2 Samweli 8
8
Ushindi wa Daudi
(1 Nyakati 18:1-17)
1Baada ya muda, Daudi akawashinda Wafilisti na kuwatiisha, naye akatwaa Metheg-Amma kutoka mikononi mwa Wafilisti.
2Pia Daudi akawashinda Wamoabu. Akawafanya walale chini kwa mstari akawapima kwa urefu wa kamba. Kila alipopima urefu wa hiyo kamba mara mbili, hilo kundi waliuawa, na alipopima mara ya tatu aliwaacha hai. Kwa hiyo Wamoabu wakawa chini ya Daudi nao wakamletea ushuru.
3Zaidi ya hayo, Daudi akapigana na Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipoenda kurudisha tena utawala wake kwenye eneo la Mto Frati. 4Daudi akateka magari yake ya vita elfu moja, waendesha hayo magari ya vita elfu saba, na askari wa miguu elfu ishirini. Daudi akawakata mishipa farasi wa magari ya vita, akabakiza farasi mia moja.
5Waaramu wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi akawashambulia na kuwaua watu elfu ishirini na mbili miongoni mwao. 6Daudi akaweka askari walinzi katika ufalme wa Waaramu huko Dameski, nao Waaramu wakawa watumwa wake na kumlipa ushuru. Mwenyezi Mungu akampa Daudi ushindi kote alipoenda.
7Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizokuwa za maafisa wa Hadadezeri na kuzileta Yerusalemu. 8Kutoka miji ya Tibathi#8:8 mji wa Aramu-Soba ambao uliitwa Teba kwa Kiaramu; pia uliitwa Beta (1 Nyakati 18:8) na Berothai, iliyokuwa miji ya Hadadezeri, Mfalme Daudi akatwaa shaba nyingi sana.
9Tou, mfalme wa Hamathi, aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri, 10akamtuma mwanawe Yoramu kwa Mfalme Daudi kumsalimu na kumpongeza kwa ushindi wake katika vita dhidi ya Hadadezeri, kwa kuwa Hadadezeri alikuwa amepigana vita na Tou. Yoramu akamletea Daudi vyombo vya fedha, dhahabu na shaba.
11Mfalme Daudi akaviweka vifaa hivi wakfu kwa Mwenyezi Mungu, kama vile alivyokuwa amefanya kwa fedha na dhahabu kutoka kwa mataifa yote aliyokuwa ameyashinda: 12yaani Edomu, Moabu, Waamoni, Wafilisti na Waamaleki. Pia akaweka wakfu nyara alizoteka kutoka kwa Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba.
13Naye Daudi akapata sifa baada ya kurudi kutoka kuwaua Waedomu elfu kumi na nane katika Bonde la Chumvi.
14Akaweka kambi za askari walinzi katika Edomu yote, nao Waedomu wakawa chini ya Daudi. Mwenyezi Mungu alimpatia Daudi ushindi kila alipoenda.
Maafisa wa Daudi
15Daudi akatawala Israeli yote, akitenda lililo haki na sawa kwa watu wake wote. 16Yoabu mwana wa Seruya alikuwa jemadari wa jeshi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi aliweka kumbukumbu; 17Sadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; Seraya alikuwa mwandishi; 18Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa msimamizi wa Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi walikuwa washauri wa mfalme.
Iliyochaguliwa sasa
2 Samweli 8: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.