Amosi 5:1-9
Amosi 5:1-9 NEN
Sikia neno hili, ee nyumba ya Israeli, ombolezo hili ninalifanya kuwahusu ninyi: “Bikira Israeli ameanguka, kamwe hatainuka tena, ameachwa pweke katika nchi yake, hakuna yeyote wa kumwinua.” Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “Wakati mmoja wa miji yako utakapopeleka watu elfu moja vitani kwa ajili ya Israeli, mia moja tu watarudi; wakati mji utakapopeleka mia moja, kumi tu ndio watarudi hai.” Hili ndilo BWANA asemalo kwa nyumba ya Israeli: “Nitafuteni mpate kuishi; msitafute Betheli, msiende Gilgali, msisafiri kwenda Beer-Sheba. Kwa maana kwa hakika Gilgali itakwenda uhamishoni, na Betheli itafanywa kuwa si kitu.” Mtafuteni BWANA mpate kuishi, au atafagia nyumba ya Yosefu kama moto; utawateketeza, nayo Betheli haitakuwa na yeyote wa kuuzima. Ninyi ambao mnageuza haki kuwa uchungu na kuiangusha haki chini (yeye ambaye alifanya Kilimia na Orioni, ambaye hugeuza giza kuwa mapambazuko na mchana kuwa usiku, ambaye huyaita maji ya bahari na kuyamwaga juu ya uso wa nchi: BWANA ndilo jina lake; yeye hufanya maangamizo kwenye ngome na kufanya mji uliozungushiwa ngome kuwa ukiwa)