Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Amosi 7

7
Maono ya kwanza: Nzige
1Hili ndilo alilonionesha Bwana Mungu Mwenyezi katika maono: Alikuwa anaandaa makundi ya nzige baada ya kuvunwa fungu la mfalme na wakati ule tu mimea ya pili ilipokuwa ikichipua. 2Wakati nzige walikuwa wamekula mimea yote ya nchi, nililia kwa sauti kuu, “Bwana Mungu Mwenyezi, samehe! Je, Yakobo atawezaje kuendelea kuishi? Yeye ni mdogo sana!”
3Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akaghairi.
Kisha Mwenyezi Mungu akasema, “Hili halitatokea.”
Maono ya pili: Moto
4Hili ndilo Bwana Mungu Mwenyezi alilonionesha katika maono: Bwana Mungu Mwenyezi alikuwa akiita hukumu ya moto; nao ulikausha vilindi vikuu, ukateketeza nchi. 5Ndipo nikalia, “Bwana Mungu Mwenyezi, nakusihi, zuia! Je, Yakobo atawezaje kuendelea kuishi? Yeye ni mdogo sana!”
6Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akaghairi.
Bwana Mungu Mwenyezi akasema, “Hili nalo halitatokea.”
Maono ya tatu: Timazi
7Hili ndilo alilonionesha katika maono: Bwana alikuwa amesimama karibu na ukuta ambao ulikuwa umejengwa kwa timazi, akiwa na uzi wa timazi mkononi mwake. 8Naye Mwenyezi Mungu akaniuliza, “Je, Amosi unaona nini?”
Nikamjibu, “Uzi wa timazi.”
Kisha Bwana akasema, “Tazama, ninaweka uzi wa timazi miongoni mwa watu wangu Israeli; sitawahurumia tena.
9“Mahali pa Isaka pa juu pa kuabudia pataangamizwa,
na mahali patakatifu pa Israeli pa kuabudia pataharibiwa;
kwa upanga wangu nitainuka
dhidi ya nyumba ya Yeroboamu.”
Amosi na Amazia
10Kisha Amazia kuhani wa Betheli akatuma ujumbe kwa Yeroboamu mfalme wa Israeli, akisema: “Amosi analeta fitina juu yako katikati ya Israeli. Nchi haiwezi kuvumilia maneno yake yote. 11Kwa kuwa hili ndilo Amosi analosema:
“ ‘Yeroboamu atakufa kwa upanga,
na kwa hakika Israeli wataenda uhamishoni,
mbali na nchi yao.’ ”
12Kisha Amazia akamwambia Amosi, “Nenda zako, ewe mwonaji! Urudi katika nchi ya Yuda. Ujipatie riziki yako huko na kutoa unabii wako. 13Usiendelee kutoa unabii katika Betheli, kwa sababu hapa ni mahali pa mfalme pa kuabudia na Hekalu la ufalme huu.”
14Amosi akamjibu Amazia, “Mimi sikuwa nabii wala mwana wa nabii, lakini nilikuwa mchungaji wa kondoo na mtunza mikuyu. 15Lakini Mwenyezi Mungu akanitoa kutoka kuchunga kondoo na kuniambia, ‘Nenda, ukawatabirie watu wangu Israeli.’ 16Sasa basi, sikieni neno la Mwenyezi Mungu. Ninyi mnasema,
“ ‘Usitabiri dhidi ya Israeli,
na uache kuhubiri dhidi ya nyumba ya Isaka.’
17“Kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“ ‘Mke wako atakuwa kahaba mjini,
nao wana wako wa kiume na wa kike watauawa kwa upanga.
Shamba lako litapimwa na kugawanywa,
na wewe mwenyewe utafia katika nchi ya kipagani.
Nayo Israeli kwa hakika itaenda uhamishoni,
mbali na nchi yao.’ ”

Iliyochaguliwa sasa

Amosi 7: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia