Kutoka 1
1
Waisraeli wagandamizwa
1Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli waliokwenda Misri pamoja na Yakobo, kila mmoja na jamaa yake:
2Reubeni, Simeoni, Lawi na Yuda;
3Isakari, Zabuloni na Benyamini;
4Dani na Naftali, Gadi na Asheri.
5Wazao wote wa Yakobo walikuwa watu sabini; Yusufu alikuwa tayari yuko Misri.
6Basi Yusufu na kaka zake wote na kizazi kile chote walikufa, 7lakini Waisraeli walikuwa wamezaana na kuongezeka sana, idadi yao ikawa kubwa mno, hadi wakaijaza nchi.
8Kisha mfalme mwingine ambaye hakufahamu habari za Yusufu akatawala Misri. 9Akawaambia watu wake, “Tazameni, Waisraeli wamekuwa wengi mno kwa idadi kuliko sisi. 10Njooni, ni lazima tuwashughulikie kwa uangalifu, la sivyo watazidi kuwa wengi zaidi, na ikiwa patatokea vita, watajiunga na adui zetu kupigana nasi, na kuondoka katika nchi hii.”
11Basi Wamisri wakaweka wasimamizi wa kuwasimamia na kuwatesa Waisraeli kwa kazi ngumu, nao wakajenga miji ya Pithomu na Ramesesi ya kuweka akiba ya Farao. 12Lakini walivyozidi kuteswa, ndivyo walivyozidi kuongezeka na kuenea katika nchi. Wamisri wakawaogopa Waisraeli, 13kwa hiyo wakawatumikisha kwa ukatili. 14Wakafanya maisha ya Waisraeli kuwa machungu kwa kufanya kazi ngumu ya kutengeneza lami na kufyatua matofali, na kazi zote za mashambani; katika kazi zao zote ngumu, Wamisri waliwatumia Waisraeli kwa ukatili.
15Mfalme wa Misri akawaita wakunga waliowazalisha Waebrania, ambao majina yao yalikuwa Shifra na Pua, akawaambia, 16“Mtakapowazalisha wanawake Waebrania, chunguzeni wanapojifungua. Ikiwa ni mtoto wa kiume, muueni; lakini ikiwa ni msichana, mwacheni aishi.” 17Lakini hao wakunga walimcha Mungu na hawakufanya kile mfalme wa Misri alichowaambia kufanya, bali wakawaacha watoto wa kiume waishi. 18Ndipo mfalme wa Misri akawaita hao wakunga, akawauliza, “Kwa nini mmefanya hivi? Mbona mmeacha watoto wa kiume waishi?”
19Wakunga wakamjibu Farao, “Wanawake wa Waebrania ni tofauti na wanawake wa Misri; wao wana nguvu, nao hujifungua watoto kabla wakunga hawajafika.”
20Kwa hiyo Mungu akawatendea mema wakunga hao. Waisraeli wakaongezeka na kuendelea kuwa wengi zaidi. 21Kwa vile hao wakunga walimcha Mungu, Mungu akawajalia kuwa na jamaa zao wenyewe.
22Kisha Farao akatoa agizo hili kwa watu wake wote: “Kila mtoto wa kiume atakayezaliwa kwa Waebrania lazima atupwe katika Mto Naili, bali kila mtoto wa kike aachwe aishi.”
Iliyochaguliwa sasa
Kutoka 1: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.