Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 7

7
Ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa Daudi
(1 Nyakati 17:1-15)
1Baada ya mfalme kuingia rasmi katika jumba lake la kifalme, naye Mwenyezi Mungu akiwa amempa amani pande zote kutoka kwa adui zake, 2akamwambia nabii Nathani, “Mimi hapa ninaishi katika jumba la kifalme la mwerezi, wakati Sanduku la Mungu limebaki katika hema.”
3Nathani akamjibu mfalme, “Lolote ulilo nalo moyoni, endelea ukalifanye, kwa maana Mwenyezi Mungu yu pamoja nawe.”
4Usiku ule neno la Mwenyezi Mungu likamjia Nathani, kusema:
5“Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Je, ewe ndiwe wa kunijengea mimi nyumba ili nikae ndani yake? 6Sijakaa ndani ya nyumba tangu siku niliyowaleta Waisraeli kutoka Misri hadi leo. Nimekuwa nikitembea kutoka mahali pamoja hadi mahali pengine na hema kama makao yangu. 7Popote nilipotembea pamoja na Waisraeli wote, je, nimewahi kumwambia kiongozi wao yeyote niliyemwamuru kuwachunga watu wangu Israeli, “Kwa nini hujanijengea nyumba ya mwerezi?” ’
8“Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: Nilikutoa malishoni na kutoka kulisha mifugo, ili uwaongoze watu wangu Israeli. 9Nimekuwa pamoja nawe popote ulipoenda, nami nimekuondolea mbali adui zako wote mbele yako. Basi nitalifanya jina lako kuwa kuu kama majina ya watu walio wakuu sana duniani. 10Nami nitawapatia watu wangu Israeli mahali niwapande humo ili wawe na nyumbani kwao wenyewe wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawatesa tena, kama walivyofanya mwanzoni, 11na kama walivyofanya tangu mwanzo wakati nilipowaweka viongozi juu ya watu wangu Israeli. Pia nitawapa amani mbele ya adui zenu wote.
“ ‘Mwenyezi Mungu akuambia kwamba Mwenyezi Mungu mwenyewe atakujengea nyumba. 12Siku zako zitakapokwisha nawe ulale pamoja na baba zako, nitainua mzao wako aingie mahali pako, ambaye atatoka viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake. 13Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu, nami nitakiimarisha kiti cha ufalme wake milele. 14Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Atakapokosea nitamwadhibu kwa fimbo ya wanadamu, kwa adhabu ya kupigwa na wanadamu. 15Lakini upendo wangu kamwe hautaondolewa kwake, kama nilivyouondoa kwa Sauli, niliyemwondoa atoke mbele yako. 16Nyumba yako na ufalme wako utadumu milele mbele zangu, kiti chako cha utawala kitaimarishwa milele.’ ”
17Nathani akamwarifu Daudi maneno yote ya maono haya.
Maombi ya Daudi
(1 Nyakati 17:16-27)
18Ndipo Mfalme Daudi akaingia ndani, akaketi mbele za Mwenyezi Mungu, akasema:
“Ee Bwana Mungu Mwenyezi, mimi ni nani, na jamaa yangu ni nini, hata umenileta hadi hapa? 19Naam, kana kwamba hili halitoshi machoni pako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi, wewe umenena pia kuhusu siku zijazo za nyumba ya mtumishi wako. Je, hii ndiyo njia yako ya kawaida ya kushughulika na mwanadamu, Ee Bwana Mungu Mwenyezi?
20“Je, Daudi aweza kukuambia nini zaidi? Kwa maana unamjua mtumishi wako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi. 21Kwa ajili ya neno lako na kwa mapenzi yako, umefanya jambo hili kubwa na kulifanya lijulikane na lifahamike kwa mtumishi wako.
22“Tazama jinsi ulivyo mkuu, Ee Bwana Mungu Mwenyezi! Hakuna mwingine kama wewe, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe, 23Naye ni nani aliye kama watu wako Israeli, taifa pekee duniani ambalo Mungu alitoka kwenda kulikomboa kwa ajili yake mwenyewe, na kujifanyia jina mwenyewe, kwa kufanya maajabu makubwa na ya kutisha kwa kuwafukuza mataifa na miungu yao mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri? 24Umeimarisha watu wako Israeli hasa kama watu wako mwenyewe milele, nawe, Ee Mwenyezi Mungu, umekuwa Mungu wao.
25“Basi sasa, Bwana Mwenyezi Mungu, ukaitimize ahadi uliyosema kuhusu mtumishi wako na nyumba yake milele. Fanya kama ulivyoahidi, 26ili jina lako litukuke milele. Ndipo watu watasema, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ni Mungu juu ya Israeli!’ Nayo nyumba ya mtumishi wako Daudi itakuwa imara mbele zako.
27“Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, umelifunua hili kwa mtumishi wako, ukisema, ‘Nitakujengea nyumba.’ Hivyo mtumishi wako amepata ujasiri kukuletea dua hili. 28Ee Bwana Mungu Mwenyezi, wewe ndiwe Mungu! Maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidi mtumishi wako mambo haya mazuri. 29Sasa naomba uwe radhi kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili idumu mbele zako milele, kwa maana wewe, Ee Bwana Mungu Mwenyezi, umesema, na kwa baraka zako nyumba ya mtumishi wako itaendelea kubarikiwa milele.”

Iliyochaguliwa sasa

2 Samweli 7: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia