Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 20

20
Paulo apita Makedonia na Uyunani
1Baada ya zile ghasia kumalizika, Paulo aliwaita wanafunzi pamoja akawatia moyo, akawaaga, akaanza safari kwenda Makedonia. 2Alipita katika sehemu zile, akinena na watu maneno mengi ya kuwatia moyo. Ndipo hatimaye akawasili Uyunani, 3ambako alikaa kwa muda wa miezi mitatu. Kwa sababu baadhi ya Wayahudi walikuwa wamepanga njama dhidi yake alipokuwa karibu kusafiri kwa meli kwenda Siria, aliamua kurudi kupitia Makedonia. 4Paulo aliandamana na Sopatro mwana wa Piro kutoka Beroya, Aristarko na Sekundo kutoka Thesalonike, na Gayo kutoka Derbe, pia Timotheo pamoja na Tikiko na Trofimo kutoka jimbo la Asia. 5Hawa watu walitutangulia wakaenda kutungojea Troa. 6Lakini sisi tukasafiri kwa meli kwa siku tano kutoka Filipi baada ya siku za Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, nasi tukaungana na wengine huko Troa, ambako tulikaa kwa siku saba.
Eutiko afufuliwa huko Troa
7Siku ya kwanza ya juma tulikutana pamoja kwa ajili ya kumega mkate. Paulo akaongea na watu, naye kwa kuwa alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliendelea kuongea hadi usiku wa manane. 8Kwenye chumba cha ghorofani walimokuwa wamekutania kulikuwa na taa nyingi. 9Kijana mmoja jina lake Eutiko, alikuwa amekaa dirishani, wakati Paulo alipokuwa akihubiri kwa muda mrefu, alipatwa na usingizi mzito, akaanguka kutoka ghorofa ya tatu, wakamchukua akiwa amekufa. 10Paulo akashuka chini, akajitupa juu yake na kumkumbatia, akasema, “Msishtuke, bado yuko hai!” 11Kisha Paulo akapanda tena ghorofani, akamega mkate na kula. Baada ya kuongea hadi mapambazuko, akaondoka. 12Watu wakamrudisha yule kijana nyumbani akiwa hai nao wakafarijika sana.
Paulo awaaga wazee wa Efeso
13Tukatangulia kwenye meli, tukasafiri kwenda Aso ambako tungemchukua Paulo. Alikuwa amefanya utaratibu huu kwa sababu alikuwa akienda huko kwa miguu. 14Alipotukuta huko Aso, alijiunga nasi kwenye meli, tukasafiri hadi Mitilene. 15Kutoka huko tuliendelea kwa meli, na kesho yake tukafika mahali panapokabili Kio. Siku iliyofuata tukavuka kwenda Samo, na kesho yake tukawasili Mileto. 16Paulo alikuwa ameamua tusipitie Efeso ili asitumie muda mwingi huko jimbo la Asia. Alikuwa na haraka ya kufika Yerusalemu kabla ya siku ya Pentekoste kama ingewezekana.
17Paulo akiwa Mileto, alituma mjumbe kwenda Efeso kuwaita wazee wa kundi la waumini waje wakutane naye. 18Walipofika akawaambia, “Ninyi wenyewe mnajua jinsi nilivyoishi muda wote nilikuwa nanyi, tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa jimbo la Asia. 19Nilimtumikia Bwana Isa kwa unyenyekevu wote na kwa machozi nikivumilia taabu na mapingamizi yaliyonipata kutokana na hila za Wayahudi. 20Mnajua kwamba sikusita kuhubiri jambo lolote ambalo lingekuwa la kuwafaa ninyi, lakini nilifundisha hadharani na nyumba kwa nyumba. 21Nimewashuhudia Wayahudi na Wayunani kwamba inawapasa kumgeukia Mungu kwa kutubu dhambi na kumwamini Bwana wetu Isa Al-Masihi.
22“Nami sasa nimesukumwa na Roho wa Mungu, ninaenda Yerusalemu wala sijui ni nini kitakachonipata huko. 23Ila ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu wa Mungu amenionya kuwa vifungo na mateso vinaningoja. 24Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani kwangu, kama kuyamaliza mashindano na kukamilisha ile kazi Bwana Isa aliyonipa, yaani kazi ya kuishuhudia Injili ya neema ya Mungu.
25“Nami sasa najua kuwa hakuna hata mmoja miongoni mwenu niliowahubiria ufalme wa Mungu atakayeniona tena. 26Kwa hiyo nawatangazia leo, sina hatia ya damu ya mtu yeyote. 27Kwa kuwa sikusita kuwatangazia mapenzi yote ya Mungu. 28Jilindeni nafsi zenu na mlilinde lile kundi lote ambalo Roho wa Mungu amewaweka ninyi kuwa waangalizi wake. Chungeni jumuiya ya waumini ya Mungu, aliowanunua kwa damu yake mwenyewe. 29Najua kwamba baada yangu kuondoka, mbwa-mwitu wakali watakuja kati yenu, ambao hawatalihurumia kundi. 30Hata kutoka miongoni mwenu watainuka watu na kuupotosha ukweli ili wawavute wanafunzi wawafuate. 31Hivyo jilindeni! Kumbukeni kwamba kwa miaka mitatu sikuacha kamwe kuwaonya kila mmoja kwa machozi usiku na mchana.
32“Sasa nawakabidhi kwa Mungu na kwa neno la neema yake, linaloweza kuwajenga na kuwapa ninyi urithi miongoni mwa wote ambao wametakaswa. 33Sikutamani fedha wala dhahabu wala vazi la mtu yeyote. 34Ninyi wenyewe mnajua kwamba mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. 35Katika kila jambo nimewaonesha kwamba kwa njia hii ya kufanya kazi kwa bidii imetupasa kuwasaidia wadhaifu, mkikumbuka maneno ya Bwana Isa mwenyewe jinsi alivyosema, ‘Ni heri kutoa kuliko kupokea.’ ”
36Paulo alipomaliza kusema haya akapiga magoti pamoja nao wote akaomba. 37Wote wakalia, wakamkumbatia Paulo na kumbusu. 38Kilichowahuzunisha zaidi ni kwa sababu ya yale maneno aliyosema kwamba kamwe hawatauona uso wake tena. Wakaenda naye hadi kwenye meli.

Iliyochaguliwa sasa

Matendo 20: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia