Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 21

21
Paulo aenda Yerusalemu
1Tulipokwisha kujitenga nao, tukasafiri kwa meli moja kwa moja hadi Kosi. Siku ya pili yake tukafika Rodo, na kutoka huko tukaenda Patara. 2Hapo tukapata meli iliyokuwa inavuka kwenda Foinike tukapanda tukasafiri nayo. 3Tulipokiona kisiwa cha Kipro, tukakizunguka tukakiacha upande wetu wa kushoto, tukasafiri hadi Siria. Tukatia nanga katika bandari ya Tiro, ambapo meli yetu ilikuwa ipakue shehena yake. 4Baada ya kuwatafuta wanafunzi wa huko, tukakaa nao kwa siku saba. Wale wanafunzi wakiongozwa na Roho wa Mungu wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu. 5Lakini muda wetu ulipokwisha, tukaondoka tukaendelea na safari yetu. Wale wanafunzi pamoja na wake zao na watoto wakatusindikiza hadi nje ya mji. Wote tukapiga magoti pale pwani tukaomba. 6Baada ya kuagana, tukapanda kwenye meli, nao wakarudi manyumbani mwao.
7Tukaendelea na safari yetu toka Tiro tukafika Tolemai, tukawasalimu ndugu wa huko, tukakaa nao kwa siku moja. 8Siku iliyofuata tukaondoka, tukafika Kaisaria. Huko tukaenda nyumbani mwa mwinjilisti mmoja jina lake Filipo, aliyekuwa mmoja wa wale Saba, tukakaa kwake. 9Filipo alikuwa na binti wanne mabikira waliokuwa wanatoa unabii.
10Baada ya kukaa kwa siku kadhaa, nabii aliyeitwa Agabo akateremka kutoka Yudea. 11Alipotufikia, akachukua mshipi wa Paulo, akajifunga, akautumia kufunga mikono na miguu yake mwenyewe, akasema, “Roho wa Mungu anasema: ‘Hivi ndivyo viongozi wa Wayahudi huko Yerusalemu watakavyomfunga mwenye mshipi huu na kumkabidhi kwa watu wa Mataifa.’ ”
12Tuliposikia maneno haya sisi na ndugu wengine tukamsihi Paulo asiende Yerusalemu. 13Lakini Paulo akajibu, “Kwa nini mnalia na kunivunja moyo? Mimi niko tayari si kufungwa tu, bali hata kufa huko Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana Isa.” 14Alipokataa kushawishika, tukaacha kumsihi, tukasema, “Mapenzi ya Mwenyezi Mungu na yatendeke.”
15Baada ya haya, tukajiandaa, tukaondoka kwenda Yerusalemu. 16Baadhi ya wanafunzi kutoka Kaisaria wakafuatana nasi na kutupeleka nyumbani mwa Mnasoni, ambaye tungekaa kwake. Yeye alikuwa mtu wa Kipro, mmoja wa wanafunzi wa zamani.
Kukamatwa kwa Paulo, na safari yake kwenda Rumi
(Matendo 21:17–28:31)
Paulo awasili Yerusalemu
17Tulipofika Yerusalemu, ndugu wakatukaribisha kwa furaha. 18Kesho yake Paulo pamoja na wengine wetu tulienda kumwona Yakobo, na wazee wote walikuwako. 19Baada ya kuwasalimu, Paulo akatoa taarifa kamili ya mambo yote ambayo Mungu alikuwa amefanya miongoni mwa watu wa Mataifa kupitia huduma yake.
20Baada ya kusikia mambo haya, wakamsifu Mungu. Ndipo wakamwambia Paulo, “Ndugu, unaona kulivyo na maelfu ya Wayahudi walioamini, nao wote wana juhudi kwa ajili ya sheria. 21Lakini wameambiwa habari zako kwamba unafundisha Wayahudi wote wanaoishi miongoni mwa watu wa Mataifa kumkataa Musa, na kwamba unawaambia wasiwatahiri watoto wao wala kufuata desturi zetu. 22Sasa tufanyeje? Bila shaka watasikia kwamba umekuja Yerusalemu. 23Kwa hiyo fanya lile tunalokuambia. Tuna watu wanne hapa ambao wameweka nadhiri. 24Jiunge na watu hawa, mfanye utaratibu wa ibada ya kujitakasa pamoja nao, na ulipe gharama ili wanyoe nywele zao. Kwa njia hii kila mtu atafahamu ya kuwa mambo waliyosikia si ya kweli na kwamba wewe unaishika sheria. 25Lakini kuhusu wale watu wa Mataifa walioamini, tumewaandikia uamuzi wetu: kwamba wajitenge na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na wajiepushe na uasherati.”
26Ndipo kesho yake Paulo akaenda na wale watu, akajitakasa pamoja nao. Akaingia ndani ya Hekalu ili atoe taarifa ya tarehe ambayo siku zao za utakaso zingemalizika na sadaka ingetolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.
Paulo akamatwa
27Zile siku saba zilipokaribia kumalizika, baadhi ya Wayahudi kutoka jimbo la Asia waliokuwa wamemwona Paulo ndani ya Hekalu, wakachochea umati wote wa watu, nao wakamkamata. 28Wakapiga kelele wakisema, “Waisraeli wenzetu, tusaidieni! Huyu ndiye yule mtu anayefundisha kila mtu na kila mahali, kinyume na watu wetu, sheria zetu na hata Hekalu hili. Zaidi ya hayo amewaleta Wayunani ndani ya Hekalu na kupanajisi mahali hapa patakatifu.” 29(Walikuwa wamemwona Trofimo Mwefeso, akiwa mjini pamoja na Paulo, wakadhani kuwa Paulo alikuwa amemwingiza Hekaluni.)
30Mji wote ukataharuki, watu wakaja wakikimbia kutoka pande zote wakamkamata Paulo, wakamburuta kutoka Hekaluni. Milango ya Hekalu ikafungwa. 31Walipokuwa wakitaka kumuua, habari zikamfikia jemadari wa jeshi la askari Warumi kwamba mji wa Yerusalemu wote ulikuwa katika machafuko. 32Mara yule jemadari akachukua maafisa wengine wa jeshi pamoja na askari, wakakimbia kwenye ule umati wa watu. Wale watu waliokuwa wakifanya ghasia walipomwona yule jemadari na askari wakija, wakaacha kumpiga Paulo.
33Yule jemadari akaja, akamkamata Paulo akaamuru afungwe kwa minyororo miwili. Akauliza yeye ni nani, na alikuwa amefanya nini. 34Baadhi ya watu katika umati ule wakapiga kelele, hawa wakisema hili na wengine lile. Yule jemadari alipoona kuwa hawezi kupata hakika ya habari kwa sababu ya taharuki, akaamuru Paulo apelekwe katika ngome ya jeshi. 35Paulo alipofika penye ngazi, ilibidi askari wambebe juu juu kwa sababu fujo za umati ule wa watu zilikuwa kubwa. 36Umati wa watu waliofuata waliendelea kupaza sauti na kusema, “Mwondoe huyu!”
Paulo anajitetea
37Mara tu Paulo alipokaribia kuingizwa kwenye ngome ya jeshi, akamwambia yule jemadari, “Je, naweza kukuambia jambo moja?”
Yule jemadari akamjibu, “Je, unajua Kiyunani? 38Je, wewe si yule Mmisri ambaye siku hizi za karibuni alianzisha uasi akaongoza kundi la magaidi elfu nne wenye silaha jangwani?”
39Paulo akajibu, “Mimi ni Myahudi kutoka Tarso huko Kilikia, raia wa mji maarufu. Tafadhali niruhusu nizungumze na hawa watu.”
40Baada ya kupata ruhusa kwa yule jemadari, Paulo akasimama penye ngazi, akawapungia watu mkono ili wanyamaze. Wote waliponyamaza, Paulo akazungumza nao kwa lugha ya Kiebrania, akasema:

Iliyochaguliwa sasa

Matendo 21: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia