Amosi 6:1-14
Amosi 6:1-14 BHN
Ole wenu nyinyi mnaostarehe huko Siyoni, nanyi mnaojiona salama mlimani Samaria! Nyinyi mwaonekana kuwa viongozi wa taifa maarufu ambao Waisraeli wote huwategemea. Haya! Nendeni Kalne mkaangalie kila mahali, tokeni huko mwende hadi mji ule mkubwa wa Hamathi, kisha teremkeni hadi Gathi kwa Wafilisti. Je, falme zao si bora kuliko zenu na eneo lao si bora kuliko lenu?” Nyinyi mnajaribu kuifukuza siku mbaya. Lakini mnauleta karibu utawala dhalimu. Ole wenu mnaolala juu ya vitanda vya pembe za ndovu na kujinyosha juu ya masofa, mkila nyama za wanakondoo na ndama! Nyinyi mnapenda kuimba ovyo na sauti ya vinubi na kubuni ala mpya za muziki mkimwiga mfalme Daudi. Mnakunywa divai kwa mabakuli, na kujipaka marashi mazuri mno. Lakini hamhuzuniki hata kidogo juu ya kuangamia kwa wazawa wa Yosefu. Kwa hiyo mtakuwa wa kwanza kwenda uhamishoni, na karamu za wenye kustarehe zitatoweka. Bwana Mwenyezi-Mungu ameapa kwa nafsi yake; Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi asema: “Nachukizwa mno na kiburi cha wazawa wa Yakobo; tena nayachukia majumba yao ya fahari. Mji wao na vyote vilivyomo nitawapa adui zao.” Kama wakibaki watu kumi katika nyumba moja, wote watakufa. Na atakapokuja mjomba wa aliyekufa kuitoa maiti nje aichome, akamwuliza yeyote atakayekuwako ndani pembeni mwa nyumba, “Je kuna mtu mwingine pamoja nawe?” Naye atamjibu, “La! Hamna!” Naye atamwambia, “Nyamaza kimya! Tusilitaje hata jina la Mwenyezi-Mungu.” Tazama! Mwenyezi-Mungu anatoa amri, nalo jumba kubwa labomoka vipandevipande, na nyumba ndogo kusagikasagika. Je, farasi waweza kupiga mbio miambani? Je, watu huilima bahari kwa ng'ombe? Lakini nyinyi mmeigeuza haki kuwa sumu, na tunda la uadilifu kuwa uchungu. Nyinyi mnashangilia juu ya Lodebari, na kusema mmeuteka Karnaimu kwa nguvu zenu wenyewe. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Enyi Waisraeli, kweli nitaleta taifa moja lije kuwashambulia, nalo litawatesa nyinyi kuanzia Lebo-hamathi kaskazini, hadi kijito cha Araba, upande wa kusini.”