Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 11:5-20

Danieli 11:5-20 NENO

“Mfalme wa Kusini atakuwa na nguvu, lakini mmoja wa majemadari wake atakuwa na nguvu zaidi yake, naye atatawala ufalme wake mwenyewe kwa nguvu nyingi. Baada ya miaka kadhaa, wataungana. Binti ya mfalme wa Kusini ataolewa kwa mfalme wa Kaskazini ili kuimarisha mapatano, lakini nguvu za huyo binti hazitadumu; hata mfalme hatadumu wala nguvu zake. Katika siku hizo atafukuzwa, pamoja na hao wasindikizaji wake wa kifalme, na baba yake, na yeyote aliyemuunga mkono. “Mmoja kutoka jamaa ya huyo binti atainuka na kuchukua nafasi yake. Atashambulia majeshi ya mfalme wa Kaskazini na kuingia katika ngome yake; atapigana dhidi yao, naye atashinda. Tena ataitwaa miungu yao, vinyago vyao vya chuma, na vitu vyao vya thamani vya fedha na dhahabu, na kuvichukua hadi Misri. Kwa miaka kadhaa atamwacha mfalme wa Kaskazini bila kumsumbua. Kisha mfalme wa Kaskazini atashambulia nchi ya mfalme wa Kusini, lakini atarudi hadi kwenye nchi yake mwenyewe. Wana wa mfalme wa Kaskazini watajiandaa kwa vita na kukusanya jeshi kubwa, ambalo litafagia nchi kama mafuriko yasiyozuilika, na kuendelea na vita hadi kwenye ngome ya mfalme wa Kusini. “Kisha mfalme wa Kusini atatoka kwa ghadhabu na kupigana dhidi ya mfalme wa Kaskazini, ambaye atakusanya jeshi kubwa, lakini litashindwa. Jeshi litakapotekwa, mfalme wa Kusini atajawa na kiburi, na atachinja maelfu mengi; hata hivyo hatabaki na ushindi. Kwa maana mfalme wa Kaskazini atakusanya jeshi kubwa kuliko lile la kwanza; baada ya miaka kadhaa, atasonga mbele na jeshi kubwa mno lililoandaliwa vizuri. “Katika nyakati hizo, wengi watainuka dhidi ya mfalme wa Kusini. Watu wenye ghasia miongoni mwa watu wako mwenyewe wataasi ili kutimiza maono, lakini bila mafanikio. Ndipo mfalme wa Kaskazini atakuja na kuuzingira mji kwa majeshi, na kuuteka mji wa ngome. Majeshi ya Kusini yatakosa nguvu za kumzuia; naam, hata vikosi vyao vya askari vilivyo bora zaidi, havitakuwa na nguvu za kuwakabili. Huyo mvamia nchi atafanya apendavyo; hakuna yeyote atakayeweza kumpinga. Atajiimarisha katika Nchi ya Kupendeza, na atakuwa na uwezo wa kuiangamiza. Ataamua kuja na nguvu za ufalme wake wote, na kufanya mapatano ya amani na mfalme wa Kusini. Naye atamtoa binti yake aolewe naye ili kuuangusha ufalme, lakini mipango yake haitafanikiwa wala kumsaidia. Ndipo atabadili nia yake na kupigana na nchi za pwani na aziteke nyingi, lakini jemadari mmoja atakomesha ufidhuli wake, na kurudisha ufidhuli wake juu yake. Baada ya hili atazigeukia ngome za nchi yake mwenyewe, lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena. “Atakayetawala baada yake atamtuma mtoza ushuru ili kudumisha fahari ya kifalme. Hata hivyo, baada ya miaka michache ataangamizwa, lakini si katika hasira wala katika vita.