Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 14

14
Kuvuka Bahari ya Shamu
1Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 2“Waambie Waisraeli wageuke nyuma na wapige kambi karibu na Pi-Hahirothi, kati ya Migdoli na bahari. Watapiga kambi kando ya bahari, mkabala na Baal-Sefoni. 3Farao atafikiri kwamba, ‘Hao Waisraeli wanatangatanga katika nchi kwa kuchanganyikiwa, nalo jangwa limewafungia.’ 4Nami nitaufanya moyo wa Farao mgumu, naye atawafuatilia. Lakini nitajipatia utukufu kwa ajili yangu mwenyewe kupitia Farao na jeshi lake lote, nao Wamisri watajua kuwa mimi ndimi Mwenyezi Mungu.” Kwa hiyo Waisraeli wakafanya hivyo.
5Mfalme wa Misri alipoambiwa kuwa Waisraeli wamekimbia, Farao na maafisa wake wakabadili nia zao kuhusu Waisraeli, wakasema, “Tumefanya nini? Tumewaachia Waisraeli waende zao na tumeukosa utumishi wao!” 6Kwa hiyo akaandaliwa gari lake la vita, naye akaenda pamoja na jeshi lake. 7Akachukua magari ya vita mia sita bora, pamoja na magari ya vita mengine yote ya Misri, pamoja na maafisa wa magari hayo yote. 8Mwenyezi Mungu akaufanya moyo wa Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, kwa hiyo akawafuatia Waisraeli, waliokuwa wakiondoka Misri kwa ujasiri. 9Nao Wamisri, yaani farasi wote wa Farao na magari ya vita, wapanda farasi na vikosi vya askari, wakawafuatia Waisraeli, wakawakuta karibu na Pi-Hahirothi, mkabala na Baal-Sefoni walipokuwa wamepiga kambi kando ya bahari.
10Farao alipokaribia, Waisraeli wakainua macho yao, wakawaona Wamisri wakija nyuma yao. Wakashikwa na hofu, wakamlilia Mwenyezi Mungu. 11Wakamwambia Musa, “Je, ni kwamba hakukuwa na makaburi huko Misri hata umetuleta tufe huku jangwani? Umetufanyia nini kututoa Misri? 12Hatukukuambia tulipokuwa huko Misri, ‘Tuache tuwatumikie Wamisri’? Ingekuwa vyema zaidi kwetu kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani!”
13Musa akawajibu Waisraeli, “Msiogope. Simameni imara, nanyi mtauona wokovu Mwenyezi Mungu atakaowapatia leo. Hao Wamisri mnaowaona leo kamwe hamtawaona tena. 14Mwenyezi Mungu atawapigania ninyi, nanyi mnatakiwa kutulia tu.”
15Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Kwa nini wewe unanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele. 16Inua fimbo yako na unyooshe mkono wako juu ya bahari ili kuyagawa maji, ili Waisraeli wapate kupita mahali pakavu baharini. 17Nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu kusudi waingie baharini wakiwafuatia. Nami nitajipatia utukufu kupitia Farao pamoja na jeshi lake lote, kupitia magari yake ya vita na wapanda farasi wake. 18Nao Wamisri watajua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu nitakapojipatia utukufu kupitia Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake.”
19Ndipo malaika wa Mungu, aliyekuwa akisafiri mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akakaa nyuma yao. Pia ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao na kusimama nyuma, 20ikakaa kati ya majeshi ya Misri na Israeli. Usiku kucha wingu likaleta giza upande mmoja na nuru kwa upande mwingine, kwa hiyo hakuna aliyemkaribia mwenzake usiku kucha.
21Ndipo Musa akanyoosha mkono wake juu ya bahari, naye Mwenyezi Mungu akayasukuma maji ya bahari nyuma kwa upepo mkali wa mashariki usiku ule wote na kupafanya nchi kavu. Maji yakagawanyika, 22nao Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, maji yakiwa ukuta upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto.
23Wamisri wakawafuatia ndani ya bahari, pamoja na farasi wote wa Farao, magari ya vita na wapanda farasi. 24Kukaribia mapambazuko, Mwenyezi Mungu akaliangalia jeshi la Wamisri kutoka ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha. 25Mungu akayaondoa magurudumu ya magari yao ya vita, kwa hivyo wakayaendesha kwa shida. Nao Wamisri wakasema, “Tuachane na Waisraeli! Mwenyezi Mungu anawapigania dhidi ya Misri.”
Wafuatiaji wazama
26Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nyoosha mkono wako juu ya bahari ili maji yarudi yawafunike Wamisri, magari yao ya vita, na wapanda farasi wao.” 27Musa akanyoosha mkono wake juu ya bahari, kulipopambazuka bahari ikarudi mahali pake. Wamisri wakajaribu kuyakimbia maji, lakini Mwenyezi Mungu akawasukumia ndani ya bahari. 28Maji yakarudiana na kuyafunika magari ya vita na wapanda farasi pamoja na jeshi lote la Farao lililokuwa limewafuata Waisraeli ndani ya bahari. Hakuna hata mmoja wao aliyenusurika.
29Lakini Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, ukiwepo ukuta wa maji upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto. 30Siku ile Mwenyezi Mungu akawaokoa Waisraeli kutoka mikononi mwa Wamisri, nao Waisraeli wakawaona Wamisri wamelala ufuoni mwa bahari wakiwa wamekufa. 31Basi Waisraeli walipoona uwezo mkubwa Mwenyezi Mungu aliodhihirisha dhidi ya Wamisri, watu wakamwogopa Mwenyezi Mungu na wakaweka tumaini lao kwake na kwa Musa mtumishi wake.

Iliyochaguliwa sasa

Kutoka 14: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia