Amosi 6:1-14
Amosi 6:1-14 NEN
Ole wenu ninyi mnaostarehe na kuridhika katika Sayuni, na ninyi mnaojisikia salama juu ya Mlima Samaria, ninyi watu mashuhuri wa taifa lililoendelea kuliko mataifa mengine, ambao watu wa Israeli wanawategemea! Nendeni Kalne mkaone kutoka huko; mwende hadi Hamathi iliyo kuu, kisha mshuke hadi Gathi ya Wafilisti. Je, wao ni bora kuliko falme zenu mbili? Je, nchi yao ni kubwa kuliko yenu? Mnaiweka mbali siku iliyo mbaya na kuleta karibu utawala wa kuogofya. Ninyi mnalala juu ya vitanda vilivyofunikwa kwa pembe za ndovu, na kujinyoosha juu ya viti vya fahari. Mnajilisha kwa wana-kondoo wazuri na ndama walionenepeshwa. Ninyi mnapiga vinubi kama Daudi, huku mkitunga nyimbo za vinanda mbalimbali. Mnakunywa mvinyo kwa bakuli zilizojazwa, na mnajipaka mafuta mazuri, lakini hamhuzuniki kwa maangamizi ya Yosefu. Kwa hiyo mtakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kwenda uhamishoni; karamu zenu na kustarehe kutakoma. BWANA BWANA Mwenyezi ameapa kwa nafsi yake mwenyewe: BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote asema: “Nachukia kiburi cha Yakobo, nachukia ngome zake; nitautoa mji wao na kila kitu kilichomo ndani mwake.” Kama watu kumi watabaki katika nyumba moja, wao pia watakufa. Kama jamaa ambaye atachoma miili akija ili kuitoa nje ya nyumba, na kumuuliza yeyote ambaye bado anajificha humo, “Je, yuko mtu yeyote pamoja nawe?” Naye akisema, “Hapana,” ndipo atakaposema, “Nyamaza kimya! Haturuhusiwi kutaja jina la BWANA.” Kwa kuwa BWANA ameamuru, naye atabomoa jumba kubwa vipande vipande na nyumba ndogo vipande vidogo vidogo. Je, farasi waweza kukimbia kwenye miamba mikali? Je, aweza mtu kulima huko kwa maksai? Lakini mmegeuza haki kuwa sumu na matunda ya uadilifu kuwa uchungu: ninyi mnaoshangilia kushindwa kwa Lo-Debari na kusema, “Je, hatukuteka Karnaimu kwa nguvu zetu wenyewe?” Maana BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote asema, “Nitainua taifa dhidi yenu, ee nyumba ya Israeli, nalo litawatesa kuanzia Lebo-Hamathi hadi Bonde la Araba.”