Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 29:14-29

Kumbukumbu 29:14-29 NENO

Ninafanya agano hili pamoja na kiapo chake, sio na ninyi tu mnaosimama hapa na sisi leo mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, bali pia pamoja na wale ambao hawapo hapa leo. Ninyi wenyewe mnajua jinsi tulivyoishi nchini Misri na jinsi tulivyopita katikati ya nchi hadi tukafika hapa. Mliona miongoni mwao machukizo yao, na sanamu za miti na mawe, za fedha na dhahabu. Hakikisheni kwamba hakuna mwanaume au mwanamke, ukoo au kabila miongoni mwenu leo ambalo moyo wake utamwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwenda kuabudu miungu ya mataifa hayo. Hakikisheni hakuna mzizi miongoni mwenu unaotoa sumu chungu ya namna hii. Mtu wa namna hii asikiapo maneno ya kiapo hiki, hujibariki mwenyewe, na kisha hufikiri, “Nitakuwa salama, hata nikiendelea kuifuata njia yangu mwenyewe.” Hili litaleta maafa juu ya nchi iliyoneshewa sawasawa na nchi kame. Mwenyezi Mungu kamwe hatakuwa radhi kumsamehe, ghadhabu na wivu wa Mungu vitawaka dhidi ya mtu huyo. Laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki zitamwangukia na Mwenyezi Mungu atafuta jina lake chini ya mbingu. Mwenyezi Mungu atamtwaa peke yake kutoka makabila ya Israeli kwa maangamizi, kulingana na laana zote za agano zilizoandikwa kwenye Kitabu hiki cha Torati. Watoto wako watakaofuata baada yako katika vizazi vya baadaye na wageni ambao watakuja kutoka nchi za mbali, wataona maafa, yaliyoipata nchi na magonjwa ambayo Mwenyezi Mungu aliyaleta juu yake. Nchi yote itakuwa jaa linaloungua la chumvi na kiberiti: hakutakuwa kilichopandwa, hakutakuwa kinachochipua, wala hakutakuwa na mimea inayoota juu yake. Itakuwa kama maangamizi ya Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, ambazo Mwenyezi Mungu aliangamiza kwa hasira kali. Mataifa yote yatauliza: “Kwa nini Mwenyezi Mungu ameifanya hivi nchi hii? Kwa nini hasira hii kali ikawaka?” Na jibu litakuwa: “Ni kwa sababu watu hawa waliacha agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, agano alilofanya nao alipowatoa katika nchi ya Misri. Walienda zao na kuabudu miungu mingine na kuisujudia, miungu wasioijua, miungu ambayo Mungu hakuwapa. Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya nchi hii, hivyo Mungu akaleta juu yake laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki. Katika hasira kali na katika ghadhabu kuu Mwenyezi Mungu aliwang’oa kutoka nchi yao na kuwasukumia katika nchi nyingine, kama ilivyo sasa.” Mambo ya siri ni ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, bali yaliyofunuliwa ni yetu na watoto wetu milele, ili tuweze kuyafanya maneno yote ya sheria hii.