Amosi 6:1-14
Amosi 6:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ole wao wanaostarehe katika Sayuni, na hao wanaokaa salama katika mlima wa Samaria, watu mashuhuri wa taifa lililo la kwanza, ambao nyumba ya Israeli huwaendea. Piteni hata Kalne, mkaone; tena tokea huko enendeni hata Hamathi iliyo kuu; kisha shukeni hata Gathi ya Wafilisti; je! Ninyi ni bora kuliko falme hizi? Au mpaka wao ni mkubwa kuliko mpaka wenu? Ninyi mnaoiweka mbali siku hiyo mbaya, na kulileta karibu kao la udhalimu; ninyi mnaolala juu ya vitanda vya pembe, na kujinyosha juu ya masemadari yenu; ninyi mnaokula wana-kondoo wa kundi, na ndama waliomo zizini; ninyi mnaoimba nyimbo za upuzi pamoja na sauti ya vinanda, na kujifanyizia vinanda vya namna nyingi, kama vile Daudi; ninyi mnaokunywa divai katika mabakuli, na kujipaka marhamu iliyo nzuri; lakini hawahuzuniki kwa sababu ya mateso ya Yusufu. Basi kwa ajili ya hayo sasa watakwenda utumwani pamoja na wa kwanza watakaokwenda utumwani, na kelele za machezo za hao waliojinyosha zitakoma. Bwana MUNGU ameapa kwa nafsi yake, asema BWANA, Mungu wa majeshi; Naizira fahari ya Yakobo, nachukizwa na majumba yake; kwa sababu hiyo nitautoa huo mji, pamoja na wote waliomo ndani yake. Hata itakuwa, wakisalia wanaume kumi katika nyumba moja, watakufa. Na mjomba wa mtu atakapomwinua, yaani, yeye amchomaye moto, ili atoe mifupa yake nyumbani, naye atakapomwambia yeye aliye katika pande za ndani za nyumba, Je! Yuko mtu ye yote pamoja nawe? Naye atakaposema, La, hapana; ndipo atasema, Nyamaza kimya; maana hatuna ruhusa kulitaja jina la BWANA. Kwa maana, angalia, BWANA atoa amri, na nyumba kubwa itapigwa na kuwa na mahali palipobomolewa, na nyumba ndogo nayo itapigwa iwe na nyufa. Je! Farasi watapiga mbio juu ya mwamba? Je! Mtu atalima na ng’ombe huko? Hata mmegeuza hukumu kuwa uchungu, na matunda ya haki kuwa pakanga; ninyi mnaolifurahia jambo lisilo na maana, msemao, Je! Hatukujipatia pembe kwa nguvu zetu wenyewe? Maana, angalia, nitaondokesha taifa juu yenu, enyi nyumba ya Israeli, asema BWANA, Mungu wa majeshi, nao watawatesa ninyi toka mahali pa kuingilia katika Hamathi hata kijito cha Araba.
Amosi 6:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Ole wenu nyinyi mnaostarehe huko Siyoni, nanyi mnaojiona salama mlimani Samaria! Nyinyi mwaonekana kuwa viongozi wa taifa maarufu ambao Waisraeli wote huwategemea. Haya! Nendeni Kalne mkaangalie kila mahali, tokeni huko mwende hadi mji ule mkubwa wa Hamathi, kisha teremkeni hadi Gathi kwa Wafilisti. Je, falme zao si bora kuliko zenu na eneo lao si bora kuliko lenu?” Nyinyi mnajaribu kuifukuza siku mbaya. Lakini mnauleta karibu utawala dhalimu. Ole wenu mnaolala juu ya vitanda vya pembe za ndovu na kujinyosha juu ya masofa, mkila nyama za wanakondoo na ndama! Nyinyi mnapenda kuimba ovyo na sauti ya vinubi na kubuni ala mpya za muziki mkimwiga mfalme Daudi. Mnakunywa divai kwa mabakuli, na kujipaka marashi mazuri mno. Lakini hamhuzuniki hata kidogo juu ya kuangamia kwa wazawa wa Yosefu. Kwa hiyo mtakuwa wa kwanza kwenda uhamishoni, na karamu za wenye kustarehe zitatoweka. Bwana Mwenyezi-Mungu ameapa kwa nafsi yake; Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi asema: “Nachukizwa mno na kiburi cha wazawa wa Yakobo; tena nayachukia majumba yao ya fahari. Mji wao na vyote vilivyomo nitawapa adui zao.” Kama wakibaki watu kumi katika nyumba moja, wote watakufa. Na atakapokuja mjomba wa aliyekufa kuitoa maiti nje aichome, akamwuliza yeyote atakayekuwako ndani pembeni mwa nyumba, “Je kuna mtu mwingine pamoja nawe?” Naye atamjibu, “La! Hamna!” Naye atamwambia, “Nyamaza kimya! Tusilitaje hata jina la Mwenyezi-Mungu.” Tazama! Mwenyezi-Mungu anatoa amri, nalo jumba kubwa labomoka vipandevipande, na nyumba ndogo kusagikasagika. Je, farasi waweza kupiga mbio miambani? Je, watu huilima bahari kwa ng'ombe? Lakini nyinyi mmeigeuza haki kuwa sumu, na tunda la uadilifu kuwa uchungu. Nyinyi mnashangilia juu ya Lodebari, na kusema mmeuteka Karnaimu kwa nguvu zenu wenyewe. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Enyi Waisraeli, kweli nitaleta taifa moja lije kuwashambulia, nalo litawatesa nyinyi kuanzia Lebo-hamathi kaskazini, hadi kijito cha Araba, upande wa kusini.”
Amosi 6:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ole wao wanaostarehe katika Sayuni, na hao wanaokaa salama katika mlima wa Samaria, watu mashuhuri wa taifa lililo la kwanza, ambao nyumba ya Israeli huwaendea. Piteni hadi Kalne, mkaone; tena tokea huko nendeni hadi Hamathi iliyo kuu; kisha shukeni hadi Gathi ya Wafilisti; je! Ninyi ni bora kuliko falme hizi? Au eneo lao ni kubwa kuliko eneo lenu? Ninyi mnaoiweka mbali siku hiyo mbaya, na kulileta karibu kao la udhalimu; ninyi mnaolala juu ya vitanda vya pembe, na kujinyosha juu ya makochi yenu; ninyi mnaokula wana-kondoo wa kundi, na ndama waliomo zizini; ninyi mnaoimba nyimbo za upuzi pamoja na sauti ya vinanda, na kujifanyia vinanda vya namna nyingi, kama vile Daudi; ninyi mnaokunywa divai katika mabakuli, na kujipaka marhamu iliyo nzuri; lakini hawahuzuniki kwa sababu ya mateso ya Yusufu. Basi kwa ajili ya hayo sasa watakwenda utumwani pamoja na wa kwanza watakaokwenda utumwani, na kelele za shangwe za hao waliojinyosha zitakoma. Bwana MUNGU ameapa kwa nafsi yake, asema BWANA, Mungu wa majeshi; Naizira fahari ya Yakobo, nachukizwa na majumba yake; kwa sababu hiyo nitautoa huo mji, pamoja na wote waliomo ndani yake. Hata itakuwa, wakisalia wanaume kumi katika nyumba moja, watakufa. Na mjomba wa mtu atakapomwinua, yaani, yeye amchomaye moto, ili atoe mifupa yake nyumbani, naye atakapomwambia yeye aliye katika pande za ndani za nyumba, Je! Yuko mtu yeyote pamoja nawe? Naye atakaposema, La, hapana; ndipo atasema, Nyamaza kimya; maana hatuna ruhusa kulitaja jina la BWANA. Kwa maana, angalia, BWANA atoa amri, na jumba kuu litabomolewa vipande vipande, na nyumba ndogo kuwa vigae. Je! Farasi watapiga mbio juu ya mwamba? Je! Mtu atalima kwa plau na ng'ombe baharini? Hata mmegeuza hukumu kuwa sumu, na matunda ya haki kuwa uchungu; ninyi mnaolifurahia jambo lisilo na maana, msemao, Je! Hatukujipatia pembe kwa nguvu zetu wenyewe? Maana, angalia, nitaleta taifa juu yenu, enyi nyumba ya Israeli, asema BWANA, Mungu wa majeshi, nao watawatesa ninyi toka mahali pa kuingilia katika Hamathi hata kijito cha Araba.
Amosi 6:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ole wenu ninyi mnaostarehe na kuridhika katika Sayuni, na ninyi mnaojisikia salama juu ya Mlima Samaria, ninyi watu mashuhuri wa taifa lililoendelea kuliko mataifa mengine, ambao watu wa Israeli wanawategemea! Nendeni Kalne mkaone kutoka huko; mwende hadi Hamathi iliyo kuu, kisha mshuke hadi Gathi ya Wafilisti. Je, wao ni bora kuliko falme zenu mbili? Je, nchi yao ni kubwa kuliko yenu? Mnaiweka mbali siku iliyo mbaya na kuleta karibu utawala wa kuogofya. Ninyi mnalala juu ya vitanda vilivyofunikwa kwa pembe za ndovu, na kujinyoosha juu ya viti vya fahari. Mnajilisha kwa wana-kondoo wazuri na ndama walionenepeshwa. Ninyi mnapiga vinubi kama Daudi, huku mkitunga nyimbo za vinanda mbalimbali. Mnakunywa mvinyo kwa bakuli zilizojazwa, na mnajipaka mafuta mazuri, lakini hamhuzuniki kwa maangamizi ya Yosefu. Kwa hiyo mtakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kwenda uhamishoni; karamu zenu na kustarehe kutakoma. BWANA BWANA Mwenyezi ameapa kwa nafsi yake mwenyewe: BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote asema: “Nachukia kiburi cha Yakobo, nachukia ngome zake; nitautoa mji wao na kila kitu kilichomo ndani mwake.” Kama watu kumi watabaki katika nyumba moja, wao pia watakufa. Kama jamaa ambaye atachoma miili akija ili kuitoa nje ya nyumba, na kumuuliza yeyote ambaye bado anajificha humo, “Je, yuko mtu yeyote pamoja nawe?” Naye akisema, “Hapana,” ndipo atakaposema, “Nyamaza kimya! Haturuhusiwi kutaja jina la BWANA.” Kwa kuwa BWANA ameamuru, naye atabomoa jumba kubwa vipande vipande na nyumba ndogo vipande vidogo vidogo. Je, farasi waweza kukimbia kwenye miamba mikali? Je, aweza mtu kulima huko kwa maksai? Lakini mmegeuza haki kuwa sumu na matunda ya uadilifu kuwa uchungu: ninyi mnaoshangilia kushindwa kwa Lo-Debari na kusema, “Je, hatukuteka Karnaimu kwa nguvu zetu wenyewe?” Maana BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote asema, “Nitainua taifa dhidi yenu, ee nyumba ya Israeli, nalo litawatesa kuanzia Lebo-Hamathi hadi Bonde la Araba.”