Kutoka 2
2
Kuzaliwa kwa Musa
1Basi mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaoa mwanamke Mlawi, 2naye mwanamke huyo akapata mimba, akazaa mtoto wa kiume. Alipoona mtoto huyo ni mzuri, akamficha kwa miezi mitatu. 3Lakini alipoona hawezi kuendelea kumficha, akamtengenezea kisafina cha mafunjo, akakipaka lami. Kisha akamweka huyo mtoto ndani yake, akakificha kwenye matete kando ya ukingo wa Mto Naili. 4Dada ya huyo mtoto akasimama mbali ili kuona kitakachompata mtoto.
5Ndipo binti Farao akateremka kwenye Mto Naili kuoga, nao wahudumu wake wakawa wanatembea ukingoni mwa mto. Binti Farao akaona kisafina kwenye matete, akamtuma mmoja wa wajakazi wake kukichukua. 6Alifungua kisafina akaona mtoto ndani yake. Mtoto alikuwa akilia, akamhurumia. Akasema, “Huyu ni mmoja wa watoto wa Waebrania.”
7Ndipo dada wa huyo mtoto akamuuliza binti Farao, “Je, niende nikakutafutie mmoja wa wanawake wa Waebrania akulelee huyu mtoto?”
8Binti Farao akamjibu, “Ndiyo, nenda.” Yule msichana akaenda akamleta mama wa mtoto. 9Binti Farao akamwambia, “Mchukue huyu mtoto unisaidie kumlea, nami nitakulipa.” Basi yule mwanamke akamchukua mtoto na kumlea. 10Mtoto alipokua, akampeleka kwa binti Farao, naye akawa mwanawe. Akamwita jina Musa, akisema, “Nilimtoa kwenye maji.”
Musa akimbilia Midiani
11Siku moja, Musa alipokuwa mtu mzima, alienda mahali walipokuwa ndugu zake, na akaona jinsi walivyokuwa wakifanyishwa kazi ngumu. Akamwona Mmisri akimpiga Mwebrania, mmoja wa watu wake. 12Musa akatazama huku na huko asione mtu yeyote, akamuua yule Mmisri, akamficha kwenye mchanga. 13Kesho yake akatoka, akaona Waebrania wawili wakipigana. Akamuuliza yule aliyekosa, “Mbona unampiga Mwebrania mwenzako?”
14Yule mtu akamjibu, “Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri?” Ndipo Musa akaogopa na kuwaza, “Jambo lile nililofanya lazima limefahamika.”
15Farao aliposikia jambo hili, alijaribu kumuua Musa, lakini Musa akamkimbia Farao na kwenda kuishi katika nchi ya Midiani, akaketi kando ya kisima. 16Kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja kisimani ili kuchota maji na kujaza birika kwa ajili ya kunyweshea mifugo ya baba yao. 17Baadhi ya wachungaji wakaja wakawafukuza hao wasichana. Ndipo Musa akainuka, akawasaidia kunywesha mifugo yao.
18Wasichana hao waliporudi nyumbani, baba yao Reueli akawauliza, “Imekuwaje leo mmerudi mapema hivyo?”
19Wakamjibu, “Mmisri mmoja alituokoa kutoka mikono ya wachungaji. Pia mtu huyo alituchotea maji na kunywesha mifugo.”
20Akawauliza binti zake, “Yuko wapi? Mbona mmemwacha? Mkaribisheni ale chakula.”
21Musa akakubali kukaa kwa huyo mtu, ambaye alimpa Musa binti yake aliyeitwa Sipora amwoe. 22Sipora alizaa mtoto wa kiume, naye Musa akamwita jina Gershomu, akisema, “Nimekuwa mgeni katika nchi ya kigeni.”
23Baada ya muda mrefu, mfalme wa Misri akafa. Waisraeli wakalia kwa huzuni katika utumwa wao, walilia na kilio chao cha kutaka msaada kwa ajili ya utumwa kikamfikia Mungu. 24Mungu akasikia kilio chao cha huzuni, akakumbuka agano alilofanya na Ibrahimu pamoja na Isaka na Yakobo. 25Kwa hiyo Mungu akawaangalia Waisraeli na kuwahurumia.
Iliyochaguliwa sasa
Kutoka 2: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.