Kutoka 15:22-27
Kutoka 15:22-27 NENO
Kisha Musa akawaongoza Israeli kutoka Bahari ya Shamu na kuingia katika Jangwa la Shuri. Kwa siku tatu walisafiri jangwani bila kupata maji. Walipofika Mara, hawakuweza kunywa maji yake kwa sababu yalikuwa machungu. (Ndiyo sababu mahali hapo panaitwa Mara.) Kwa hiyo watu wakamnung’unikia Musa, wakisema, “Tunywe nini?” Ndipo Musa akamlilia Mwenyezi Mungu, naye Mwenyezi Mungu akamwonesha kipande cha mti. Akakitupa ndani ya maji, nayo maji yakawa matamu. Huko Mwenyezi Mungu akawapa amri na sheria na huko akawajaribu. Mungu akasema, “Mkisikiliza kwa makini sauti ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kuyafanya yaliyo mema machoni pake, na mkiyatii maagizo yake na kuzishika amri zake zote, sitaleta juu yenu ugonjwa wowote niliowaletea Wamisri, kwa kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, niwaponyaye.” Kisha wakafika Elimu, mahali palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na miti sabini ya mitende, wakapiga kambi huko karibu na maji.