Amosi 8
8
Maono ya nne: Kikapu cha matunda yaliyoiva
1Hili ndilo alilonionesha Bwana Mungu Mwenyezi katika maono: kikapu cha matunda yaliyoiva. 2Akaniuliza, “Amosi, unaona nini?”
Nikajibu, “Kikapu chenye matunda yaliyoiva.”
Ndipo Mwenyezi Mungu akaniambia, “Wakati umewadia kwa watu wangu Israeli; sitawahurumia zaidi.”
3Bwana Mungu Mwenyezi asema, “Katika siku ile, nyimbo katika Hekalu zitageuka kuwa maombolezo. Miili mingi, mingi sana: itatupwa kila mahali! Kimya!”
4Lisikieni hili, ninyi ambao mnawagandamiza wahitaji,
na kuwaonea maskini wa nchi,
5mkisema,
“Ni lini Mwezi Mwandamo utakapopita
ili tupate kuuza nafaka,
na Sabato itakwisha lini
ili tuweze kuuza ngano?”
Mkipunguza vipimo,
na kuongeza bei,
na kudanganya kwa mizani zisizo sawa,
6mkiwanunua maskini kwa fedha,
na wahitaji kwa jozi ya viatu,
na mkiuza hata takataka za ngano
pamoja na ngano.
7Mwenyezi Mungu ameapa kwake mwenyewe, aliye Fahari ya Yakobo: “Kamwe sitasahau chochote ambacho wamefanya.
8“Je, nchi haitatetemeka kwa ajili ya hili,
nao wote wanaoishi ndani yake hawataomboleza?
Nchi yote itainuka kama Mto Naili;
itapanda na kushuka kama mto wa Misri.
9“Katika siku ile,” asema Bwana Mungu Mwenyezi,
“Nitalifanya jua litue alasiri na kuifanya dunia
iwe giza wakati wa mchana mwangavu.
10Nitageuza sikukuu zenu za kidini kuwa maombolezo,
na kuimba kwenu kote kuwe kilio.
Nitawafanya ninyi nyote mvae magunia
na kunyoa nywele zenu.
Nitaufanya wakati ule uwe kama wa kuombolezea mwana wa pekee,
na mwisho wake kama siku ya uchungu.
11“Siku zinakuja,” asema Bwana Mungu Mwenyezi,
“wakati nitakapotuma njaa katika nchi yote:
si njaa ya chakula wala kiu ya maji,
lakini njaa ya kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu.
12Wanaume watayumbayumba kutoka bahari hadi bahari
na kutangatanga kutoka kaskazini mpaka mashariki,
wakitafuta neno la Mwenyezi Mungu,
lakini hawatalipata.
13“Katika siku ile
“wasichana wazuri na wavulana wenye nguvu
watazimia kwa sababu ya kiu.
14Wale waapao kwa aibu ya Samaria,
au kusema, ‘Hakika kama miungu yenu iishivyo, ee Dani,’
au ‘Hakika kama mungu wa Beer-Sheba aishivyo’:
wataanguka, wala hawatasimama tena.”
Iliyochaguliwa sasa
Amosi 8: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.