Amosi 5:1-9
Amosi 5:1-9 BHN
Sikilizeni maombolezo yangu juu yenu, enyi Waisraeli: Umeanguka na hutainuka tena ewe binti Israeli! Umeachwa pweke nchini mwako, hamna hata mtu wa kukuinua. Maana Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu 1,000 watatoka mjini kwenda kupigana lakini watarejea 100 tu; wataondoka watu 100 wa kijiji kimoja lakini watanusurika watu kumi tu.” Mwenyezi-Mungu awaambia hivi Waisraeli: “Nitafuteni mimi nanyi mtaishi! Lakini msinitafute huko Betheli wala msiende Gilgali wala msivuke kwenda Beer-sheba. Maana wakazi wa Gilgali, hakika watachukuliwa uhamishoni, na Betheli utaangamizwa!” Mtafuteni Mwenyezi-Mungu, nanyi mtaishi! La sivyo, atawalipukia wazawa wa Yosefu kama moto; moto utawateketeza wakazi wa Betheli na hakuna mtu atakayeweza kuuzima. Tahadhari enyi mnaogeuza haki kuwa uchungu, na kuuona uadilifu kuwa kama takataka! Huyo aliyezifanya Kilimia na sayari Orioni, ambaye huligeuza giza nene kuwa mchana, na mchana kuwa usiku; yeye ambaye ayaitaye pamoja maji ya bahari na kuyamwaga juu ya nchi kavu, Mwenyezi-Mungu ndilo jina lake. Yeye ndiye anayewaangamiza wenye nguvu, na kuziharibu ngome zao.