Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 28:30-44

Kumbukumbu 28:30-44 NENO

Utaposa mke, lakini mtu mwingine atakutana naye kimwili. Utajenga nyumba, lakini hutaishi ndani yake. Utapanda shamba la mizabibu, lakini hutakula matunda yake. Ng’ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako lakini hutakula nyama yake. Punda wako atachukuliwa kwa nguvu kutoka kwako wala hatarudishwa. Kondoo wako watapewa adui zako, wala hakuna mtu yeyote wa kuwaokoa. Wanao wa kiume na wa kike watatolewa kwa mataifa mengine, nawe utayachosha macho yako ukiwatazamia siku baada ya siku, hutakuwa na nguvu kuinua mkono. Taifa usilolijua watakula mazao ya nchi yako na taabu ya kazi yako, hutakuwa na chochote, bali kuonewa kikatili siku zako zote. Vitu utakavyoviona kwa macho yako vitakufanya wazimu. Mwenyezi Mungu atayapiga magoti yako na miguu yako kwa majipu yenye maumivu makali yasiyoponyeka, yakienea kutoka nyayo za miguu yako hadi utosini. Mwenyezi Mungu atakupeleka wewe na mfalme uliyemweka juu yako uende kwenye taifa ambalo hukulijua wewe wala baba zako. Huko utaabudu miungu mingine, miungu ya miti na mawe. Utakuwa kitu cha kuchukiza, tena kitu cha kudharauliwa na kudhihakiwa kwa mataifa yote huko Mwenyezi Mungu atakakokupeleka. Utapanda mbegu nyingi katika shamba lakini utavuna haba, kwa sababu nzige watazila. Utapanda mashamba ya mizabibu na kuyapalilia, lakini hutakunywa divai yake wala hutakusanya zabibu, kwa sababu wadudu watazila. Utakuwa na mizeituni katika nchi yako yote, lakini hutatumia hayo mafuta yake, kwa sababu zeituni zitapukutika. Utakuwa na wana wa kiume na wa kike, lakini hawatakuwa nawe, kwa sababu watachukuliwa mateka. Makundi ya nzige yatavamia miti yako yote na mazao ya nchi yako. Mgeni anayeishi miongoni mwako atazidi kuinuka juu yako, lakini wewe utaendelea kushuka chini zaidi. Yeye atakukopesha, lakini wewe hutamkopesha. Yeye atakuwa kichwa, lakini wewe utakuwa mkia.