aliporudi ili kuwabariki watu wa nyumbani mwake, Mikali binti Sauli akatoka nje kumlaki, akamwambia, “Tazama jinsi mfalme wa Israeli alivyojibainisha mwenyewe leo kwa kuvua mavazi yake machoni pa vijakazi wa watumishi wake, vile mtu asiye na adabu angefanya!”
21Daudi akamwambia Mikali, “Nilifanya hivyo mbele za Mwenyezi Mungu ambaye alinichagua mimi badala ya baba yako au mwingine yeyote kutoka nyumba yake aliponiweka niwe mtawala wa Israeli, watu wa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo nitacheza mbele za Mwenyezi Mungu. 22Nitakuwa asiye na heshima kuliko sasa, nami nitajishusha machoni pangu mwenyewe. Lakini kwa hawa vijakazi uliosema habari zao nitaheshimiwa.”
23Naye Mikali binti Sauli hakuwa na watoto hadi siku ya kufa kwake.
Iliyochaguliwa sasa
2 Samweli 6: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.