Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 21:27-40

Matendo 21:27-40 NENO

Zile siku saba zilipokaribia kumalizika, baadhi ya Wayahudi kutoka jimbo la Asia waliokuwa wamemwona Paulo ndani ya Hekalu, wakachochea umati wote wa watu, nao wakamkamata. Wakapiga kelele wakisema, “Waisraeli wenzetu, tusaidieni! Huyu ndiye yule mtu anayefundisha kila mtu na kila mahali, kinyume na watu wetu, sheria zetu na hata Hekalu hili. Zaidi ya hayo amewaleta Wayunani ndani ya Hekalu na kupanajisi mahali hapa patakatifu.” (Walikuwa wamemwona Trofimo Mwefeso, akiwa mjini pamoja na Paulo, wakadhani kuwa Paulo alikuwa amemwingiza Hekaluni.) Mji wote ukataharuki, watu wakaja wakikimbia kutoka pande zote wakamkamata Paulo, wakamburuta kutoka Hekaluni. Milango ya Hekalu ikafungwa. Walipokuwa wakitaka kumuua, habari zikamfikia jemadari wa jeshi la askari Warumi kwamba mji wa Yerusalemu wote ulikuwa katika machafuko. Mara yule jemadari akachukua maafisa wengine wa jeshi pamoja na askari, wakakimbia kwenye ule umati wa watu. Wale watu waliokuwa wakifanya ghasia walipomwona yule jemadari na askari wakija, wakaacha kumpiga Paulo. Yule jemadari akaja, akamkamata Paulo akaamuru afungwe kwa minyororo miwili. Akauliza yeye ni nani, na alikuwa amefanya nini. Baadhi ya watu katika umati ule wakapiga kelele, hawa wakisema hili na wengine lile. Yule jemadari alipoona kuwa hawezi kupata hakika ya habari kwa sababu ya taharuki, akaamuru Paulo apelekwe katika ngome ya jeshi. Paulo alipofika penye ngazi, ilibidi askari wambebe juu juu kwa sababu fujo za umati ule wa watu zilikuwa kubwa. Umati wa watu waliofuata waliendelea kupaza sauti na kusema, “Mwondoe huyu!” Mara tu Paulo alipokaribia kuingizwa kwenye ngome ya jeshi, akamwambia yule jemadari, “Je, naweza kukuambia jambo moja?” Yule jemadari akamjibu, “Je, unajua Kiyunani? Je, wewe si yule Mmisri ambaye siku hizi za karibuni alianzisha uasi akaongoza kundi la magaidi elfu nne wenye silaha jangwani?” Paulo akajibu, “Mimi ni Myahudi kutoka Tarso huko Kilikia, raia wa mji maarufu. Tafadhali niruhusu nizungumze na hawa watu.” Baada ya kupata ruhusa kwa yule jemadari, Paulo akasimama penye ngazi, akawapungia watu mkono ili wanyamaze. Wote waliponyamaza, Paulo akazungumza nao kwa lugha ya Kiebrania, akasema