Danieli 11:5-20
Danieli 11:5-20 Biblia Habari Njema (BHN)
“ ‘Mfalme wa kusini atakuwa mwenye nguvu. Lakini mmoja wa majemadari wake atakuwa na nguvu kuliko yeye na utawala wake utakuwa mkubwa zaidi. Baada ya miaka kadhaa, watafanya mkataba; binti mfalme wa kusini ataolewa katika jamaa ya mfalme na kuratibisha huo mkataba; wa kaskazini, lakini hataendelea kuwa na nguvu, pia mfalme na wazawa wake hawatavumilia; na huyo binti, mwanawe na watumwa wa kike aliokwenda nao, wote watauawa. Baadaye, mmojawapo wa ukoo wa huyo binti atakuwa mfalme. Huyo atayashambulia majeshi ya mfalme wa kaskazini na kuingia katika ngome zao na kushinda. Atazibeba sanamu za kusubu za miungu yao na vyombo vya thamani vya fedha na dhahabu mpaka nchini Misri. Kwa muda wa miaka kadhaa, mfalme wa kusini hatamshambulia mfalme wa kaskazini. Lakini baadaye, mfalme huyu wa kaskazini atauvamia ufalme wa kusini, ila atalazimika kurudi katika nchi yake. “ ‘Wana wa mfalme wa kaskazini watakusanya jeshi kubwa na kujiandaa kwa vita. Jeshi hilo litasonga mbele kama mafuriko litapita na kupigana vita mpaka ngome ya adui. Hapo, mfalme wa kusini, kwa hasira yake, atapigana vita na mfalme wa kaskazini ambaye naye atamkabili kwa jeshi kubwa, lakini litashindwa. Baada ya kulishinda vibaya jeshi la kaskazini na kuua maelfu, ataanza kujisifu, ila hataendelea kuwa mshindi. “ ‘Maana mfalme wa kaskazini baadaye ataandaa jeshi kubwa kuliko lile la awali. Kisha baada ya miaka kadhaa atarudi na jeshi kubwa lenye vifaa vingi. Wakati huo watu wengi watamwasi mfalme wa kusini. Baadhi ya watu wakatili wa taifa lako Danieli, wataasi ili kutekeleza maono haya, lakini hawatafaulu. Ndipo mfalme wa kaskazini atauzingira mji wenye ngome imara na kuuteka. Wanajeshi wa kusini hawatastahimili, hata wale wateule, maana hawatakuwa na nguvu. Mvamizi atawatenda kama apendavyo, hakuna atakeyethubutu kupingana naye. Atasimama katika nchi tukufu, na nchi hiyo yote itakuwa chini ya mamlaka yake. “ ‘Huyo mvamizi atakusudia kuja na jeshi lake lote, naye atafanya mapatano na kuyatekeleza. Atamwoza binti mmoja ili kuuangamiza ufalme wa adui yake; lakini mpango wake hautafaulu, wala kumfaidia lolote. Baadaye, atazigeukia na kuzishambulia nchi nyingi za pwani na kuzishinda. Lakini jemadari mgeni atamshinda na kuyakomesha majivuno yake mwenyewe; naam, atamrudishia mfalme wa kaskazini majivuno yake mwenyewe. Hapo atageuka kurudi katika ngome za nchi yake mwenyewe, lakini atajikwaa na kuanguka vitani na huo ndio utakaokuwa mwisho wake. “ ‘Huyu atafuatwa na mfalme mwingine ambaye atatuma mtozaushuru kupitia katika fahari ya ufalme wake. Mfalme huyo atauawa baada ya siku chache, lakini si kwa hasira wala vitani.
Danieli 11:5-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na mfalme wa kusini atakuwa na nguvu; lakini mmoja wa maofisa wake atakuwa na nguvu zaidi kuliko yeye, na atatawala; himaya kubwa zaidi kuliko yeye. Na baada ya miaka kadhaa watashirikiana; kwa kuwa binti wa mfalme wa kusini atakuja kwa mfalme wa kaskazini, ili kufanya mapatano naye; lakini hatakuwa na nguvu za mkono wake sikuzote; wala mfalme yule hatasimama, wala mkono wake; lakini yule binti atatolewa, na hao waliomleta, na yeye aliyemzaa, na yeye aliyemtia nguvu, zamani zile. Lakini katika chipukizi la mizizi yake atasimama mmoja mahali pake atakayeliendesha jeshi la askari, naye ataingia katika ngome ya mfalme wa kaskazini, na kuwatenda mambo, na kuwashinda; na miungu yao, pamoja na sanamu zao, na vyombo vyao vizuri vya fedha na dhahabu atavichukua mpaka Misri; kisha atajizuia miaka kadhaa asimwendee mfalme wa kaskazini. Naye huyo ataingia katika ufalme wa mfalme wa kusini, lakini atarudi mpaka nchi yake mwenyewe. Na wanawe watafanya vita, na kukusanya mkutano wa majeshi makuu; watakaokuja na kufurika na kupita katikati; nao watarudi na kufanya vita mpaka penye ngome yake. Na mfalme wa kusini ataingiliwa na ghadhabu, naye atatoka na kupigana naye, yaani, na mfalme wa kaskazini; naye atapanga jeshi kubwa; na jeshi hilo litawekwa mikononi mwake. Atakapokwisha kuchukua lile jeshi, moyo wake utatukuzwa; naye atawaangusha makumi ya maelfu; lakini hataongezewa nguvu. Kwa maana mfalme wa kaskazini atarudi, naye atapanga jeshi kubwa kuliko lile la kwanza; naye hakika atakuja mwisho wa zamani zile, yaani, baada ya miaka kadhaa, pamoja na jeshi kubwa na mali nyingi. Na zamani zile watu wengi watasimama ili kumpinga mfalme wa kusini; pia, wenye jeuri miongoni mwa watu wako watajiinua ili kuyathibitisha maono; lakini wataanguka. Basi mfalme wa kaskazini atakuja, na kufanya kilima, na kuupiga mji wenye maboma; na silaha za kusini hazitaweza kumpinga, wala watu wake wateule, wala hapatakuwa na nguvu za kumpinga. Maana ajaye kupigana naye atatenda kadiri apendavyo, wala hapana mtu atakayesimama mbele yake; naye atasimama katika nchi ya uzuri, na uharibifu utakuwa mkononi mwake. Naye atakaza uso wake ili aje pamoja na nguvu zote za ufalme wake, naye atafanya mapatano naye; naye atatenda kadiri apendavyo; naye atampa binti amuoe, ili hatimaye amwangamize huyo mfalme; lakini hataweza kumwangamiza. Baada ya hayo atauelekeza uso wake kwenye visiwa, naye atavipiga visiwa vingi; lakini mkuu mmoja ataikomesha aibu iliyoletwa na yeye; naam, aibu yake hiyo atamrudishia mwenyewe. Ndipo atauelekeza uso wake kwenye ngome za nchi yake mwenyewe; lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena. Ndipo badala yake atasimama mmoja, atakayepitisha mwenye kutoza ushuru kati ya utukufu wa ufalme wake; lakini katika muda wa siku chache ataangamizwa, si kwa hasira, wala si katika vita.
Danieli 11:5-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na mfalme wa kusini atakuwa hodari; na mmoja wa wakuu wake atakuwa hodari kuliko yeye, naye atakuwa na mamlaka; mamlaka yake itakuwa mamlaka kubwa. Na baada ya miaka kadha wa kadha watashirikiana; kwa kuwa binti wa mfalme wa kusini atakuja kwa mfalme wa kaskazini, ili kufanya mapatano naye; lakini hatakuwa na nguvu za mkono wake sikuzote; wala mfalme yule hatasimama, wala mkono wake; lakini yule binti atatolewa, na hao waliomleta, na yeye aliyemzaa, na yeye aliyemtia nguvu, zamani zile. Lakini katika chipukizi la mizizi yake atasimama mmoja mahali pake atakayeliendesha jeshi la askari, naye ataingia katika ngome ya mfalme wa kaskazini, na kuwatenda mambo, na kuwashinda; na miungu yao, pamoja na sanamu zao, na vyombo vyao vizuri vya fedha na dhahabu atavichukua mpaka Misri; kisha atajizuia miaka kadha wa kadha asimwendee mfalme wa kaskazini. Naye huyo ataingia katika ufalme wa mfalme wa kusini, lakini atarudi mpaka nchi yake mwenyewe. Na wanawe watafanya vita, na kukusanya mkutano wa majeshi makuu; watakaokuja na kufurika na kupita katikati; nao watarudi na kufanya vita mpaka penye ngome yake. Na mfalme wa kusini ataingiliwa na ghadhabu, naye atatoka na kupigana naye, yaani, na mfalme wa kaskazini; naye atapanga jeshi kubwa; na jeshi hilo litawekwa mikononi mwake. Atakapokwisha kuchukua lile jeshi, moyo wake utatukuzwa; naye atawaangusha makumi elfu; lakini hataongezewa nguvu. Kwa maana mfalme wa kaskazini atarudi, naye atapanga jeshi kubwa kuliko lile la kwanza; naye hakika atakuja mwisho wa zamani zile, yaani, baada ya miaka kadha wa kadha, pamoja na jeshi kubwa na mali nyingi. Na zamani zile watu wengi watasimama ili kumpinga mfalme wa kusini; pia, wenye jeuri miongoni mwa watu wako watajiinua ili kuyathibitisha maono; lakini wataanguka. Basi mfalme wa kaskazini atakuja, na kufanya kilima, na kuupiga mji wenye maboma; na silaha za kusini hazitaweza kumpinga, wala watu wake wateule, wala hapatakuwa na nguvu za kumpinga. Maana ajaye kupigana naye atatenda kadiri apendavyo, wala hapana mtu atakayesimama mbele yake; naye atasimama katika nchi ya uzuri, na uharibifu utakuwa mkononi mwake. Naye atakaza uso wake ili aje pamoja na nguvu zote za ufalme wake, naye atafanya mapatano naye; naye atatenda kadiri apendavyo; naye atampa binti wa watu ili amharibu; lakini hilo halitasimama wala kumfaa. Baada ya hayo atauelekeza uso wake kwenye visiwa, naye atavipiga visiwa vingi; lakini mkuu mmoja ataikomesha aibu iliyoletwa na yeye; naam, aibu yake hiyo atamrudishia mwenyewe. Ndipo atauelekeza uso wake kwenye ngome za nchi yake mwenyewe; lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena. Ndipo badala yake atasimama mmoja, atakayepitisha mwenye kutoza ushuru kati ya utukufu wa ufalme wake; lakini katika muda wa siku chache ataangamizwa, si kwa hasira, wala si katika vita.
Danieli 11:5-20 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Mfalme wa Kusini atakuwa na nguvu, lakini mmoja wa majemadari wake atakuwa na nguvu zaidi yake, naye atatawala ufalme wake mwenyewe kwa nguvu nyingi. Baada ya miaka kadhaa, wataungana. Binti ya mfalme wa Kusini ataolewa kwa mfalme wa Kaskazini ili kuimarisha mapatano, lakini nguvu za huyo binti hazitadumu; hata mfalme hatadumu wala nguvu zake. Katika siku hizo atafukuzwa, pamoja na hao wasindikizaji wake wa kifalme, na baba yake, na yeyote aliyemuunga mkono. “Mmoja kutoka jamaa ya huyo binti atainuka na kuchukua nafasi yake. Atashambulia majeshi ya mfalme wa Kaskazini na kuingia katika ngome yake; atapigana dhidi yao, naye atashinda. Tena ataitwaa miungu yao, vinyago vyao vya chuma, na vitu vyao vya thamani vya fedha na dhahabu, na kuvichukua hadi Misri. Kwa miaka kadhaa atamwacha mfalme wa Kaskazini bila kumsumbua. Kisha mfalme wa Kaskazini atashambulia nchi ya mfalme wa Kusini, lakini atarudi hadi kwenye nchi yake mwenyewe. Wana wa mfalme wa Kaskazini watajiandaa kwa vita na kukusanya jeshi kubwa, ambalo litafagia nchi kama mafuriko yasiyozuilika, na kuendelea na vita hadi kwenye ngome ya mfalme wa Kusini. “Kisha mfalme wa Kusini atatoka kwa ghadhabu na kupigana dhidi ya mfalme wa Kaskazini, ambaye atakusanya jeshi kubwa, lakini litashindwa. Jeshi litakapotekwa, mfalme wa Kusini atajawa na kiburi, na atachinja maelfu mengi; hata hivyo hatabaki na ushindi. Kwa maana mfalme wa Kaskazini atakusanya jeshi kubwa kuliko lile la kwanza; baada ya miaka kadhaa, atasonga mbele na jeshi kubwa mno lililoandaliwa vizuri. “Katika nyakati hizo, wengi watainuka dhidi ya mfalme wa Kusini. Watu wenye ghasia miongoni mwa watu wako mwenyewe wataasi ili kutimiza maono, lakini bila mafanikio. Ndipo mfalme wa Kaskazini atakuja na kuuzingira mji kwa majeshi, na kuuteka mji wa ngome. Majeshi ya Kusini yatakosa nguvu za kumzuia; naam, hata vikosi vyao vya askari vilivyo bora zaidi, havitakuwa na nguvu za kuwakabili. Huyo mvamia nchi atafanya apendavyo; hakuna yeyote atakayeweza kumpinga. Atajiimarisha katika Nchi ya Kupendeza, na atakuwa na uwezo wa kuiangamiza. Ataamua kuja na nguvu za ufalme wake wote, na kufanya mapatano ya amani na mfalme wa Kusini. Naye atamtoa binti yake aolewe naye ili kuuangusha ufalme, lakini mipango yake haitafanikiwa wala kumsaidia. Ndipo atabadili nia yake na kupigana na nchi za pwani na aziteke nyingi, lakini jemadari mmoja atakomesha ufidhuli wake, na kurudisha ufidhuli wake juu yake. Baada ya hili atazigeukia ngome za nchi yake mwenyewe, lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena. “Atakayetawala baada yake atamtuma mtoza ushuru ili kudumisha fahari ya kifalme. Hata hivyo, baada ya miaka michache ataangamizwa, lakini si katika hasira wala katika vita.